Papa Leo XIV: Kristo Yesu Ni Ufunuo wa Huruma na Upendo wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV ameadhimisha Dominika ya Utume wa Bahari tarehe 13 Julai 2025 kwenye Parokia ya Kipapa ya “San Tommaso da Villanova, iliyoko Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, nje kidogo ya mji wa Roma. Maadhimisho haya yamenogeshwa na kauli; “Mahujaji wa matumaini, Madaraja ya Kuwakutanisha Nchi Maadui, Manabii wa Amani.” Kwa hakika bahari ni kiungo muhimu sana kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto na mwaliko wa kuwa na mwelekeo mpana zaidi, kwa kudumisha amani badala ya kuendekeza migogoro, mipasuko na vita. Mara baada ya Ibada ya Misa Takatifu, Baba Mtakatifu Leo XIV amewaongoza waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari na kusali Sala ya Malaika wa Bwana kwenye uwanja wa “Piazza della Libertà” ulioko Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Leo XIV tangu Dominika tarehe 6 Julai 2025 anapata mapumziko mafupi kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, huko Albano.
Injili ya Msamaria mwema ni muhtasari wa Amri kuu ya upendo kwa Mungu na jirani na ni moja ya sehemu muhimu sana ya mafundisho ya Kristo Yesu. Injili ya Msamaria Mwema ni mmojawapo ya mifano yenye kuleta uchokozi wa mawazo, hoja na changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema. Yesu amefunga safari ya kuelekea Yerusalemu pamoja na wafuasi wake. Njiani anakutana na mwanasheria ambaye anazungumza naye kuhusu urithi wa uzima wa milele. Mwanasheria huyo lengo lake hasa lilikuwa ni kumjaribu Kristo Yesu katika swala ambalo ni tete na lilikuwa linaleta changamoto kubwa kwa jamii ya wakati ule - Amri ipi ni muhimu kuliko zote ambayo uzima wa milele hunategemea? Swali la Mwanasheria ni fursa kwa Yesu kutoa mfano wa Msamaria Mwema ambao hufafanua uhusiano kati ya Sheria na moyo wake au hulka yake jinsi ilivyokusudiwa na Mwenyezi Mungu; “Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi.” Lk 10: 25-28.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema kwamba, hili ni swali zuri linaloonesha hamu ya kudumu katika maisha ya mwamini, tamaa ya wokovu yaani kuishi bila kushindwa na uovu na kifo. Uzima wa milele ambao ni Mungu peke yake anayeweza kuutoa, unapitishwa kwa mwanadamu kama urithi kutoka kwa Baba hadi kwa Mwana na kwamba, ili kupokea zawadi hii kutoka kwa Mungu lazima waamini wakubali kutekeleza mapenzi ya Mungu kama yalivyo andikwa katika Torati ya Musa: “Mpende Bwana Mungu kwa moyo wako wote na mpende na jirani yako kama nafsi yako. Kwa kufanya hivi, waamini wanalingana na upendo wa Mumgu na kwa hakika hii ni sheria ya uzima wa milele ambayo inafuatwa kwanza kutoka kwa waamini, kwa kuwapenda kwanza katika Mwana wake mpendwa Kristo Yesu na Roho Mtakatifu.
Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumtazama Kristo Yesu kwani Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu. Huu ni upendo unaotoa na usio miliki; ni upendo unaosamehe na usio na unafiki, ni upendo unaosaidia na usio telekeza kamwe. Katika Kristo, Mungu alijifanyika jirani kwa kila mtu: kwa hiyo, kila mtu anayo lazima ya kuwa na jirani, yaani hawa ni watu wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku. Kwa kufuata mfano wa Kristo Yesu, Mwokozi wa ulimwengu, waamini pia wanaitwa kuwa vyombo na mashuhuda wa kuleta faraja na tumaini, hasa kwa wale wote waliopondeka na kuvunjika moyo. Maisha ya uzima wa milele ni mwaliko wa kuwajali na kuwathamini wengine, hii kimsingi ndiyo Sheria kuu ambayo inakuja mbele ya kila utawala wa kijamii na kuipatia maana. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Leo XIV amewataka waamini kumwomba Bikira Maria, Mama wa Huruma awasaidie kukaribisha ndani mwao, mapenzi ya Mungu yanayosimikwa katika upendo na wokovu, ili waweze kuwa ni wapatanishi, mashuhuda na vyombo vya amani kila siku ya maisha yao.