Jumuiya ya Mt.Egidio:Juni 15,Mtumishi wa Mungu Floribert Bwana Chui,atatangazwa kuwa Mwenyeheri
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, kwa furaha inatangaza kuwa tarehe 15 Juni 2025, katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta, Mtumishi wa Mungu Floribert Bwana Chui, atatangazwa kuwa Mwenyeheri katika misa itakayofanyika saa 11,30 jioni ambayo itaongozwa na Kardinali Marcello Semerero, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu. Maadhimisho hayo yatawaona washiriki kutoka Jimbo la Goma kuanzia na Askofu wake Willy Ngumbi, na wawakilishi wa Kanisa la Congo, miongoni mwao Kardinali Fridolin Ambongo, Askofu Mkuu wa na Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu katoliki Afrika(SECAM).
“Tunatoa shukrani kwa ushuhuda wa imani na utakatifu wa kijana huyu aliyeshiriki maisha ya Jumuiya kwa upendo kwa maskini na ulinzi wa watoto wadogo. Kwa upande wa maisha yake, Floribert, afisa wa forodha katika mpaka na Rwanda, akifanya kazi tangu alipokuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu katika Shule ya Amani ya Mtakatifu Egidio huko Goma, alikataa kuruhusu, kupewa fedha chafu ya mizigo ya vyakula vilivyoharibika ambavyo vingeweka maisha ya maskini zaidi hatarini,” inabainisha taarifa ya kuelezea wasifu wa Mtumishi wa Mungu huyo.
2007 aliteswa na kuuawa
Kwa njia hiyo ya kupinga katika hilo, “mnamo Julai 2007, aliteswa na kuuawa akiwa na umri wa miaka ishirini na sita tu. Kuuawa kwake kwa imani “kwa kuchukia imani yake” kulitambuliwa mnamo Novemba mwaka 2024 na Papa Francisko na hivyo kutengeneza njia ya kutangazwa mwenyeheri, kwani ndiyo kunahusishwa na tukio la ufisadi na miungu ya pesa kwa gharama yoyote ile, ambayo inachafua mustakabali na matumaini ya Afrika.” Aidha “Upinzani wake dhidi ya maovu ni ishara ya matumaini na ufufuko kwa eneo linaloteswa la Kivu, ambalo limevuka kwa miaka mingi na vita vya wenyewe kwa wenyewe, vyenye uchungu, ambavyo vimezidi kuwa vibaya katika miezi ya hivi karibuni, lakini pia kwa vijana wote wa bara ambao wanawakilisha idadi kubwa ya watu wake,” inabainisha taarifa.
Papa Francisko:kama mkristo alisali akawafikiria wengine na kuwa mnyoofu
Kwa maneno haya Baba Mtakatifu Francisko alimkumbuka tarehe 2 Februari 2023, katika Uwanja wa Mashahidi mjini Kinshasa, wakati wa ziara yake ya Kitume katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwamba: “Kijana wa aina yake Floribert Bwana Chui akiwa na umri wa miaka ishirini na sita tu aliuawa huko Goma kwa kuzuia kupitisha bidhaa za vyakula vilivyoharibika ambavyo vingeweza kuharibu afya za watu, angeweza kuviachia wasingeligundua na hata angepata faida. Lakini, akiwa Mkristo, alisali, akawafikiria wengine na akachagua kuwa mnyoofu, akisema hapana kwa uchafu wa ufisadi. Huku ni kuweka mikono yako safi, huku mikono ambayo pesa za ufisadi huchafuliwa na damu. Mtu akikukabidhi bahasha, akakuahidi neema na utajiri, usiingie kwenye mtego, usidanganywe, usijiruhusu kumezwa na dimbwi la uovu. Usijiruhusu kushindwa na uovu, usiamini katika njama za giza za pesa, ambazo hukufanya kuzama usiku. Kuwa mwaminifu kunang'aa mchana, ni kueneza nuru ya Mungu, ni kuishi furaha ya haki: shinda uovu kwa wema!" Alisisitiza Papa Francisko wakati wa mahubiri yake.