Ask,Mapunda kwa VIWAWA:tupokea Sakramenti ya Kitubio na Ekaristi chemichemi ya uzima
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kiini cha Heri za Mlimani, kiliongoza ufafanuzi mpana zaidi wa Askofu Edward Elias Mapunda, wa Jimbo Katoliki la Singida, na Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Kichungaji kwa ajili ya Walei ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania(TEC), wakati akiongoza Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la VI Kitaifa, la Vijana Wakatoliki wafanyakazi(VIWAWA),tarehe 23 Agosti 2025, lililofanyika katika Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya nchini Tanzania. Akianza kudadavua Injili iliyosomwa, Askofu alisema, Ndugu zangu katika Injili, Yesu inatuambia kuhusu heri. Heri ni mhutasari wa maneno yote yaliyo andikwa katika Biblia nzima. Jinsi Yesu alivyo na tabia yake, tunahitaji Roho Mtakatifu ili tuweze kuzifahamu heri hizo za Injili na kumjua Yesu Kristo. Heri ni hekima ya kimungu. Heri ni sheria au ratiba ya utakatifu, mtu mwenye kutekeleza heri ni mtakatifu ni mtu wa Mungu ni rafiki ya Mungu.
Ndugu zangu kuwa Mtakatifu si lelemama ni kazi sisi sote tumealikwa kuwa watakatifu na wajibu wetu sisi vijana ni kuutakatifuza Ulimwengu, huu ndiyo utume wa walei, kuutakatifuza Ulimwengu, kuufanya Ulimwengu, kumjua Mungu, kumpenda Mungu na kumuabudu Mungu, na kumtumikia Mungu. Huu ndio utume wetu kama vijana, sisi wenyewe kuutafuta utakatifu, na kuufanya Ulimwengu uwe Mtakatifu, Ulimwengu umtukuze Mungu. Heri ya Injili siyo raha au starehe burudani, Yesu anataka kutuambia furaha ya kweli haipatikani katika anasa au katika dhambi Kwa heri hizi, Yesu anatuambia sisi vijana, furaha ya kweli haipatikani katika anasa au katika dhambi, furaha ya kweli inapatikana katika kuishi maisha matakatifu. Heri hizi zinaleta furaha ya ndani, furaha ya kweli na furaha ya kudumu. Mtakatifu Augustino kwa miaka kumi na nne (14) alitafuta furaha katika uzinifu, je alipata furaha?, Alipata aibu na huzuni. Alipata furaha wakati alipongoka na kumpenda Mungu kwa moyo wake wote, Augustino alipata furaha kubwa.
Ndugu zangu, kuziishi hizi heri si jambo jepesi na si jambo rahisi, tunahitaji neema na baraka za Mungu ili tuweze kuziishi heri hizi tunaalikwa kwanza: kuwa watu wa sala, tunalikuwa sisi vijana kuwa watu wa sala, kwa mfano, tutakuwaje watu wa usafi wa moyo? Maana Yesu amesema: “heri wenye Moyo safi maana hao watamuona Mungu.” Sasa usafi wa moyo si jambo jepesi, si jambo rahisi, linahitaji msaada wa mungu. Sasa tunaalikwa tusali. Sala ni amri, sala ni sheria, ni agizo. Yesu ametuambia “tusali ili tusiingie majaribuni,”… tusali ili tupate nguvu ya kuwa na moyo safi, ili tumuone Mungu, tusali ili kuwa masikini wa Roho, tusali ili kuwa watu wenye huzuni, lakini huzuni wa dhambi. Kijana asiye Sali ana hali ipi? Kijana asiye sali Jumapili, kwenye Jumuia anakuwa na hali gani? … hali mbaya, ni wakuhurumiwa, hali ya kufa kifo cha pole pole. Kwa hiyo kijana unaalikwa kusali.
Ninashukuru kwenye mada, sala imesisitizwa, kwa sababu sala ndiyo nguvu ya kupambana na maovu, sala ni nguvu ya ushindi, ni sala kuungana na Mungu. Asiye sali, anakufa pole pole, kwa hiyo kijana unaalikwa kusali, uwe mstari wa mbele kwenye Jumuia, uwe mstari wa mbele kanisani, uwe mstari wa mbele kumtanguliza Mungu katika maisha yako, na hapo maisha yako ya tafanikiwa. Lakini pia nawaalika vijana kusoma na kutafakari Neno la Mungu, kijana uwe rafiki wa Maandiko Matakatifu. Bahati nzuri siku hizi simu zetu, ndani wameweka Biblia si ndiyo? Sasa soma, tusiangalie tu mambo mengine. Tupate muda wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu.
