Papa Leo XIV: Wakristo Wote Wanaitwa na Kutumwa Kushuhudia na Kutangaza Injili
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa linalosafiri duniani, kwa tabia yake ni la kimisionari, sababu limepata asili yake katika kutumwa kwa Mungu Mwana na kutumwa kwa Roho Mtakatifu, kufuatana na azimio la Mungu Baba, chemchemi ya huruma na upendo, ili kuwatangazia watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Kristo Yesu alilisimika Kanisa lake kama Sakramenti ya wokovu na hivyo kuwatuma Mitume wake wakaihubiri Injili kwa watu wote wa Mataifa, kwa Sakramenti na vyombo vingine vya neema, lipate kuwaongoza watu kufikia imani, uhuru na amani ya Kristo Yesu, na hivyo liwaandalie njia nyeupe na thabiti ifikishayo kwenye kushiriki kikamilifu Fumbo la Kristo Yesu. Rej. AG. 1- 9. Tena waamini wanakumbushwa na Kristo Yesu kwamba, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache; basi mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake.” Lk 10:2. Kanisa linaendelea kujitahidi kutafakari kwa kina na mapana kuhusu: Ukuu na utakatifu wa Fumbo la wito, maisha na utume wa Kipadre na Maisha ya kuwekwa wakfu, ili kuweka bayana, thamani yake isiyoweza kupimika kwa mizani ya kibinadamu. Lengo ni: kulinda, kuhifadhi na kudumisha usafi na utakatifu wake kama wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa. Jambo la msingi kwa Mapadre na watawa ni kutambua kwamba, Kanisa linawahimiza kuwa kweli ni watumishi waaminifu, watakaomuakisi Kristo fukara, Kristo mtii na Kristo msafi katika useja! Mapadre na watawa wanapaswa kukumbuka kwamba, wao ni zawadi ya Mungu kwa Kanisa linaloendelea kuhitaji watenda kazi: wema, watakatifu, wachamungu na wachapakazi na hodari, kwa maneno mengine, mashuhuda wenye mvuto na mashiko kama sehemu muhimu sana ya mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Dominika tarehe 6 Julai 2025 amegusia umuhimu wa utume wa Wakristo wote wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia kila mtu kwa kadiri wito, karama na mazingira anamoishi. Injili inasimulia kuhusu kutumwa kwa wanafunzi Sabini na wawili ili kumtayarishia njia Kristo Yesu katika vijiji na mahali atakapopita. Yesu anawapa maagizo mahususi ya kiutendaji kabla ya kuanza utume wao wa kutangaza Habari Njema ya wokovu. Maagizo haya yamekusudiwa kuwaongoza katika utume huu, na pia kuwakumbusha kwamba hatimaye, ni kazi ya Mungu na wao ni vyombo vyake tu. Kwa hiyo wanapaswa daima kubaki wanyenyekevu, watulivu na kumtegemea Mungu kabisa katika shughuli zao za kimisionari ili hatimaye, watu wengi zaidi waweze kufikia upendo wa Mungu na hivyo kukombolewa. Kwa upande mmoja anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, Mungu katika ukarimu wake ndiye mpandaji wa mbegu hii katika moyo wa binadamu na katika historia yake, ili mwanadamu apate ukamilifu wa maisha na kuokolewa na kumweka huru, ndiyo maana Kristo Yesu anasema, mavuno ni mengi lakini watenda kazi ni wachache. Huu ni Ufalme wa Mungu unaoendelea kuchipua sehemu mbalimbali za dunia, lakini inasikitisha kuona kwamba, binadamu katika ulimwengu mambo leo “ameugeuzia kisogo” kiasi kwamba, mwanadamu anajikuta akiwa amezingirwa na mambo mengi; wanaendelea kusubiri utabiri kuhusu ukweli mkuu, hata kama kwa sasa binadamu anaonekana kumezwa na masuala mengine, lakini bado wanaendelea kujikita katika mchakato wa kutafuta ukamilifu wa maisha yao, wana kiu na hamu ya haki pamoja na maisha ya uzima wa milele.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna uhaba mkubwa wa watenda kazi katika shamba la Bwana, bado hawajatambua: “Tazama, mimi nawaambieni, Inueni macho yenu myatazame mashamba, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno. Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja. Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine. Mimi naliwatuma myavune yale msiyoyataabikia; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao.” Yn 4: 35-38. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu anapenda kutenda jambo kubwa katika maisha ya waamini wake na ulimwenguni kote katika ujumla wake. Bahati mbaya sana kwamba, ni watu wachache ambao wametambua jambo hili, tayari wanajishughulisha kuipokea zawadi hii, kwa kuitangaza, kuishuhudia na kuwarithisha jirani zao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, walimwengu wanataka kuwaona mashuhuda, vyombo na watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu, wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika shamba la Bwana, wakiwa na ari na upendo, tayari kutangaza na kushuhudia Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: Kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Walimwengu wasingependa kuwaona watenda kazi wanaoibuka, ili kutumia fursa, ili kuonesha hali yao ya maisha, au kwa kushiriki katika matukio mbalimbali ya imani. Kuna watu wachache ambao usiku na mchana wanaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, huku wakiendelea kupalilia ile mbegu njema iliyopandwa nyoyoni mwao, kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwenye familia, mahali pa kazi, shuleni na katika medani mbalimbali za maisha ya mwanadamu, anayehitaji msaada.
Ili kutekeza dhamana na wajibu huu, waamini wanahamasishwa kusali ili kumwomba Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake! Pili wahakikishe kwamba, wanajenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu kwa njia ya Sala, Neno na Sakramenti zake na kwa hakika Kristo Yesu atawafanya kuwa ni wahudumu na mashuhuda wa Ufalme wa Mungu. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwendea Bikira Maria aliyejisadaka bila ya kujibakiza, kwa njia ya ukarimu kiasi cha kutikia “Ndiyo” yake, iliyomwezesha kushiriki katika kazi ya ukombozi, aweze kuwaombea na hatimaye, kuwasindikiza katika hija ya kumfuasa Kristo Yesu, ili hatimaye, hata wao waweze kuwa ni wafanyakazi wenye furaha na mashuhuda wa Ufalme wa Mungu.