杏MAP导航

Tafuta

Papa Leo XIV Awataka Waamini Wajifunze Utamaduni wa Ukarimu

Papa Leo XIV katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana tarehe 20 Julai 2025 kutoka Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, amewaalika waamini kote ulimwenguni kutafakari juu ya thamani ya ukarimu, akitumia mfano wa Abraham na Sara kutoka Agano la Kale na Martha na Maria rafiki wa Yesu kutoka Injili ya Luka 10:38-42. “Kila mara tunaposhiriki katika karamu ya Bwana na kushiriki katika chakula cha Ekaristi ni Mungu mwenyewe anayekuja kutuhudumia,” alisema.

Na Sarah Pelaji, -Vatican.

Baba Mtakatifu Leo XIV katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 20 Julai 2025 kutoka Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfo, amewaalika waamini kote ulimwenguni kutafakari juu ya thamani ya ukarimu, akitumia mfano wa Abraham na Sara kutoka Agano la Kale na Martha na Maria rafiki wa Yesu kutoka Injili ya Luka 10:38-42. “Kila mara tunaposhiriki katika karamu ya Bwana na kushiriki katika chakula cha Ekaristi ni Mungu mwenyewe anayekuja kutuhudumia,” alisema Papa Leo XIV huku akirejea maneno ya Yesu katika Injili ya Lk 12:37 akisisitiza kuwa Mungu anabaki kuwa mgeni anayebisha hodi mlangoni mwa mioyo yetu. Alitaja kuwa katika lugha ya Kiitalia, neno moja linaweza kumaanisha ‘mgeni’na ‘mwenyeji,’ jambo linaloonesha undani wa mchakato wa kutoa na kupokea ukarimu.

Waamini wakisali Sala ya Malaika wa Bwana, Castel Gandolfo
Waamini wakisali Sala ya Malaika wa Bwana, Castel Gandolfo   (ANSA)

Papa Leo XIV aliongeza kuwa unyenyekevu ni muhimu si tu katika kumpokea mgeni bali pia katika kuruhusu sisi wenyewe kupokelewa. Akimwelezea Martha alisema kwamba, ingawa alikuwa mkarimu, alikaribia kupoteza nafasi adimu ya kukutana na Yesu kwa kuwa alikuwa amezingatia maandalizi pekee. “Yesu alimwalika Martha kuwa zaidi ya mkarimu, hivyo alimwita kuacha maandalizi na kutumia muda naye,” alisema Baba Mtakatifu Leo XIV. Akizungumzia kuhusu maisha ya kila siku, Papa Leo XIV alisema kuwa maisha yanaweza kunawiri pale tu tunapojifunza kufunguka kwa kitu kikubwa kuliko sisi, kitu kinachotuletea furaha na utimilifu wa kweli. Aliwataka waamini kutumia Likizo ya kipindi cha kiangazi kama fursa ya kujifunza kuwa kama Maria ambaye alikaa karibu na Yesu badala ya kuwa kama Martha aliyejishughulisha na mambo mengi. “Tunahitaji kuchukua muda wa kupumzika na kujifunza vyema sanaa ya ukarimu,” alisema.

Sala ya Malaika wa Bwana, Castel Gandolfo
Sala ya Malaika wa Bwana, Castel Gandolfo   (@Vatican Media)

Alikosoa namna tasnia ya utalii inavyojaribu kuuza ‘uzoefu’ ambao pengine siyo unaohitajika. Kukutana na kuzungumza katika kubadilishana uzoefu iwe ni sehemu ya mikutano ya kukutana na Mungu au binadamu hakuhitaji kununuliwa bali ni bure na huru. “Tunahitaji tu kujifunza sanaa ya ukarimu, ambayo inajumuisha kuwakaribisha wengine na pia kujiruhusu sisi wenyewe kupokelewa. Tuna mengi ya kupokea si kutoa tu,” aliongeza. Alikumbusha jinsi Abraham na Sara licha ya uzee wao walivyopokea uzazi baada ya kuwakaribisha wageni watatu waliomwakilisha Mwenyezi Mungu. Kwa njia hiyo alisema, sisi pia tuna mengi ya kupokea katika maisha ikiwa tuko tayari kufungua mioyo yetu. Alimwombea kila mmoja kwa Bikira Maria Mama Yetu, aliyemkaribisha Kristo Yesu na kumpatia makao, kiasi cha kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. “Katika Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa tunauona uzuri wa wito wetu, wito wa Kanisa wa kuwa nyumba iliyo wazi kwa wote na kwa njia hiyo kumkaribisha Kristo Yesu anayebisha hodi mlangoni,” Papa Leo XIV alihitimisha tafakari yake! Na kwa waamini kote ulimwenguni, ujumbe huu wa Papa Leo XIV ni mwaliko wa kutafakari, kujifunza na kuishi kiundani zaidi Injili ya ukarimu wa kweli unaojikita katika upendo wa Mungu na kwa jirani.

Malaika wa Bwana
20 Julai 2025, 14:21

Sala ya Malaika wa Bwana ni sala inayowakumbusha waamini Fumbo la Umwilisho na husaliwa mara tatu kwa siku: Saa 12:00 asubuhi, Saa 6:00 mchana na Saa 12:00, wakati ambapo kengele ya Sala ya Malaika wa Bwana hugongwa. Neno Malaika wa Bwana limetolewa kutoka katika Sala ya Malaika wa Bwana aliyempasha Bikira Maria kwamba, atamzaa Kristo Yesu na husaliwa Salam Maria tatu. Sala hii husaliwa na Papa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro wakati wa Jumapili na Wakati wa Siku kuu na Sherehe. Kabla ya Sala, Papa hutangulia kutoa tafakari akifanya rejea kwa Masomo ya siku. Baadaye kunafuatia salam kwa wageni na mahujaji. Kuanzia Sherehe ya Pasaka hadi Pentekoste, badala ya Sala ya Malaika wa Bwana, waamini husali Sala ya Malkia wa Bwana, sala inayokumbuka Ufufuko wa Kristo Yesu na mwishoni, husaliwa Sala ya Atukuzwe Baba mara tatu.

Sala ya Malaika wa Bwana/ Malkia wa Mbingu ya hivi karibuni

Soma yote >