杏MAP导航

Tafuta

Katekesi ya Papa Leo XIV: Kuponywa Kwa Mwanamke Na Kufufuliwa Binti Yairo

Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 25 Juni 2025 imenogeshwa na matukio mawili ya kusikitisha sana: Kuponywa kwa mwanamke aliyetokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili na imani inayomfufua Binti Yairo, kielelezo kwamba, Kristo Yesu ni matumaini ya waja wake katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi. Kristo Yesu ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo kwa waja wake, wakimwendea kwa imani na ujasiri mkuu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo: Kristo Tumaini letu, Hayati Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 alianzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu: Maisha ya Kristo Yesu: Mifano ya Injili na akaanza kwa mfano wa Baba Mwenye huruma, kama unavyosimuliwa na Mwinjili Luka 15: 32. Hii ni mifano inayokita ujumbe wake katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwamba kiini cha Injili ya Luka ni Baba Mwenye Huruma, yaani Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo na kwamba, Injili inataka kuwapatia watu wa Mungu matumaini katika maisha kwani Mwenyezi Mungu daima yuko katika harakati za kuwatafuta waja wake, kama Kondoo au shilingi iliyopotea, kama Baba mwenye huruma na watoto wake wawili. Ni katika mwendelezo wa Injili ya Matumaini, Baba Mtakatifu Leo XIV tayari amekwisha kugusia kuhusu: Mfano wa mpanzi na kwamba, Injili ya Kristo Yesu ni mbegu iliyopandwa kwenye udongo wa maisha ya mwamini na Mwenyezi Mungu ndiye anayesongesha historia. Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, amewakirimia waja wake chemchemi ya matumaini mapya. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni.

Kristo Yesu alimfufua Binti Yairo: yesu ni chemchemi ya matumaini
Kristo Yesu alimfufua Binti Yairo: yesu ni chemchemi ya matumaini   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV amekwisha kugusia pia kuhusu Wafanyakazi katika Shamba la Bwana: “enendeni nanyi katika shamba” sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Mathayo 20:17. Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 11 Juni 2025 ilinogeshwa na Injili kama ilivyoandikwa na Marko kuhusiana na kuponywa kwa Bartimayo, Mwana wa Timayo yule Mwombaji kipofu: Mama Kanisa katika Injili ya Marko 10: 46-52 anatuwekea mbele ya macho yetu, Kipofu Bartimayo Mwana wa Timayo kama kielelezo cha imani na matumaini kwa Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai. Kristo Yesu alikuwa anasafiri kutoka Yerusalemu pamoja na wanafunzi wake na mkutano mkubwa, huku akielekea kukabiliana na Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake kwa wafu! Bartimayo Mwana wa Timayo aliposikia kwamba, Yesu anapita, akapiga kelele “Mwana wa Daudi Yesu, Unirehemu.” Wakataka kumnyamazisha, lakini yeye akapaaza sauti na kuvunjilia mbali viunzi na vizingiti vilivyokuwa vinamzuia, kiasi kwamba, Kristo Yesu, akaisikia na kujibu sauti yake. Hii inaonesha kwamba, Kristo Yesu ni Njia, Ukweli na Uzima; ni mwanga wa mataifa na kiini cha Habari Njema ya Wokovu.

Yesu alimponya mwanamke aliyetokwa damu kwa muda wa miaka 12
Yesu alimponya mwanamke aliyetokwa damu kwa muda wa miaka 12   (@Vatican Media)

Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 18 Juni 2025 imenogeshwa na sehemu ya Injili kama ilivyoandikwa na Yohane pale ambapo Kristo Yesu anamponya mgonjwa kule Yerusalemu. Kristo Yesu anawaganga na kuwaponya wale wote waliokata na kukatishwa tamaa ya maisha, wale ambao hawana tena ari na mwamko wa “kupambana na hali yao.” Kristo Yesu anasimama kwenye mlango wa birika liitwalo kwa lugha ya Kiebrania Bethzatha, maana yake “Nyumba ya Huruma.” Hiki kina weza kuwa ni kielelezo cha Kanisa, mahali ambapo wagonjwa na maskini, wanakusanyika na Kristo Yesu anawaendea ili kuwaganga, kuwaponya na kuwapatia tena matumaini mapya. Ni katika muktadha huu, Kristo Yesu anamponya mgonjwa aliyekuwa amepooza kwa miaka thelathini na nane, na kwa hakika alikuwa amekwisha kujikatia tamaa. Hivi ndivyo inavyokuwa hata kwa waamini wanapokumbana na hali ya kukata tamaa, kuna hatari ya kutumbukia kwenye uvivu, kiasi kwamba, hata ile hamu ya kupona inaanza kutoweka, ndiyo maana Kristo Yesu anamuuliza mgonjwa, Je, Wataka kuwa mzima? Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuomba zawadi ya kufahamu wapi ambapo wamekwama, wawe na ari na ujasiri wa kutaka kuponywa. Baba Mtakatifu Leo XIV anawaalika waamini kuwaombea wale watu ambao wamekwama katika magonjwa haya, ili waweze kuona njia ya kupitia, tayari kurejea na kuishi tena katika Moyo Mtakatifu wa Yesu, Nyumba ya huruma!

Katekesi: Mwanamke mgonjwa na Ufufuo wa Binti Yairo
Katekesi: Mwanamke mgonjwa na Ufufuo wa Binti Yairo   (@Vatican Media)

Katekesi ya Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumatano tarehe 25 Juni 2025 imenogeshwa na matukio mawili ya kusikitisha sana: Kuponywa kwa mwanamke aliyetokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili na imani inayomfufua Binti Yairo. “Na alikuwepo mama mmoja aliyekuwa amesumbuliwa na tatizo la kutokwa damu kwa miaka kumi na miwili. Mama huyu alikuwa amehangaika sana, akiwa ametibiwa na waganga wa kila aina na kutumia fedha yake yote kwa waganga lakini hakupata nafuu. Hali yake ilizidi kuwa mbaya.  Alikuwa amesikia habari za Yesu kwa hiyo alimfuata kwa nyuma, akapenyeza kati ya watu, akaligusa vazi lake.  Maana alisema moyoni mwake, “Nikiligusa vazi lake tu, nitapona.”  Mara damu iliyokuwa inamtoka ikakauka; akajisikia amepona kabisa.  Yesu akafahamu kuwa nguvu zimemtoka. Akageuka, akawauliza wale watu, “Ni nani amenigusa?” Wanafunzi wake wakamjibu, “Mbona unauliza ni nani ameku gusa? Huoni umati huu ulivyokusonga?”  Lakini Yesu alizidi kutazama aone ni nani aliyemgusa. Kisha yule mwanamke, akijua kilichomtokea, akaja, akaanguka miguuni kwake akitetemeka kwa hofu, akamweleza ukweli wote. Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.” Yesu Amfufua Binti Yairo: Alipokuwa akiongea, watu wakafika kutoka nyumbani kwa Yairo wakamwambia, “Usimsumbue tena mwalimu, binti yako amefariki.” Lakini Yesu hakuyatilia maanani maneno hayo, akamwambia Yairo, “Usiogope, bali amini tu.” Mk 5: 21-43.

Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na matumaini thabiti
Kristo Yesu ni chemchemi ya imani na matumaini thabiti   (ANSA)

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Mwanamke anaponywa na Binti Yairo kwa imani anafufuliwa na kulikuwepo msichana wa miaka kumi na miwili, aliyekuwa kufani na sasa Mwinjili Marko anaweka mbele ya macho ya wasomaji wake mwanamke ambaye alitokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Marko anaonesha imani na matumaini thabiti ya Mkuu wa Sinagogi, Baba wa Binti Yairo, hata pale anapoletewa habari kwamba, Binti yake alikuwa amekwisha kufariki dunia, lakini bado alionesha imani na matumaini kwa Kristo Yesu kwamba, angeweza kumfufufa Binti yake. Yule Mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, akaonesha ujasiri, imani na matumaini; mambo yaliyoleta mabadiliko makubwa katika maisha yake. Huyu ni yule mwanamke aliyekuwa ametengwa na kuishi katika upweke hasi, akajitokeza kwa nyuma na kugusa vazi la Kristo Yesu na hivyo kupona kabisa. Hii ni njia ya wokovu inayosimikwa katika imani na matumaini kwa Kristo Yesu anayeganga na kuwaponya waja wake wanaomwendea kwa: ujasiri, imani na matumaini. Kristo Yesu alikuwa amezungukwa na umati mkubwa wa watu, lakini imani ikafanikiwa kumgusa Kristo Yesu anasema Mtakatifu Augostino. Kwa hakika, waamini wakimwendea Kristo Yesu kwa imani na matumaini, atawakirimia neema na baraka, chemchemi ya mabadiliko katika maisha. Hii ni changamoto kwa waamini kumwendea Kristo Yesu kwa imani, matumaini na ujasiri; kwa kushinda woga na hofu kama ilivyokuwa kwa yule mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili. Ndani mwake akasikia kwamba ameponywa na Kristo Yesu akamwambia: “Binti, imani yako imekuponya, enenda zako kwa amani.” Mk 5: 36.

Umati mkubwa wa waamini na mahujaji umehudhuria katekesi ya Papa
Umati mkubwa wa waamini na mahujaji umehudhuria katekesi ya Papa   (@Vatican Media)

Wakati yote haya yanatendeka anasema Baba Mtakatifu Leo XIV, Mkuu wa Sinagogi, Baba yake Binti Yairo akaletewa habari za kifo cha binti yake, lakini Kristo Yesu akamwambia Mkuu wa Sinagogi “Usiogope, amini tu.” Mk 5: 36. Wakaongozana hadi nyumbani kwa Mkuu wa Sinagogi, akawaambia waombolezaji “kijana hakufa, bali amelala tu.” Mk 5: 39. Akaingia ndani alimokuwamo yule kijana akamshika mkono akamwambia, “Talitha, kumi”; tafsiri yake, “Msichana, nakuambia, inuka!” Akasimama na kuanza kutembea. Rej Mk 5: 41-42. Hiki ni kielelezo kwamba, Kristo Yesu anaponya magonjwa na kuwainua wale waliolala katika usingizi wa amani. Kwa Mwenyezi Mungu ambaye ni asili ya maisha na uzima wa milele, kifo kwake ni kama kulala usingizi, lakini kifo cha kweli ni kile cha maisha ya kiroho, ambacho waamini wanapaswa kukiogopa! Baada ya kumfufua Binti Yairo, Kristo Yesu anawaamuru wazazi wake kumpatia chakula, kielelezo cha ukaribu wa Kristo Yesu katika mahangaiko ya binadamu. Hii ni changamoto kwa wazazi na walezi kuhakikisha kwamba, pale watoto wao wanapotumbukia katika ugonjwa wa sonona, watambue kwamba, wanahitaji hata tiba ya maisha ya kiroho. Kumbe, waamini waendelee kujitajirisha na Neno la Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema katika maisha kuna nyakati za kukata na kukatishwa tamaa sanjari na uzoefu wa kifo. Huu ni mwaliko kwa waamini kujifunza kutoka kwa yule mwanamke aliyekuwa anatokwa damu kwa miaka kumi na miwili, wapige moyo konde na kumwendea Kristo Yesu, kwani anaweza kuwaganga na kuwaponya; anaweza kuwasimamisha tena kwa sababu Kristo Yesu ni chemchemi ya matumaini kwa waja wake.

Papa leo XIV akisalimiana na mahujaji na waamini
Papa leo XIV akisalimiana na mahujaji na waamini

Baba Mtakatifu Leo XIV akizungumza na makundi mbalimbali ya mahujaji na waamini amewataka, wawe ni mashuhuda amini wa huruma na upendo wa Mungu na wamisionari wa haki na amani; wawe kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za Injili ya Kristo Yesu. Katika kipindi hiki cha Likizo ya Kiangazi, iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya kijamii na kidini; kwa wanandoa wapya, likizo hii iwasaidie kujenga na kudumisha umoja wao, ili kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wagonjwa wafanikiwe kuonja ukaribu wa ndugu, jamaa na marafiki zao. Vijana wajenge na kudumisha utamaduni wa kusali na kulitafakari Neno la Mungu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuukimbilia Moyo Mtakatifu wa Yesu, unaofahamu kupenda, kusamehe na kuwahudumia wengine. Wamwombe Kristo Yesu ili aweze kuwaongezea imani, matumaini na mapendo thabiti katika maisha.

Katekesi Jubilei 2025
25 Juni 2025, 15:31

Mikutano ya Baba Mtakatifu kwa siku za hivi karibuni

Soma yote >