Papa Leo XIV: Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Ushirika, Ukarimu, Upendo na Amani
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu ni mkate na kinywaji kilichoshuka kutoka mbinguni kwa ajili ya maisha ya uzima wa milele; ni sadaka ya Kristo mwenyewe kwa ajili ya binadamu! Huyu ni Mwana wa mtu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni Mwana Kondoo wa Pasaka, anayemkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na hivyo kumwongoza katika Nchi ya ahadi. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Kristo Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau akiwafafanulia Maandiko Matakatifu! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha; na hatimaye, kuwaunga mkono katika mchakato wa mapambano ya kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano.
Katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anajisadaka mwenyewe kama nguvu ya maisha ya kiroho ili kuwajengea uwezo wafuasi wake wa kumwilisha Amri ya upendo: kwa kupenda kama alivyopenda Yeye mwenyewe; kwa kujenga na kudumisha jumuiya inayomsimikwa katika: Upendo na ukarimu, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, wanyonge na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kulishwa na Kristo Yesu kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu ni kujiaminisha kwake na kumwachia nafasi ili aweze kuwaongoza. Huu ni mwaliko wa kumpokea na kumpatia Kristo Yesu nafasi ya kwanza katika maisha, tayari kupokea na kumwilisha upendo unaobubujika kutoka katika umoja wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, dhamana ya Roho Mtakatifu anayerutubisha na kuimarisha upendo kwa Mungu na jirani; watu wanaokutana nao kila siku ya maisha yao! Kwa kulishwa na kunyweshwa Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, waamini wanakuwa kweli ni sehemu ya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kwa kuhamasishwa kujenga na kudumisha umoja na upendo vinavyobubujika kutoka katika Fumbo la Ekaristi Takatifu kama ambavyo waamini wanavyokumbushwa na Mtakatifu Paulo, Mtume kwamba Ekaristi Takatifu ni kifungo cha upendo na umoja.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu: Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, Baba Mtakatifu Leo XIV wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 22 Juni 2025 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, Mama Kanisa sehemu mbalimbali za dunia anaadhimisha Sherehe ya Fumbo la Ekaristi Takatifu: Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu: “Corpus Domini.” Mwinjili Luka anasimulia muujiza wa Kristo Yesu kuwalisha watu mia tano kwa mikate mitano na samaki mawili, watu wakala, wakashiba na hatimaye, wakakusanya vikapu kumi na viwili. Rej. Lk 9: 11-17. Hii ni alama inayowakumbusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, zawadi ya Mungu, hata kama ni kidogo kiasi gani, lakini, watu wanaposhirikishwa, inaongezeka maradufu. Zawadi ya Mungu ni chemchemi ya huruma na upendo wake wa daima. Mwenyezi Mungu ni Muumbaji chanzo cha maisha ya binadamu, amesadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu ameshiriki maisha ya binadamu katika udhaifu wake, isipokuwa hakuwa na dhambi, akateswa na hatimaye akafa Msalabani! Kristo Yesu ameshiriki umaskini wa binadamu, akajinyenyekesha katika huduma ya upendo.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kuna furaha kubwa pale mtu anapothamini zawadi anayokirimiwa. Ni katika muktadha huu, wa Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi anakuwa ni kiungo kati ya waamini na Mwenyezi Mungu. Kristo anakuja kupokea, kutakatifuza na kubariki Mkate na Divai; kazi ya mikono ya wanadamu inayotolewa Altareni sanjari na maisha ya waamini, ili yageuzwe kuwa ni Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu; Sadaka ya upendo inayotolewa kwa ajili ya wokovu wa walimwengu. Mwenyezi Mungu anaungana na waja wake, huku akipokea kwa furaha sadaka na majitoleo ya waamini wake; mwaliko kwa waamini kuungana na Mwenyezi Mungu kushirikishana na walimwengu hii furaha inayobubujika kutoka katika zawadi yake ya upendo. Mtakatifu Augustino anasema, chembechembe za ngano zinapounganika kwa pamoja, zinatengeneza Mkate mmoja na kwamba, amani na maridhiano katika upendo, yanaunda Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Baba Mtakatifu Leo XVI amehitimisha tafakari yake Sherehe ya Fkupigieumbo la Ekaristi kwa kusema kwamba, Maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu yanafumbatwa katika: Ibada ya Misa Takatifu, Maandamano ya Ekaristi Takatifu kuzunguka mitaa ya Roma na hatimaye, watapata fursa ya Kumwabudu Kristo Yesu katika Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu, mbele ya Kanisa kuu la Bikira Mkuu Jimbo kuu la Roma, ili kuomba neema na baraka kwa ajili ya nyumba, familia na kwa ajili ya binadamu wote. Huu ni mwaliko kwa waamini kila siku wanaposhiriki Fumbo la Ekaristi Takatifu, kuwa ni alama angavu ya dhamana ya waamini kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli vyombo na mashuhuda wa ushirika, amani, ukarimu na upendo kwa jirani zao.