杏MAP导航

Tafuta

2025.04.21 PAPA FRANCISKO 2025.04.21 PAPA FRANCISKO 

Maisha ya Papa Francisko kwa ajili ya Kanisa na watu wake!

Kardinali Kevin Joseph Farrell,ambaye ni Camerlengo alitangaza kwa masikitiko kifo cha Baba Mtakatifu Francisko kwa maneno haya:"kaka na dada wapendwa ni kwa huzuni kubwa kwamba sina budi kutangaza kifo cha Baba yetu Mtakatifu Francisko.Saa 1.35 asubuhi ya leo,(Jumatatu 21 Aprili 2025),Askofu wa Roma,Francisko,alirejea nyumbani kwa Baba."Papa alizaliwa katika mji mkuu wa Argentina mnamo tarehe 17 Desemba 1936,mtoto wa wahamiaji wa kutoka Piemonte nchini Italia.

Na Angella Rwezaula - Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameaga dunia Jumatatu asubuhi tarehe 21 Aprili 2025 saa 1.35 kama ilivyotangazwa na Camerlengo wa Kanisa Katoliki la Roma na la mitume, Kardinali Kevin Joseph Farell. Tunakumbuka Papa Francisko kwa masuala mengi. Baba Mtakatifu alikuwa Papa wa kwanza kutoka Amerika ya Kusini na  Mjesuit wa Argentina,  Jorge Mario Bergoglio, na ambaye alikuwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires tangu 1998. Alikuwa ni  mashuhuri katika bara zima na mchungaji rahisi na aliyependwa sana katika jimbo lake, ambaye alisafiri katika sehemu  mbali na mbali, hata kwa njia ya ya ardhi na Bus: "Watu wangu ni maskini na mimi ni mmoja wao," alisema wakati mmoja kuelezea chaguo lake la kuishi katika ghorofa na kupika chakula chake cha jioni. Daima alipendekeza huruma, ujasiri na milango wazi kwa mapadre wake. Kitu kibaya zaidi ambacho kinaweza kutokea katika Kanisa, alielezea katika baadhi ya matukio, "ni kile ambacho mwandishi de Lubac anachokiita ulimwengu wa kiroho," ikiwa na  maana "kujiweka katikati au kimbelembele." Na alipotaja haki ya kijamii, alitualika kuchukua  kusoma  tena katekisimu ya Kanisa Katoliki, Amri Kumi za Mungu na kushiki Heri. Licha ya tabia yake ya aibu, alikuwa mtu wa kumbukumbu kwa nyadhifa zake wakati wa mzozo wa kiuchumi ambao ulitikisa nchi yake mnamo 2001.

Alizaliwa 17 Desemba 1936

Alizaliwa katika mji mkuu wa Argentina mnamo tarehe 17 Desemba 1936, mtoto wa wahamiaji kutoka Piemonte nchini Italia : baba yake Mario alikuwa mhasibu, aliajiriwa kwenye reli, wakati mama yake, Regina Sivori, alitunza nyumba na elimu ya watoto wake watano. Baada ya kufuzu kama fundi wa  kemikali, alichagua njia ya upadre  kwa kuingia katika seminari ya jimbo. Mnamo tarehe 11  Machi 1958, alijiunga na Jumuiya ya Yesu(Wajesuit). Alimaliza masomo yake ya kibinadamu nchini Chile na mwaka wa 1963, aliporudi Argentina, alihitimu katika falsafa katika Chuo cha Mtakatifu  José huko Mtakatifu Miguel. Kati ya 1964 na 1965 alikuwa profesa wa fasihi na saikolojia katika Chuo cha Bikira maria msafi wa Roho  huko Mtakatifu Fé na mnamo 1966 alifundisha masomo yale yale katika Chuo cha Salvador huko Buenos Aires. Kuanzia 1967 hadi 1970 alisoma Taalimungu, na kuhitimu kutoka chuo cha Mtakatifu Yosefu.

