Papa Leo XIV: Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo: Uekumene wa Damu na Utume
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mama Kanisa anaendelea kukazia: Uekumene wa: damu, maisha ya kiroho, sala na huduma, kwani uekumene wa damu na ule wa utakatifu wa maisha, ni mambo msingi yanayoshuhudiwa na Wakristo sehemu mbalimbali za dunia katika umoja, udugu na upendo kama kikolezo cha ujenzi wa Ufalme wa Mungu na Fumbo la Mwili wa Kristo yaani Kanisa. Uekumene wa damu unajikita katika: Vita, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo. Lakini, ikumbukwe kwamba, damu ya mashuhuda hawa wa imani ni chachu ya Ukristo. Uekumene wa maisha ya kiroho na utakatifu wa maisha unafumbatwa katika toba na wongofu wa ndani; kwa kujikana na kujivika fadhila ya unyenyekevu; moyo wa ukarimu na udugu wa kibinadamu; upole, uvumilivu na kutumikia bila ya kujibakiza. Wakristo wanakumbushwa kwamba, kadiri wanavyojitahidi kuishi maisha matakatifu mintarafu tunu msingi za Kiinjili, ni kwa kadiri ileile watahamasisha na kutekeleza umoja wa Wakristo na udugu wa kibinadamu kati yao. Uekumene wa huduma unatekelezwa kwa njia ya sera na mikakati ya shughuli za kichungaji sanjari na maisha ya kitume.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu Petro na Paulo, Mitume na Miamba wa Kanisa, Baba Mtatifu Leo XIV, Dominika tarehe 29 Juni 2025 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa mara nyingine tena amekazia kuhusu uekumene wa damu unaoshuhudiwa na watakatifu, wafiadini na waungama imani. Hawa ni mashuhuda wa Injili kiasi hata cha kumwaga damu yao kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa Mataifa. Ndani ya Kanisa hata kama bado hakuna ushirika kamili kati ya Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo, lakini wote wanaunganishwa katika uekumene wa damu.Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa sasa ni huduma kwa ajili ya ushirika wa Kanisa la Roma ambalo limepambwa kwa damu ya watakatifu Petro na Paulo, ili kuendeleza mchakato wa ujenzi wa umoja na ushirika kati ya Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema: “Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika Maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu? Mt 21:42. Kumbe, Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na ule wa Mtakatifu Paulo, Nje ya Kuta za Roma, ni kielelezo cha Mitume ambao hapo awali, hawakuonekana kuwa ni “mali kitu” kadiri ya maoni ya walimwengu. Lakini kwa wale wanaothubutu kumfuasa na kutembea katika nyayo za Kristo Yesu mintarafu Heri za Mlimani zinakuwa ni dira na mwongozo wa maisha yao.
Heri Nane za Mlimani au Hotuba ya Mlimani ni: Muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Hii ni Katiba ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na neema; ni ufalme wa haki, mapendo na amani. Huu ni mwaliko kwa waamini kuchuchumilia na kufumbata: umaskini wa roho, upole, huruma, kiu na njaa ya haki; watu wanaojisadaka kwa ajili ya ujenzi wa haki na amani duniani na wapatanishi, hata kama watahudhiwa, watanyanyaswa na kudhulumiwa; utukufu wa Mungu utaendelea kung’ara miongoni mwa rafiki zake na katika kuenenda kwao watakuwa wanapandikiza toba na wongofu wa ndani unaoongoa.Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, kwa takribani miaka elfu mbili, waamini wamekuwa wakifanya hija ya kiroho kwenye Makaburi ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume, changamoto na mwaliko kwa waamini kugundua kwamba, wanaweza kuishi kutoka katika wongofu hadi kufikia wongofu.
Agano Jipya halifichi makosa, migongano, kinzani, na dhambi za wale wanaoheshimiwa kama Mitume wakuu. Lakini ikumbukwe kwamba ukuu wao unapata chimbuko lake kutoka katika Msamaha wa Kristo Yesu, aliyewawezesha mara kwa mara kurejea katika mstari wa mafundisho yake. Kristo Yesu daima anatoa fursa na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ndiyo maana waamini wote wanaweza kutumaini kila wakati kama ambavyo wanahamasishwa na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Baba Mtakatifu Leo XIV anakaza kusema, umoja katka Kanisa na kati ya Makanisa unastawishwa na kudumishwa na mchakato wa kusameheana na kuaminiana kwa kuanzia ndani ya familia, na jamii katika ujumla wake. Kwa hakika, ikiwa kama Kristo Yesu anawaamini na wao pia wanaweza kuaminiana katika Jina lake. Mitume Petro na Paulo, pamoja na Bikira Maria, wawaombee waamini na watu wote wenye mapenzi mema ili katika ulimwengu huu uliopasuka na kumegeka Kanisa liwe ni nyumba na shule ya umoja na ushirika.