Papa Francisko Mwenyezi Mungu Anapanda Ngano Safi na Shetani Magugu: Uvumilivu wa Mungu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 23 Julai 2023 baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Tatu ya Babu, Bibi na Wazee Duniani ambayo imenogeshwa na kauli mbiu “Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi” Lk. 1:50; ameongoza Sala ya Malaika wa Bwana na tafakari ya Injili Dominika ya 16 ya Mwaka A wa Kanisa. Kristo Yesu akawatolea mfano mwingine akisema “Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake; lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake. Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.” Mt 13: 24-26. Baba Mtakatifu katika tafakari yake, amejikita zaidi kuhusu konde ambalo ni moyo wa mwanadamu, ambamo Mungu anapanda ngano na Shetani anapanda magugu na kuna konde la Kimungu na konde la ujirani mwema anataka kuliona likikuwa katika mazuri na kuliwezesha kukua hadi wakati wa mavuno. Kristo Yesu anasema, konde kubwa ambalo ndani mwake kuna ngano iliyopandwa na Mwenyezi Mungu na magugu yaliyopandikizwa na Shetani, Ibilisi, lakini ngano na magugu yanakuwa pamoja. Hii ndiyo hali halisi inayojitokeza katika jamii, ndani ya familia na hata katika Kanisa. Pale inapogundulika ngano safi, kunakuwepo na kishawishi cha kutaka kuyang’oa magugu, lakini hiki ni kishawishi ambacho Kristo Yesu anakitolea onyo kwa kusema kwamba, si rahisi kutengeneza dunia iliyo kamilifu au kuwaenzi watenda mema na kuwafutilia mbali watu wabaya na watenda dhambi, kwani matokeo yake ni hatari ya “kumtupilia mbali mtoto na mbereko.”
Baba Mtakatifu anasema, konde la pili ni moyo wa mwanadamu, mahali pekee, ambako mwamini anaruhusiwa kupatengeneza ili pawe safi, lakini hata katika moyo wa mwanadamu kuna ngano safi na magugu yanayokuwa na kukomaa kwa pamoja na hivyo kutengeneza konde kubwa la ulimwengu. Moyo wa mwanadamu ni uwanda wa uhuru, ambao uko wazi lakini ni dhaifu, kumbe, ili kupandikiza mbegu ili iweze kuzaa matunda mema, ngano bora kuna haja ya kuwa waangalifu, kwanza kabisa kwa kuona na kutambua magugu katika maisha ya mwanadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini kuchunguza dhamiri zao ili kuangalia ni kipi kinachokua na kuchukua nafasi katika dhamiri zao; Je, ni wema au ubaya wa moyo? Ili kuweza kufikia maamuzi thabiti, mwamini anasaidiwa na zoezi la kuchunguza dhamiri, kwa mwanga wa Mungu anaweza kuona kile kinachoendelea katika sakafu ya moyo wake.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, konde la tatu ni ujirani mwema unaosimikwa katika mwingiliano na mafungamano ya kijamii, mwaliko kwa waamini kwanza kabisa kabla ya kuona magugu katika maisha yao, wajitahidi walau kutambua ngano bora iliyopandwa na Mwenyezi Mungu katika maisha yao. Huu ni mwaliko wa kumwomba Mwenyezi neema na baraka ya kuangalia mema yaliyoko ndani mwao na katika jirani zao, kwa jicho la mwamini, kwa sababu Mwenyezi Mungu ndiye mkulima kwenye uwanda mkubwa wa ulimwengu, anaangalia mema ya nchi, anayakuza na kuyakomaza hadi wakati wa mavuno na hapo itakuwa ni sherehe kubwa. Baba Mtakatifu amehitimisha tafakari yake ya Sala ya Malaika wa Bwana kwa kuwataka waamini kuondokana na maamuzi mbele katika konde la ulimwengu; katika konde la moyo wa mtu, ajitafakari na kujiangalia mwenyewe ikiwa kama ni mkweli mbele ya Mungu, tayari kutafuta magugu katika maisha yake ili kuyatupia katika moto wa huruma na upendo wa Mungu. Katika uwanda wa ujirani mwema; Je, mwamini anaongozwa na hekima inayomsaidia kuona mema na mazuri kutoka kwa jirani zake? Bikira Maria awasaidie waamini kukuza na kudumisha uvumilivu kwa kile ambacho Mwenyezi Mungu amepandikiza katika konde la maisha ya mwanadamu.