Daraja la Upadre 1969

Tarehe 13 Desemba 1969 alipewa daraja la Upadre na Askofu Mkuu Ramón José Castellano. Aliendelea na maandalizi yake kati ya 1970 na 1971 nchini Hispania, na tarehe 22 Aprili 1973 alifunga nadhiri za daima katika shirika la Wajesuit. Huko Argentina, alikuwa Mwalimu wa wanovisi huko Mtakatifu Miguel, profesa katika kitivo cha Taalimungu, mshauri wa Kanda ya Jumuiya ya Yesu na mkuu wa Chuo. Mnamo tarehe 31 Julai 1973 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kanda ya Kijesuit nchini  Argentina. Miaka sita baadaye alianza tena kazi yake katika uwanja wa chuo kikuu na kati ya 1980 na 1986, alikuwa tena mkuu wa chuo cha Mtakatifu José, na vile vile Padre wa  parokia tena huko Mtakatifu  Miguel. Machi 1986 alikwenda Ujerumani kukamilisha shahada  yake ya udaktari; kisha wakuu wake wakamtuma kwa chuo cha Mwokozi huko Buenos Aires na kisha kwa katika jiji la Cordoba, kama mkurugenzi wa kiroho na muungamishi. Alikuwa ni Kardinali Quarracino aliyemtaka kama kuwa mshiriki wake wa karibu huko Buenos Aires. Hivyo tarehe 20 Mei 1992 Yohane Paulo II akamteua kuwa Askofu mkuu wa Auca na msaidizi wa Buenos Aires. Tarehe 27 Juni alipata daraja la uaskofu kutoka mikononi mwa  kardinali mwenyewe katika kanisa kuu.

Kauli mbiu Miserando atque eligendo

Kama kauli mbiu yake alichagua Miserando atque eligendo yaani nilitazama kwa huruma na wakati huo huo kuchagua. Kauli mbiu  hii ya Papa Francisko kwa hakika imemuongoza na inaweza kutafsiriwa kama: kusamehe na kuchagua. Inafafanulia  zaidi kutoka katika Injili yote, Yesu alikaribisha na kusamehe. Msamaha unakuwa chaguo, 'uchaguzi' na katika koti lake aliweka Moto wa IHS, ishara ya Jumuiya ya Yesu. Mara moja aliteuliwa kuwa wa eneo la Flores na tarehe 21 Desemba 1993 akawa makamu mkuu. Basi, haikuwa ajabu wakati tarehe 3 Juni 1997 alipopandishwa wadhifa  na kuwa askofu mkuu mwandamizi wa Buenos Aires. Hata miezi tisa baadaye, baada ya kifo cha Kardinali Quarracino, alimrithi, tarehe 28 Februari 1998, kama askofu mkuu wa Argentina, wa kawaida kwa waamini wa nchi ya Mashariki mwa nchi na kansela mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki. Katika Mkutano wa Baraza la Makardinali  mnamo tarehe  21 Februari 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II alimuumba kuwa Kardinali, na jina la makao yake Mtakatifu  Roberto Bellarmino. Mnamo Oktoba 2001 aliteuliwa kuwa naibu mwandishi mkuu katika mkutano mkuu wa kawaida wa kumi wa Sinodi ya Maaskofu, iliyowekwa kwa huduma ya kiaskofu.

Uinjilishaji 

Katika Bara la Amerika ya Kusini wakati huo huo takwimu yake ilizidi kuwa maarufu. Mnamo mwaka 2002 alikataa kuteuliwa kuwa rais wa Baraza la Maaskofu wa Argentina, lakini miaka mitatu baadaye alichaguliwa na kisha kuthibitishwa tena kwa muhula mwingine wa miaka mitatu mwaka 2008. Wakati huo huo, mwezi wa Aprili 2005, alishiriki katika Baraza la Makardinali  la Uchanguzi  ambalo lilimchangua Papa Benedikto XVI. Akiwa Askofu Mkuu wa Buenos Aires - wenyeji milioni tatu, alifikiria juu ya mipango ya kimisionari inayozingatia ushirika na uinjilishaji. Malengo makuu manne yalikuwa: jumuiya zilizo wazi na za kidugu, jukumu kuu la walei wanaofahamu; uinjilishaji unaolenga kila mkazi wa jiji, msaada kwa maskini na wagonjwa, na kuwaalika makuhani na walei kufanya kazi kwa pamoja. Mnamo Septemba 2009, alizindua kampeni ya mshikamano wa kitaifa kwa miaka mia mbili ya uhuru wa nchi: kazi mia mbili za upendo zitakamilishwa ifikapo mwaka 2016. Na, katika ngazi ya bara, alikuwa na  matumaini makubwa kutokana na ujumbe wa Kongamano la Aparecida la mwaka 2007, hadi kulifafanua kuwa kama "Evangelii nuntiandi ya Amerika ya Kusini". Alichaguliwa kuwa Papa wa Roma  tarehe 13 Machi 2013 na leo hii tarehe 21 Aprili 2025 amerudi kwa Mungu Baba Mwenyezi akiwa na umri wa miaka 88.

Maisha ya Papa
21 Aprili 2025, 11:33