Papa Leo XIV kwa wanahija wa Congo,kwa Floribert:Jumuiya inaweka watu wote kwenye meza moja
Na Angella Rwezaula–Vatican.
Jumatatu tarehe 16 Juni 2025, Baba Mtakatifu Leo XIV alikutana na wanahija waliokuja kwa ajili ya fursa ya kutangazwa Mwenyeheri Floribert Bwana Chui, aliyetangazwa Dominika tarehe 15 Juni 2025 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta Roma. Akianza hotuba yake, kwa Ishara ya Msalaba, Papa aliwakaribisha kwa furaha baada ya tukio hilo. Aliwasalimia maaskofu waliokuwapo kwa namna ya pekee wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Askou wa Goma, jimbo ambapo aliishi mwenyeheri mpya. Alimsalimia Mama na familia ya Mwenyeheri Floribert kama vile Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ambamo alikuwa mshirika.
Kijana huyo alikutana na kifo cha kishahidi huko Goma kunako tarehe 8 Julai 2007. Maneno ya Mpandwa Hayati Papa Francisko yanamkumbuka akiwaelekea vijana huko Kinshasa, wakati wa ziara yake ya Kitume nchini Congo kuwa: “Kijana kama ninyi Floribert Bwana Chui: (…) akiwa na miaka 26 tu aliuawa huko Goma kwa sababu ya kuzuia kuingiza bidhaa za chakula zilizoharibika, ambazo zingeleta madhara ya afya ya watu(…). Akiwa Mkristo, alisali, akawafikiria wengine na akachagua kuwa mnyoofu, akisema hapana kwa uchafu wa ufisadi. Huku ni kubaki na mikono safi, wakati mikono inayotumia pesa haramu ikichafuliwa na damu. Kuwa mwaminifu ni kung'aa mchana, ni kueneza nuru ya Mungu, ni kuishi furaha ya haki: shinda uovu kwa wema!" (2 Februari 2023).
Papa Leo XIV aliuza swali kuwa “je Kijana alipata wapi nguvu ya kupinga ufisadi, uliokita mizizi katika fikra za sasa na uwezo wa kufanya vurugu zozote? Chaguo la kuwa na mikono yake safi akiwa Afisa wa forodha - alikomaa katika dhamiri iliyoundwa na sala, kwa kusikiliza Neno la Mungu, kwa ushirika na ndugu zake. Aliishi hali ya kiroho ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ambayo Papa Francisko aliifupisha kwa "P" tatu za kiitaliano; (Preghiera,Poverta e Pace’, ikiwa na maana: sala, maskini, amani. Maskini walikuwa na maamuzi katika maisha yake. Mwenyeheri Floribert aliishi maisha ya kujitolea na watoto wa mitaani, waliosukumwa na vita kwenda Goma, waliodharauliwa na yatima. Aliwapenda kwa mapendo ya Kristo: alipendezwa nao na kujali kuhusu malezi yao ya kibinadamu na ya Kikristo. Nguvu ya Floribert ilikua katika uaminifu kwa maombi na kwa maskini.
Rafiki mmoja alimkumbuka kuwa: "Alikuwa na hakika kwamba tulizaliwa kufanya mambo makubwa, kuwa na matokeo kwenye historia, kubadilisha ukweli." Alikuwa mtu wa amani. Katika eneo lenye mateso kama Kivu, lililokumbwa na vurugu, aliendelea na vita vyake vya amani kwa upole, akiwatumikia maskini, akifanya mazoezi ya urafiki na kukutana katika jamii iliyovunjika. Mtawa mmoja alikumbuka kwamba alisema: "Jumuiya inaweka watu wote kwenye meza moja." Kijana huyu, hakukubali kabisa uovu, aliota ndoto, ambayo ililishwa na maneno ya Injili na ukaribu na Bwana.
Vijana wengi walihisi kuachwa na bila tumaini, lakini Floribert alisikiliza neno la Yesu: "Sitawaacha ninyi yatima; nitakuja kwenu" (Yh 14:19). Hakuna ardhi iliyoachwa na Mungu! Aliwaalika marafiki zake kutokata tamaa na kutoishi kwa ajili yao wenyewe. Licha ya kila kitu, alionesha imani katika siku zijazo. Alisema: "Bwana anatayarisha ulimwengu mpya, ambapo vita havitakuwapo tena, chuki itafutwa, jeuri haitaonekana tena kama mwizi usiku ... watoto watakua kwa amani. Ndiyo, ni ndoto kubwa. Tusiishi, basi, kwa kile kisichofaa. Hebu tuishi badala ya ndoto hii kuu!"
Kwa kuhitimisha, Papa Leo alisema “shahidi huyo wa Afrika, bara tajiri la vijana kwake anaonesha kuwa inawezekana kuwa na msimamo wa amani na kuondoa silaha. Mlei huyo wa Congo anaweka mwanga wa thamani msingi wa ushuhda wa walei na vijana.” Kwa njia hiyo “tunaweza kuomba wa maombezi ya Bikira Maria na Mwenyeheri Floribert kutimiza kwa haraka utulivu wa Kivu, huko Congo na Afrika yote.