杏MAP导航

Tafuta

Papa Leo XIV Katekesi Mwaka wa Jubilei 2025: Fumbo la Pasaka

Ni katika muktadha wa Fumbo la Pasaka, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano, tarehe 6 Agosti 2025 ameanza kufanya tafakari ya Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Baba Mtakatifu ameanza tafakari yake kwa Neno “Maandalio” ya Karamu ya Pasaka; “Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile Pasaka? Kifo cha Mt. Paulo VI

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo: Kristo Tumaini letu, Hayati Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 alianzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu: Maisha ya Kristo Yesu: Mifano ya Injili na akaanza kwa mfano wa Baba Mwenye huruma, kama unavyosimuliwa na Mwinjili Luka 15: 32. Hii ni mifano inayokita ujumbe wake katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwamba kiini cha Injili ya Luka ni Baba Mwenye Huruma, yaani Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo na kwamba, Injili inataka kuwapatia watu wa Mungu matumaini katika maisha kwani Mwenyezi Mungu daima yuko katika harakati za kuwatafuta waja wake, kama Kondoo au shilingi iliyopotea, kama Baba mwenye huruma na watoto wake wawili. Ni katika mwendelezo wa Injili ya Matumaini, Baba Mtakatifu Leo XIV tayari amekwisha kugusia kuhusu: Mfano wa mpanzi na kwamba, Injili ya Kristo Yesu ni mbegu iliyopandwa kwenye udongo wa maisha ya mwamini na Mwenyezi Mungu ndiye anayesongesha historia. Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, amewakirimia waja wake chemchemi ya matumaini mapya.

Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa
Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV amekwisha kugusia pia kuhusu Wafanyakazi katika Shamba la Bwana: “enendeni nanyi katika shamba” sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 20:17. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 11 Juni 2025 ilinogeshwa na Injili kama ilivyoandikwa na Marko kuhusiana na kuponywa kwa Bartimayo, Mwana wa Timayo yule Mwombaji kipofu: Mama Kanisa katika Injili ya Marko 10: 46-52 anatuwekea mbele ya macho yetu, Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo kama kielelezo cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa, huku akielekea kukabiliana na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Bartimayo Mwana wa Timayo aliposikia kwamba, Yesu anapita, akapiga kelele “Mwana wa Daudi Yesu, Unirehemu.” Wakataka kumnyamazisha, lakini yeye akapaaza sauti na kuvunjilia mbali viunzi na vizingiti vilivyokuwa vinamzuia, kiasi kwamba, Kristo Yesu, akaisikia na kujibu sauti yake. Hii inaonesha kwamba, Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima; ni mwanga wa mataifa na kiini cha Habari Njema ya Wokovu.

Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini
Fumbo la Pasaka ni chemchemi ya wokovu, imani na matumaini   (@Vatican Media)

Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 18 Juni 2025 ilinogeshwa na sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Yohane pale ambapo Kristo Yesu anamponya mgonjwa kule Yerusalemu. Kristo Yesu anawaganga na kuwaponya wale wote waliokata na kukatishwa tamaa ya maisha, wale ambao hawana tena ari na mwamko wa “kupambana na hali yao.” Kristo Yesu anasimama kwenye mlango wa birika liitwalo kwa lugha ya Kiebrania Bethzatha, maana yake “Nyumba ya Huruma.” Hiki kina weza kuwa ni kielelezo cha Kanisa, mahali ambapo wagonjwa na maskini, wanakusanyika na Kristo Yesu anawaendea ili kuwaganga, kuwaponya na kuwapatia tena matumaini mapya. Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anamponya mgonjwa aliyekuwa amepooza kwa miaka thelathini na nane, na kwa hakika alikuwa amekwisha kujikatia tamaa. Hivi ndivyo inavyokuwa hata kwa waamini wanapokumbana na hali ya kukata tamaa, kuna hatari ya kutumbukia kwenye uvivu, kiasi kwamba, hata ile hamu ya kupona inaanza kutoweka, ndiyo maana Kristo Yesu anamuuliza mgonjwa, Je, Wataka kuwa mzima? Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba zawadi ya kufahamu wapi ambapo wamekwama, wawe na ari na ujasiri wa kutaka kuponywa. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kuwaombea wale watu ambao wamekwama katika magonjwa haya, ili waweze kuona njia ya kupitia, tayari kurejea na kuishi tena katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, Nyumba ya huruma!

Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa
Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa

Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 25 Juni 2025 imenogeshwa na matukio mawili ya kusikitisha sana: Kuponywa kwa mwanamke aliyetokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili na imani inayomfufua Binti Yairo. “Na alikuwepo mama mmoja aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. Mama huyu alikuwa amehangaika sana, akiwa ametibiwa na waganga wa kila aina na kutumia fedha yake yote kwa waganga lakini hakupata nafuu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya.  Alikuwa amesikia habari za Yesu kwa hiyo alimfuata kwa nyuma, akapenyeza kati ya watu, akaligusa vazi lake.  Maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitapona.”  Mara damu iliyokuwa inamtoka ikakauka; akajisikia amepona kabisa.  Yesu akafahamu kuwa nguvu zimemtoka. Akageuka, akawauliza wale watu, “Ni nani amenigusa?” Wanafunzi wake wakamjibu, “Mbona unauliza ni nani ameku gusa? Huoni umati huu ulivyokusonga?”  Lakini Yesu alizidi kutazama aone ni nani aliyemgusa. Kisha yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni kwake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.” Yesu Amfufua Binti Yairo: Alipokuwa akiongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo wakamwambia, “Usimsumbue tena mwalimu, binti yako amefariki.” Lakini Yesu hakuyatilia maanani maneno hayo, akamwambia Yairo, “Usiogope, bali amini tu.” Mk 5: 21-43.

Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa binadamu
Kanisa ni Sakramenti ya wokovu kwa binadamu   (@Vatican Media)

Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani, maisha na utume wa Kanisa! Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu ni kilele cha ukweli wa imani katika Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na hatimaye kufufuka kutoka wafu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Ni ufunuo wa Uungu wa Kristo Yesu unaowapatia waamini maisha ya uzima mpya na hivyo kuhesabiwa haki pamoja na kufanywa wana wateule wa Mungu. Ufufuko wa Kristo ni msingi wa ufufuko wa miili na uzima wa milele ijayo! Ndiyo maana Pasaka ni Sherehe kubwa katika Kanisa. Hii ni Sherehe ya upendo, huruma na msamaha wa Baba wa milele unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Kwa njia ya Fumbo la Pasaka, wote wamehesabiwa haki, kwa vile wamefufuka katika Kristo Yesu, wanapaswa kuyatafuta na kuyaambata yale ya mbinguni, ushuhuda wa imani tendaji. Kwa wale waliozaliwa upya kwa kuuvua utu wao wa kale, wataweza kuhesabiwa haki mbele ya Kristo. Wakristo wawe na ujasiri wa kumwachia Kristo Yesu, aweze kuosha na kutakasa macho ya imani, ili kuona na kutenda vyema, kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa Kristo Mfufuka. Kwa kuishi vyema Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, waamini wanaalikwa kuiga mfano wa maisha ya Bikira Maria aliyefuatana na Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu katika Njia yake ya Msalaba, akateseka sana pamoja naye hadi kudiriki kusimama chini ya Msalaba bila kumwonea aibu! Ni Mama ambaye, moyo wake ulisheheni furaha isiyokuwa na kipimo, kwa Fumbo la Ufufuko wa Kristo kutoka wafu. Maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, yawawezeshe waamini kushiriki kikamilifu ili waweze kupyaisha maisha, wito na utume wao wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia.

