杏MAP导航

Tafuta

Papa Leo XIV Katekesi Mwaka wa Jubilei 2025: Bartimayo Kipofu

Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, imenogeshwa na Injili ya Marko kuhusiana na kuponywa kwa Bartimayo, Mwana wa Timayo yule Mwombaji kipofu: Mk 10: 46-52 anatuwekea mbele ya macho yetu, Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo kama kielelezo cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa, huku akielekea kukabiliana na Fumbo la Kifo! Matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu” ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kristo Tumaini letu, Hayati Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 alianzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu mifano ya Injili na akaanza kwa mfano wa Baba Mwenye huruma, kama unavyosimuliwa na Mwinjili Luka 15: 32. Hii ni mifano inayokita ujumbe wake katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwamba kiini cha Injili ya Luka ni Baba Mwenye Huruma, yaani Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo na kwamba, Injili inataka kuwapatia watu wa Mungu matumaini katika maisha kwani Mwenyezi Mungu daima yuko katika harakati za kuwatafuta waja wake, kama Kondoo au shilingi iliyopotea, kama Baba mwenye huruma na watoto wake wawili. Ni katika mwendelezo wa Injili ya Matumaini, Baba Mtakatifu Leo XIV tayari amekwisha kugusia kuhusu mfano wa mpanzi na kwamba, Injili ya Kristo Yesu ni mbegu iliyopandwa kwenye udongo wa maisha ya mwamini na Mwenyezi Mungu ndiye anayesongesha historia. Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, amewakirimia waja wake chemchemi ya matumaini mapya.

Bartimayo Mwana wa Timayo Mwombaji Kipofu: Shuhuda wa imani na matumaini
Bartimayo Mwana wa Timayo Mwombaji Kipofu: Shuhuda wa imani na matumaini   (@Vatican Media)

Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Baba Mtakatifu Leo XIV amekwisha kugusia pia kuhusu Wafanyakazi katika Shamba la Bwana: “enendeni nanyi katika shamba” sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 20:17.Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 11 Juni 2025 imenogeshwa na Injili kama ilivyoandikwa na Marko kuhusiana na kuponywa kwa Bartimayo, Mwana wa Timayo yule Mwombaji kipofu: Mama Kanisa katika Injili ya Marko 10: 46-52 anatuwekea mbele ya macho yetu, Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo kama kielelezo cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa, huku akielekea kukabiliana na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Bartimayo Mwana wa Timayo aliposikia kwamba, Yesu anapita, akapiga kelele “Mwana wa Daudi Yesu, Unirehemu.” Wakataka kumnyamazisha, lakini yeye akapaaza sauti na kuvunjilia mbali viunzi na vizingiti vilivyokuwa vinamzuia, kiasi kwamba, Kristo Yesu, akaisikia na kujibu sauti yake.

Bartimayo mwana wa Timayo ni kielelezo cha imani na matumaini
Bartimayo mwana wa Timayo ni kielelezo cha imani na matumaini

Hii inaonesha kwamba, Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima; ni mwanga wa mataifa na kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Tunakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, daima anasikiliza kilio cha maskini, wanapomlilia kwa imani na matumaini kama alivyofanya Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo, ambaye hakuogopa kupaaza sauti na hatimaye, kusikilizwa na Kristo Yesu kwa imani thabiti, kiasi cha kubisha hodi katika moyo wa Mwenyezi Mungu, licha ya kutoeleweka na mapingamizi aliyokutana nayo njiani. “Yesu akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona. Yesu akamwambia, Enenda zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani.” Mk 10: 51-52.Bartimayo kipofu anaomba makuu kutoka kwa Kristo Yesu, anaomba “rehema” ili Kristo Yesu aweze kumrehemu kwa jinsi alivyo! Anainuka na kujionesha kwa Kristo Yesu jinsi alivyo katika utu na maisha yake! Anaomba: upendo, huruma na faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Bartimayo Mwana wa Timayo, anajiaminisha kwa huruma na upendo wa Mungu, kwa kuomba mambo msingi yatakayoweza kupyaisha tena maisha yake! Haya ni mambo ambayo kwa macho ya kibinadamu hayawezekani, lakini kwa Mwenyezi Mungu inawezekana. Bartimayo yule mwombaji kipofu, anamwonesha Kristo Yesu upofu wake, lakini ndani ya sakafu ya moyo wake, kulifunikwa madonda makubwa, nyanyaso, dharau, ndoto zilizotoweka kama “umande wa asubuhi”, mapungufu na makosa aliyotenda kama binadamu!

Enenda zako imani yako imekuponya
Enenda zako imani yako imekuponya   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, maneno ya Bartimayo mwana wa Timayo “Mwana wa Daudi Yesu, Unirehemu” imekuwa ni sala maarufu sana kwenye Mapokeo ya Makanisa ya Mashariki; ni sala ambayo hata waamini wengine wanaweza kusali “Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, Unihurumie mimi mdhambi.” Bartimayo kipofu alikuwa na uwezo wa kuona mbali zaidi hata kuliko wale waliokuwa wamebahatika kuwa na macho, kwani aliweza kumtambua Kristo Yesu, Mwana wa Daudi, Mungu akasikiliza na kujibu kilio chake, akamchangamotisha kusimama na kuanza kutembea na hivyo kufufuka kutoka katika udhaifu wake wa kimwili, akapata ujasiri wa kutupa vazi lake, akaruka na kumwendea Kristo Yesu! Hilo vazi lake ndilo lililokuwa kielelezo cha usalama wake, nyumba yake na hifadhi ya maisha yake. Ili Kristo Yesu aweze kukuponya, kuna haja ya kujiachia na kujiaminisha mbele yake. Hii ni hatua muhimu sana, kuweza kupata uponyaji kutoka kwa Kristo Yesu! Anataka kuona tena, kurejeshewa utu, heshima na haki zake msingi na kwamba, imani yake ndicho chanzo cha uponywaji wake, tayari kumfuasa Kristo Yesu chanzo cha maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujiaminisha kwa Kristo Yesu, tayari kumpelekea magonjwa yao na yale ya ndugu na jamaa zao; wampelekee Kristo Yesu, shida, mateso na mahangaiko ya wale wanaoteseka, bila ya kupata msaada. Kwa pamoja, wapaaze sauti zao na kwa hakika Kristo Yesu ataweza kuwasikiliza pamoja na kuwajibu!

Bartimayo Kipofu
11 Juni 2025, 16:52

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >