杏MAP导航

Tafuta

2025.06.10 Floribert Bwana Chui Bin Kositi 2025.06.10 Floribert Bwana Chui Bin Kositi 

DRC:Kuheshimu ujasiri na uaminifu:Kutangazwa mwenyeheri kwa Floribert Bwana Chui

Tarehe 15 Juni,Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Ukuta huko Roma,Italia,litashuhudia kutangazwa mwenyeheri kwa Floribert Bwana Chui Bin Kositi,kijana kutoka Congo mwanachama wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio,shahidi aliyesimama kidete kupinga ufisadi.Sherehe hizo zitaongozwa na Kardinali Marcello Semeraro,Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Watakatifu.

Na Padre Paul Samasumo – Vatican.

Papa Francis akikumbuka kijana Floribert Bwana Chui alisema: “Ninafikiri kuhusu ushahidi uliotolewa na kijana kama nyinyi, Floribert... mwenye umri wa miaka ishirini na sita tu, aliuawa huko Goma kwa kuzuia kupita vyakula vilivyoharibika ambavyo vingeweza kudhuru afya za watu.  Kama angeweza kufumbia macho kwa urahisi; hakuna mtu ambaye angejua, na angeweza hata kupata faida. Lakini, akiwa Mkristo, alisali. Aliwafikiria wengine na kuchagua uaminifu, akisema hapana kwa ufisadi. Hiyo ndiyo maana ya kuweka mikono na moyo wako safi.” Baba Mtakatifu Francisko alieleza maneno haya kwa maelfu ya vijana wa Congo waliokusanyika katika Uwanja wa michezo mjini Kinshasa tarehe 2 Februari 2023 wakati wa Ziara yake ya Kitume katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Kubeba tukio hili kwa maombi

Katika barua ya hivi karibuni ya tarehe 20 Aprili 2025, ikitangaza kutangazwa mwenyeheri kwa Jimbo la  Goma, Askofu wa Kawaida wa Jimbo hilo, Willy Ngumbi Ngengele, M. Afr., alizungumza juu ya kutangazwa kuwa mwenyeheri kama mmiminiko wa matumaini kwa watu wa Congo. Alisema kuwa Jimbo la Goma litaadhimisha Mwenyeheri mpya tarehe 8 Julai 2025 katika mji wa Goma.

"Napenda kutangaza mapema kwamba hapa Goma, tutafanya Misa takatifu kwa heshima ya Floribert Bwana Chui Jumanne, tarehe 8 Julai 2025, siku ya kumbukumbu ya kifo chake. Tayari atakuwa ametangazwa kuwa Mwenyeheri," alisema Askofu Ngumbi. Aliendelea kusema, “Kutangazwa kwake kuwa mwenyeheri, kwa Kanisa la Congo kwa ujumla, na kwa Jimbo la Goma hasa, ni mmiminiko wa matumaini na sababu ya kumshukuru Bwana, ambaye anatuonesha maajabu yake daima.

Kifo cha Floribert  Bwana Chui Bin Kositi, kimsingi ni heshima kwa walei na vijana wetu, wito kwa sisi sote kujitolea kwa undani zaidi haki, amani na udugu katika imani na imani kwa Kristo Mfufuka. Tunapongojea siku hii ya furaha, sasa ninawaalika wana na binti wote wa Jimbo letu, pamoja na watu wote kwa nia njema, kubeba tukio hili katika sala,” alisema Askofu wa Goma. Floribert Bwana Chui atakuwa wa nne kuwa mwenyeheri katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, kufuatia kutangazwa mwenyeheri Anuarite Nengapeta, Isidore Bakanja, na Padre Albert Joubert—aliyeuawa pamoja na wamisionari watatu wa Shirika la Mtakatifu Xaveri huko Uvira, mashariki mwa DRC.

Floribert alikuwa nani?

Kulingana na Maelezo ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Floribert alizaliwa tarehe 13 Juni 1981 huko Goma, mji mkuu wa Kivu Kaskazini, mashariki mwa Congo. Alikulia katika eneo lililokumbwa na migogoro na machafuko kwa muda mrefu. Goma na eneo la mashariki mwa DRC kwa sasa linakaliwa na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao walichukua udhibiti wa mji huo mwishoni mwa Januari 2025 kufuatia mashambulizi. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio  inaeleza kuwa Goma ni eneo lenye utajiri wa asili na utajiri wa madini; hata hivyo, pia ni eneo tata la kisiasa na lenye matatizo, lililoathiriwa na ghasia za muda mrefu za miaka mingi.

Masomo ya Floribert yaliishia katika digrii ya sheria. Hapo awali alifanya kazi katika Ofisi ya Uthibiti mjini Kinshasa, ambyo ni wakala wa serikali unaohusika na udhibiti wa ubora wa bidhaa kutoka nchi nyingine. Baada ya kipindi cha mafunzo katika jiji kuu—ambapo fursa zilikuwa nyingi—Floribert alichagua kurudi Goma, mji wa nyumbani kwao. Licha ya umri wake mdogo, Floribert alifanya matokeo makubwa katika ofisi ya forodha ya Goma. Tofauti na watangulizi wake, alikataa kupokea rushwa ili kupitisha vyakula vilivyooza au vichafu. Uadilifu wake hatimaye uligharimu maisha yake, kwani aliteswa na kuuawa kwa kukataa kwake kusalitiwa na ufisadi.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ilizungumza juu ya furaha yake kwamba mmoja wa washiriki wake alikuwa akitambuliwa na Kanisa la ulimwengu kwa uaminifu na imani yake. "Tunatoa shukrani kwa ushuhuda wa imani na utakatifu wa kijana huyu, ambaye alishiriki maisha ya Jumuiya kwa upendo kwa maskini na ulinzi wa watoto wadogo," inasomeka sehemu ya taarifa ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio. Jumuiya hiyo  pia ilieleza kuwa maadhimisho hayo yatakayofanyika mjini Roma yatahudhuriwa na Jimbo la Goma likiongozwa na Askofu wake Willy Ngumbi na wawakilishi wengine wa Kanisa la Congo akiwemo Kadinali Fridolin Ambongo wa Kinshasa.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ni Jumuiya ya Kikristo iliyoanzishwa mwaka 1968, muda mfupi baada ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Ilianzishwa na Bwana Andrea Riccardi jijini Roma, imeibuka kuwa Mtandao wa kimataifa na uwepo katika zaidi ya nchi 70. Jumuiya inalenga kufikia kando kando ya maeneo hasa kwa kuhudumia watu waliotengwa na walio katika mazingira magumu, kwa kusikiliza Injili na kujitolea kwa hiari na kwa uhuru kuwasaidia maskini na kuendeleza amani.

10 Juni 2025, 15:07