杏MAP导航

Tafuta

'Kijana wa mwoyo safi',Floribert Bwana Chui atatangazwa Mwenyeheri

Papa Francisko wakati wa Ziara ya Kitume nchini DRC kunako Februari 2023 mbele ya vijana wengi alitoa wito kwa taifa kwamba:“ufisadi ukome.“Ushuhuda wa Floribert Bwana Chui “Nguvu dhaifu ya mwamini,ambaye alipinga uovu kwa manufaa ya watu wake, inatupatia matumaini ya Afrika na Ulimwengu usio na ufisadi.”Kijana mwenye moyo safi,”Video ya Papa pia picha na shuhuda kumhusu kijana shahidi atakayetangazwa Mwenyeheri 15 Juni 2025.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Tarehe 15 Juni 2025 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta, Roma, saa 11.30 masaa ya  Ulaya, Kijana Floribert Bwana Chui, atatangazwa na kuwa Mwenyeheri , kijana wa Congo aliyekuwa wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, shahidi wa Ufisadi. Maadhimisho hayo yataongozwa na Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu kwa niaba ya Baba Mtakatifu. Kwa mujibu wa Jumuiya hiyo ilitangaza kuwa maadhimisho hayo yataona ushiriki wa waamini kutoka Jimbo katoliki la Goma kuanzia na Askofu wake Willy Ngumbi, na wawakilishi wengine wa Kanisa la Congo, miongoni mwake akiwemo Kardinali Fridolin Ambongo, Askofu Mkuu wa Kinshasa.

Katika kumbuka Mtumishi wa Mungu, Wakati wa Ziara yake Hayati Baba Mtakatifu Francisko kunako Februari 2023 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,  akikutana na vijana waliokusanyika katika Uwanja wa Mashahidi huko Kinshasa, alisisitiza juu ya kijana huyo wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio huko Goma ambaye alikuwa anafanya kazi kwenye mpaka kati ya Congo na Rwanda, na ambaye alikataa kuingiza bidhaa za vyakula vilivyoharibika kwa hongo ya pesa na kwa sababu hiyo aliteswa sana na mwishowe akauawa. Papa Francisko alisema: “Kijana kama ninyi Floribert Bwana Chui akiwa na umri wa miaka ishirini na sita tu aliuawa kule Goma kwa kuzuia upitishaji wa vyakula vilivyoharibika ambavyo vingeharibu afya za wananchi, angeweza kuviachia wasingeligundua na hata angepata faida."

Papa Francisko na mkutano na Vijana huko DRC 2023

Akiendelea Papa Francisko aliongeza "Lakini, akiwa Mkristo, alisali, akawafikiria wengine na akachagua kuwa mnyoofu, akisema hapana kwa uchafu wa ufisadi. Huku ni kubaki mikono safi, wakati mikono inayotumia pesa haramu ikichafuliwa na damu. Mtu akikukabidhi bahasha, akakuahidi neema na utajiri, usiingie kwenye mtego, usidanganywe, usijiruhusu kumezwa na dimbwi la uovu. Usijiruhusu kushindwa na uovu, usiamini katika njama za giza za pesa, ambazo hukufanya kuzama usiku. Kuwa mwaminifu ni kung'aa mchana, ni kueneza nuru ya Mungu, ni kuishi furaha ya haki: shinda uovu kwa wema!" Nguvu dhaifu ya mwamini, ambaye alipinga uovu kwa manufaa ya watu wake, inatupatia matumaini ya Afrika na ulimwengu usio na ufisadi,"alisema Papa Francisko.

Furaha ya mama, Gertrude Kamara Ntawiha

Gertrude Kamara Ntawiha, mama yake Floribert, akihojiwa alionesha furaha yake na shukrani kwa habari ambayo inatuliza maumivu ambayo alikuwa amezama baada ya kifo cha kusikitisha cha mwanawe. Kwa kushuhudia alisema: "Floribert  aliuawa kwa jina la imani yake ya Kikristo, kwa kukataa pendekezo la hongo lililolenga kuwezesha kuingia kwa bidhaa za chakula ambazo zingeweza kuhatarisha afya ya umma katika eneo la Congo. Alifanya uchaguzi wake kwa Mungu hadi mwisho na akachagua kufa ili kuishi ndani ya Kristo.” Hata hivyo Mama Gertrude aliwaomba vijana kuiga mfano wa Floribert, "kutokubali kupotoshwa na kufuata tunu za Injili." Aidha  Mama huyo aliomba "mamlaka ya Congo amani, hasa katika eneo la mashariki mwa DRC ambako Floribert aliuawa na ambako wakazi wamekuwa wakiishi kwa tabu kwa zaidi ya miongo mitatu, chini ya tishio la makundi yenye silaha na uchokozi wa baadhi ya nchi jirani."

Mama Gertrude  Kamara Ntawira
Mama Gertrude Kamara Ntawira

Kaka:Kifo cha Floribert hakikuwa bure

Kwa "uaminifu na uadilifu wake wa kimaadili, Floribert Bwana Chui ni mfano sio tu kwa vijana wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, lakini pia kwa wale ulimwenguni kote," alisisitiza haya  Trésor, kaka mdogo wa Floribert. "Kwangu mimi, vita vyake havikuwa vya bure, alidumisha uhuru wake. Huu ni mfano kwetu sisi Wakristo, Wakatoliki, vijana duniani kote, na hasa kwa wale wa Congo, ambako vitendo vya rushwa bado vinapaswa kupigwa vita”, alisema kijana huyo wa Kikongo, ambaye kwa mujibu wa kutangazwa kuwa mwenyeheri kaka yake aliongeza "lazima kuibue hisia za walimwengu katika ukweli huu wa kusikitisha ambao unakuwa njia ya kujipatia faida zisizo na uwiano. Mfano wa Floribert unaweza kutusaidia "kuwa waadilifu zaidi na wenye kushikamana, kwa sababu pesa au bidhaa za ulimwengu huu haziwezi kushinda kila wakati", alisisitiza Trésor.

