Papa Leo XIV: Katekesi Kuhusu Mwaka wa Jubilei 2025: Injili ya Msamaria Mwema
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu” ni sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Kristo Tumaini letu, Hayati Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 16 Aprili 2025 alianzisha mzungumko mpya wa Katekesi kuhusu mifano ya Injili na akaanza kwa mfano wa Baba Mwenye huruma, kama unavyosimuliwa na Mwinjili Luka 15: 32. Hii ni mifano inayokita ujumbe wake katika uhalisia wa maisha ya kila siku na kwamba kiini cha Injili ya Luka ni Baba Mwenye Huruma, yaani Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo na kwamba, Injili inataka kuwapatia watu wa Mungu matumaini katika maisha kwani Mwenyezi Mungu daima yuko katika harakati za kuwatafuta waja wake, kama Kondoo au shilingi iliyopotea, kama Baba mwenye huruma na watoto wake wawili.
Ni katika mwendelezo wa Injili ya Matumaini, Baba Mtakatifu Leo XIV tayari amekwisha kugusia kuhusu mfano wa mpanzi na kwamba, Injili ya Kristo Yesu ni mbegu iliyopandwa kwenye udongo wa maisha ya mwamini na Mwenyezi Mungu ndiye anayesongesha historia. Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, amewakirimia waja wake chemchemi ya matumaini mapya. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni.
Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi! Hayati Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, huruma ya Mungu inajidhihirisha kwa namna ya pekee katika: Maadhimisho ya Sakramenti za Uponyaji yaani: Sakramenti ya Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Baba Mtakatifu anapenda kutoa mkazo wa pekee katika Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini huruma, upendo na msamaha wa dhambi; mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kumwilisha upendo wa Mungu katika maisha tayari kuwaonjesha majirani upendo huo kama ilivyokuwa kwa mfano wa Msamaria mwema, maarufu kama Injili ya Msamaria mwema.
“Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.” Lk 10: 25-37.
Baba Mtakatifu Leo XIV katika Katekesi yake, Jumatano tarehe 28 Mei 2025 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kuwa na mwelekeo mpya wa maisha mintarafu Injili ya huruma na upendo kwa jirani, ili hatimaye, waweze kuurithi uzima wa milele. Kristo Yesu katika Injili hii ya Msamaria mwema anatoa mfano wa njia ya maisha kadiri ya Msamaria mwema anayeangukia mikononi mwa wanyang’anyi wanaomtenda vibaya na kumwacha karibu ya kufa. Katika njia hii ya maisha, akapita: Kuhani na Mlawi walipita kando, lakini, Baba Mtakatifu Leo XIV anakumbusha kwamba, mtu kabla ya kuwa ni mwamini anakumbushwa kwamba, ni binadamu. Inasikitisha kuona kwamba, haraka ya maisha inawafanya watu kushindwa kuwahudumia jirani zao kwa huruma na upendo.
Msamaria mwema ndiye mtu pekee aliyethubutu kumwonea huruma, akamkaribia na kumfunga jeraha zake, akazitia mafuta na divai. Lakini ikumbukwe kwamba, Wasamaria ni watu waliokuwa wanadharaulika sana. Rej. 2 Fal 17. Msamaria mwema aliweza kusimama na kushuka kwa sababu aliguswa na utu, akawa tayari kumsaidia na kumhudumia yule mtu aliyekuwa amejeruhiwa, akampeleka kwenye nyumba ya kutunza wageni na kuahidi kumgharimia zaidi kwa kutambua kwamba, huyu alikuwa ni mtu aliyehitaji huduma yake na wala si mzigo wa kuegeshwa pale kwenye nyumba ya wageni! Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, hii ni changamoto kwa waamini kusitisha safari zao kwa muda, ili kuwahudumia jirani wanaohitaji huruma na upendo. Kristo Yesu amejisadaka na kuwaonea huruma na upendo waja wake na kwa njia hii, atawawezesha waamini kuwa wenye upendo na huruma. Wataweza kukua na kuongezeka katika ut una hivyo kuboresha mahusiano na mafungamano yao yanayorutubishwa kwa huruma na upendo. Waamini wamwombe Kristo Yesu ili awakirimie neema ya kuwa na huruma na upendo kama alivyo yeye mwenyewe!