Mkutano mkuu wa kwanza mjini Vatican umeanza
Vatican News.
Mkutano Mkuu wa kwanza wa Makardinali asubuhi ya leo, tarehe 22 Aprili 2025, umeanza siku moja baada ya kifo cha Baba Mtakatifu Francisko, ambao ulidumu saa moja na nusu, kuanzia saa 3.00 kamili hadi 4:30, masaa ya Ulaya. Waliokuwepo katika Ukumbi wa Sinodi Mpya walikuwa ni makardinali wapatao sitini walioanza kikao hicho kwa muda wa sala kwa ajili ya Papa Francisko na ambaye mazishi yake yatafanyika Jumamosi ijayo tarehe 26 Aprili 2025 mbele ya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro.
Makardinali waliapa kwa kuzingatia kwa uaminifu kanuni za Katiba ya Kitume(Universi Dominici Gregis) kuhusu nafasi ya Kiti kilicho wazi cha Kitume na kuchaguliwa kwa Papa wa Roma, kisha wakaimba(Adsumus Sancte Spiritus),wimbo wa kumuomba Roho Mtakatifu awaangazie. Ibara ya 12 na 13 ya Katiba ya Kitume ilisomwa na Kardinali Joseph Kevin Farrell, Camerlengo wa Kanisa Takatifu Katoliki la Roma, akiwasomea pia waliohudhuria Wosia wa Baba Mtakatifu Francisko uliochapishwa jioni Jumatatu tarehe 21 Aprili 2025.
Mkutano wa Pili wa Baraza la Makardinali utafanyika tarehe 23 Aprili
Katika Muktadha wa Mkutano huo wa Makardinali pia ulitoa uamuzi wa tarehe za uhamisho wa mwili wa Papa na mazishi, kama ilivyotangazwa na Ofisi ya Maadhimisho ya Liturujia za Kipapa hapo awali. Kwa njia hiyo Mkutano wa pili utaendelea kesho Jumatano 23 Aprili, saa 11.00 jioni, masaa ya Ulaya kwa sababu asubuhi makardinali watashiriki ibada ya kuhamisha mwili wa Papa Francisko kutoka katika kikanisa cha Mtakatifu Marta, hadi kuletwa katika Basilika ya Mtakatifu Petro.
Kusitishwa kwa maadhimisho ya kutangazwa mwenyeheri hadi Papa mpya
Katika Mkutano huo mkuu wa Makardinali uliofanyika umetoa pia uamuzi wa kusitisha sherehe za kutangazwa mwenyeheri iliyokuwa imepangwa kufanyika hadi hapo patakapotolewa uamuzi wa Baba Mtakatifu mpya wa Roma.
Misa ya Dominika ya Pili ya Pasaka tarehe 27 Aprili 2025, ambayo pia ni ya huruma ya Mungu, itafanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro ikiongozwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu wa Vatican na itakuwa ni misa ya pili kati ya misa 9 ambazo zinapaswa kusali kwa ajili ya Papa( Novendiali.) Kwa njia hiyo maadhimisho ya misa 9 hizi zitafanyika kila siku saa kumi na moja jioni, masaa ya Ulaya na saa 12 saa za Afrika Mashariki na kati.
Makardinali wa Tume ya kumsaidia Camerlengo wanapigiwa kura
Katika mkutano huo wa kwanza pia makardinali watatu wa Tume inayosaidia Camerlengo kwa maamuzi ya kawaida walipigiwa kura, na hawa ni Kardinali Pietro Parolin, Stanisław Ryłko na Fabio Baggio, mmoja mmoja kwa kila utaratibu ambao Baraza linaundwa: ule wa maaskofu, mapadre na mashemasi. Makardinali hao wa Tume hiyo wanapigiwa kura kila baada ya siku 3.
Sala ya Rozari katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Wakati huo huo, kusali Rozari katika uwanja wa Mtakatifu Petro wa saa 1:30 usiku, umeanza tena kama ilivyo fanyika hata Jumatatu na hivyo hata jioni hii umetangazwa kupitia akaunti ya X ya Sekretarieti ya Vatican @TerzaLoggia. Na sala hiyo itaongozwa na Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali na wakati huo huo hata Baraza la Maaskofu wa Italia wanaungana katika maombi.