Kaka mdogo wa Frolibert
Kaka mdogo wa Frolibert

Kuomba ili janga la ufisadi liishe

Trésor bado anaendelea kudumisha kumbukumbu ya kaka yake mkubwa kama mtu wa kuigwa. "Alikuwa na njia yake ya kuishi maisha ya Kikristo, aliishi kwa hofu ya Mungu.” Floribert alihusika katika vikundi na Harakati mbalimbali ya kikanisa, alikuwa mvulana anayetumikia katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu huko Goma, alikuwa sehemu ya kwaya ya Kilatini ya Parokia ya Roho Mtakatifu. "Aliimarisha zaidi imani yake kwa kushiriki Injili katika Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ambapo alikuwa rafiki na ndugu, pamoja na wale waliohitaji sana, ikiwa ni pamoja na watoto wa mitaani."

Ikiwa Trésor angekuwa na ujumbe kwa Floribert,  alisema kwamba angemwomba  ili aombe kwa Muumba "kwa ajili ya Congo na kwa ajili ya dunia nzima, ili janga hili la ufisadi, uovu huu mbaya, ukome na tutembee katika haki." Mdogo wake aliongeza kusema kuwa "Floribert, ameweza kuhifadhi uhuru wake na hivyo aliishi maisha yake kama Mkristo mfululizo." Akifanya maneno ya Papa Francisko kuwa yake mwenyewe, Trésor alisisitiza kwamba: " Floribert angeweza kupata pesa nyingi kwa kushindwa na vishawishi, lakini kinyume chake, anaeleza, "alichagua kuwa mnyoofu, kukataa uchafu wa uharibifu wa maadili. Maneno ya Papa Francisko yanapaswa pia kuwatia moyo wanasiasa wetu katika maisha yao."


Floribert Bwana Chui, afisa kijana aliyejitolea

Désiré Pengele, afisa katika Idara ya Kamishna wa Ofisi ya Udhibiti ya Congo (OCC), alimwongoza Floribert Bwana Chui katika hatua zake za kwanza ndani ya Taasisi hiyo, huko Kinshasa. Wakati huo, vijana wapya walioajiriwa wa OCC, waliopewa idara hii, walikabidhiwa kwake kufuatwa katika mchakato wao wa kujumuisha. Kwa upande wake alibainisha kuwa: "Kati ya wimbi jipya la wahitimu vijana waliofika kati ya 2006 na 2007 pia kulikuwa na Floribert kijana sana." Karibu na ofisi zao huko Gombe, mji ulio katika mji mkuu wa Congo, kuna Parokia ya Mtakatifu Anna, ambapo misa mbili huadhimishwa kila asubuhi, ya kwanza kwa waamini na ya pili kuanzia saa 1.00 hadi 1:30, kwa Wakristo ambao wameondoka nyumbani mapema kwenda Gombe kufanya kazi lakini ambao wanachukua fursa ya kusali kabla ya kwenda kazini, na ndipo - Désiré alianza pamoja na kijana hyuo Floriberti."

Urafiki wa kiroho, zaidi ya mahusiano ya kazi

Hivi ndivyo urafiki wa kiroho ulizaliwa, ambao ulikwenda zaidi ya uhusiano rahisi wa kazi.  Kwa mujibu wa Afisa huyo alisema kuwa "Floribert kila mara alikuwa na vitabu naye na alisoma sana, alikuwa mwenye busara na alijifunza mengi. Aliendelea hivyo hata aliporudi Goma, kufuatia uhamisho kwa sababu za kibinafsi. Mwisho wa Juma moja kabla ya kifo chake, Désiré alisema avyoota ndoto, usiku kati ya Dominika na Jumatatu, ambamo Floribert aliniambia, mara tatu: 'Pengele, subiri." Akiwa hajaelewa chochote, msimamizi huyo wa zamani alijaribu kumpigia simu kwa namba yake ya simu mapema Jumatatu asubuhi, akifikiri kwamba huenda anahitaji hati inayohusiana na kazi, kama alivyofanya mara kwa mara. Lakini kwa bahati mbaya simu haikulia.”

Hata hivyo baada ya kile kilichotokea cha mauaji ya mateso Mkuu wa Idara hiyo alikwenda peke yake katika mji mkuu wa Kivu Kaskazini kuhudhuria mazishi. Wenzake wengine waliadhimisha misa. Kwa mujibu wake alisema: "Nadhani nilimwona mara mbili katika ndoto. Na hatimaye, kwa furaha yangu kuu, nilifahamu kwamba Baba Mtakatifu Francisko alimwinua  kuwa Mtumishi wa Mungu na kwamba baadaye angetangazwa kuwa mwenyeheri na nimekuwa nikizungumza kila mara kuhusu Floribert, nikiwa na matumaini kwamba anaiombea nchi yetu, vijana wetu na kwa ajili ya kampuni yetu, Ofisi ya Uthibiti ya Congo.

12 Juni 2025, 11:05