Ufufuko wa Kristo ni Msingi wa Ufufuko wa miili na uzima wa milele
Ufufuko wa Kristo ni Msingi wa Ufufuko wa miili na uzima wa milele   (ANSA)

Ni katika muktadha wa Fumbo la Pasaka, Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano, tarehe 6 Agosti 2025 ameanza kufanya tafakari ya Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Baba Mtakatifu ameanza tafakari yake kwa Neno “Maandalio” ya Karamu ya Pasaka; “Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka? Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni; na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu? Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni. Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa Pasaka.” Mk 14:12-16. Ukisoma kwa umakini “Maandalio” haya ya Karamu ya Pasaka inaonesha kana kwamba, kila kitu kilikuwa kimekwisha kuandaliwa kwa ajili ya Karamu ya Pasaka, kielelezo cha upendo wa dhati unaotekelezwa kwa ufahamu mkubwa; upendo unaohitaji maandalizi ya kina na uaminifu, safari inayokita mizizi yake katika uhuru na utunzaji bora wa Injili ya upendo. Huu ni ushuhuda kwamba, sadaka ya maisha ya Kristo Yesu ni chimbuko la nia ya dhati kabisa kutoka katika undani wa maisha yake.

Pasaka ni sherehe ya huruma, upendo na msamaha wa Baba wa milele.
Pasaka ni sherehe ya huruma, upendo na msamaha wa Baba wa milele.

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwenyezi Mungu daima anawatangulia waja wake, lakini wanapaswa kujiandaa kwa ajili ya kuupokea wema na ukarimu wake, kwani Kristo Yesu amekwisha waandalia rafiki zake chumba cha Karamu ya Pasaka. Hapa ni mahali ambapo, marafiki wa Kristo Yesu wataweza kutambuana, kwani Pasaka ya Bwana iliyokuwa inaandaliwa na Kristo Yesu, tayari ilikwisha kuandaliwa katika Moyo Mtakatifu wa Kristo Yesu, mwaliko kwa rafiki zake kutekeleza dhamana na wajibu wao, kwani neema ina amsha na kupyaisha uhuru wa wafuasi wa Kristo na kwamba, zawadi ya Mungu inaimarisha uwajibikazi na hatimaye, kuonesha matokeo. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu linaloadhimishwa kila siku katika maisha ya wafuasi wa Kristo Yesu, kwa kuishi katika sadaka na kuonesha moyo wa shukrani. Maandalizi ya Fumbo la Ekaristi Takatifu yasifanyike kwa waamini kujisikia, kwani kutawapotezesha lengo, lakini maandalizi yanawaongoza na kuwapatia dira, ili kuweza kukutana na Kristo Mfufuka, kielelezo cha upendo thabiti, karamu ya umoja na ushirika. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, waamini wanahamasishwa kufanya maandalizi ya Karamu ya Bwana Kiliturujia, lakini zaidi katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku; kwa kuwajibika, katika hali ya uvumilivu, ili kuweza kutengeneza mahali ambapo Mwenyezi Mungu ataweza kuishi. Maandalizi yaanze kwa mwamini mmoja mmoja, kwa kusikiliza kwa makini, kwa kutenda na kujifunza zaidi. Huu ni mwaliko kwa waamini kuandaa mahali pa kukutana na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao; kwa kutambua alama muhimu zinazopaswa kuwamo katika chumba kile, ili hatimaye, kuweza kuadhimisha Fumbo la Upendo wa Kristo usiokuwa na kifani. Kristo Yesu katika sehemu hii ya maandalizi, anaonesha uwepo wake wa unyenyekevu, mwaliko kwa waamini kuweza kukuza ndani mwao, ile imani inayowawezesha kukabiliana na changamoto mamboleo kwa moyo wazi, kwani hapa ni mahali ambapo upendo umeandaliwa na hivyo maisha yanaweza kuchanua!

Papa Leo XIV Fumbo la Pasaka
06 Agosti 2025, 15:49

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >