Katekesi ya Papa Leo XIV: Kristo Yesu Ni Mganga wa Roho na Mwili: Chemchemi ya Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu” ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kristo Tumaini letu, Hayati Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 alianzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu mifano ya Injili na akaanza kwa mfano wa Baba Mwenye huruma, kama unavyosimuliwa na Mwinjili Luka 15: 32. Hii ni mifano inayokita ujumbe wake katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwamba kiini cha Injili ya Luka ni Baba Mwenye Huruma, yaani Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo na kwamba, Injili inataka kuwapatia watu wa Mungu matumaini katika maisha kwani Mwenyezi Mungu daima yuko katika harakati za kuwatafuta waja wake, kama Kondoo au shilingi iliyopotea, kama Baba mwenye huruma na watoto wake wawili. Ni katika mwendelezo wa Injili ya Matumaini, Baba Mtakatifu Leo XIV tayari amekwisha kugusia kuhusu mfano wa mpanzi na kwamba, Injili ya Kristo Yesu ni mbegu iliyopandwa kwenye udongo wa maisha ya mwamini na Mwenyezi Mungu ndiye anayesongesha historia. Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, amewakirimia waja wake chemchemi ya matumaini mapya.
Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Baba Mtakatifu Leo XIV amekwisha kugusia pia kuhusu Wafanyakazi katika Shamba la Bwana: “enendeni nanyi katika shamba” sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 20:17. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 11 Juni 2025 ilinogeshwa na Injili kama ilivyoandikwa na Marko kuhusiana na kuponywa kwa Bartimayo, Mwana wa Timayo yule Mwombaji kipofu: Mama Kanisa katika Injili ya Marko 10: 46-52 anatuwekea mbele ya macho yetu, Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo kama kielelezo cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa, huku akielekea kukabiliana na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu!
Bartimayo Mwana wa Timayo aliposikia kwamba, Yesu anapita, akapiga kelele “Mwana wa Daudi Yesu, Unirehemu.” Wakataka kumnyamazisha, lakini yeye akapaaza sauti na kuvunjilia mbali viunzi na vizingiti vilivyokuwa vinamzuia, kiasi kwamba, Kristo Yesu, akaisikia na kujibu sauti yake. Hii inaonesha kwamba, Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima; ni mwanga wa mataifa na kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 18 Juni 2025 imenogeshwa na sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Yohane pale ambapo Kristo Yesu anamponya mgonjwa kule Yerusalemu: “Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano. Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza, wakingoja maji yachemke. (Kwa maana kuna wakati ambapo malaika hushuka, akaingia katika ile birika, akayatibua maji. Basi yeye aliyeingia wa kwanza baada ya maji kutibuliwa, akapona ugonjwa wote uliokuwa umempata.) Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda.” Yn 5: 2-9.
Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Kristo Yesu anawaganga na kuwaponya wale wote waliokata na kukatishwa tamaa ya maisha, wale ambao hawana tena ari na mwamko wa “kupambana na hali yao.” Kristo Yesu anasimama kwenye mlango wa birika liitwalo kwa lugha ya Kiebrania Bethzatha, maana yake “Nyumba ya Huruma.” Hiki kina weza kuwa ni kielelezo cha Kanisa, mahali ambapo wagonjwa na maskini, wanakusanyika na Kristo Yesu anawaendea ili kuwaganga, kuwaponya na kuwapatia tena matumaini mapya. Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anamponya mgonjwa aliyekuwa amepooza kwa miaka thelathini na nane, na kwa hakika alikuwa amekwisha kujikatia tamaa. Hivi ndivyo inavyokuwa hata kwa waamini wanapokumbana na hali ya kukata tamaa, kuna hatari ya kutumbukia kwenye uvivu, kiasi kwamba, hata ile hamu ya kupona inaanza kutoweka, ndiyo maana Kristo Yesu anamuuliza mgonjwa, Je, Wataka kuwa mzima?
Uvivu ni hali inayowalazimisha watu wengine kukuhudumia, kwani mgonjwa anajiona hawezi kitu hata pengine hataki kujishughulisha. Lakini Kristo Yesu anapokea jibu kutoka katika undani wa mgonjwa anayeonesha ule utashi wa kutaka kuponywa, akionesha hali yake halisi, kwamba hana mtu wa kumtia birikani, maji yanapotibuliwa, kumbe hapa hana kosa, lakini anashindwa kuwajibika barabara! Lakini jambo la kujiuliza, Je, hakuwa na mtu wa kuweza kumsaidia? Mtakatifu Augostino anasema, kwa hakika alimhitaji mtu, tena zaidi ya mtu alimhitaji Mungu, ili aweze kumganga na kumponya! Kwa hakika, huyu mgonjwa alikwisha kujikatia tamaa ya maisha, akashindwa katika mapambano ya maisha. Kristo Yesu anamkirimia matumaini na kumwambia asimame, ajitwike godoro lake na aende. Lile godoro ni kielelezo cha ugonjwa na historia ya maisha yake, kamwe hapaswi kuviacha. Huu ni mwaliko wa kutembea, wa kuwajibika na kuchagua njia ya kufuata! Yote haya yanawezekana kutokana na uwepo wa Kristo Yesu, mganga wa maisha ya kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba zawadi ya kufahamu wapi ambapo wamekwama, wawe na ari na ujasiri wa kutaka kuponywa. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kuwaombea wale watu ambao wamekwama katika magonjwa haya, ili waweze kuona njia ya kupitia, tayari kurejea na kuishi tena katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, Nyumba ya huruma!