Mtakatifu Paulo amesistiza sana umuhimu wa kutafakari, umuhimu wa kusoma Neno la Mungu. Tena ukisoma katika Waraka wake wa Wakolosai, 3:16 anasema: “Neno la Kristo na likae kwa wingi, ndani yenu, katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa Zaburi na nyimbo na Tenzi za rohoni huku mkimuimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.” Sasa Neno la Mungu litakaaje kwa wingi mioyoni mwenu na ndani yako, kama husomi na kutafakari? Tusome na kutafakari Neno la Mungu, huu ndiyo msisitizo mkubwa sana. Tusisubiri kusomewa tu, vijana wengine hata hawana Biblia. Vijana wengine tikiuliza ni nani hapa ana Biblia tutakuwa na kizungumkuti. Je nani aliyefika na Biblia kwenye Kongamano hili?... Nani aliyefika amebeba Biblia?... Umebeba simu?... Mbona hujasoma tafakari tangu juzi?... Unasoma meseji za wapi hizo?... Meseji za Kongamano?... Kwa hiyo tusome Neno la Mungu, limeandikwa kwa ajili yetu, limeandikwa kwa ajili ya wokovu wetu na uzima wetu, kwa hiyo, tulisome na kutafakari, ili litusaidie katika maisha yetu.
Lakini jambo lingine ambalo Baba Lukoo amesisitiza jana ni ulazima wa kupokea Sakramenti ya kitubio, Sakramenti ya Upatanisho. Kwa hiyo vijana tupende kupokea Ekaristi Takatifu, chemichemi ya uzima wetu. Kwanza kabisa tunaalikwa tutambue uwepo wa dhambi, kwa sasa kuna changamoto hapo watu kutotambua uwepo wa dhambi. Yaani mtu anafanya jambo, anajua ni dhambi, lakini anaona siyo dhambi, si ndiyo? Mtu anapokea rushwa, lakini hajui kama hiyo ni dhambi. Mtu ni shoga lakini hajui kama hiyo ni dhambi ya mauti, anaona ni sawa tu. Neno dhambi lilishapotea, si ndiyo? Sasa leo tusilipoteze neno hilo, kijana asiye pokea sakramenti ya kitubio ana hali gani? …. Kijana asiye pokea sakramenti ya kitubio amekufa kiroho au kuna lugha nyingine nyepesi tunayoweza kusema.... Leo tutapokea Rehema kamili, lakini Rehema kamili inadai kitubio, ili upate Rehema kamili unahitaji kupokea Sakramenti ya Kitubio.
Kwa hiyo vijana tukapokea Sakramenti ya Kitubio, tupokee Ekaristi Takatifu, chemichemi ya uzima wetu. Ekaristi Takatifu ni chemichemi ya uzima wetu. Yesu ametuambia: “ anayekula mwili wangu na kuinywa damu yangu hukaa ndani yangu na mimi ukaa ndani yake, anayekula mwili wangu na kuinywa damu yangu ataishi milele.”() Hii ni Sakramenti ya mtu asiye taka kufa, kama hutaki kufa, upoke Sakaramenti ya Kitubio na Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, chemchemi ya uzima, kiini na kilele cha maisha ya mkristo, kiini na kilele cha maisha ya kijana. Kijana asiyepokea Ekaristi maisha yake, yakoje?... kijana huyo ni shahidi wa Kristo?... Kwa hiyo, tukazi e mambo haya, tukazie sala, maisha ya sala, tukazie kusoma na kutafakari Neno la Mungu, tukazie maisha ya kupokea Sakramenti ya Kitubio na kupokea Sakramenti ya Ekaristi Rakatifu, tutakuwa hai, hatutakuwa hoi, tutakuwa vijana hai, hatutakuwa vijana hoi.
Kwa hiyo, vijana, napenda kuchukua nafasi kuwashukuru sana kwa kuja kwenye Kongamano hili, limefana sana, hongereni. Kongamano letu la sita, kitaifa la VIWAWA Mwaka huu, hapa Jimboni Mbeya limefana sana! Asanteni kwa kuwa usikivu, asanteni kwa sala, asanteni kwa kuyapokea mafundisho, kuwa wapya. Kanisa Katoliki linatosha, sema: Kanisa Katoliki linatosha..! Hatuta tangatanga katika imani,… katika ushirikina… Kanisa Katoliki linatosha, kutufikisha mbinguni. Kuna Sakramenti ya Kitubio na kila kitu kipo, kwa kuzaliwa katika Kanisa moja Takatifu la Mitume. Basi ninaomba tena kwa mara nyingine nili shukuru Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya, kutukaribisha hapa Jimboni Mbeya kwa ajili ya hija yetu, Kongamano letu la Sita la VIWAWA Kitaifa. Asante sana Baba Askofu Mkuu. Asante sana kwa upendo na ukarimu, asante kwa mapokezi mazuri, tumefurahi, tumeenjoy hapa mbele. Asante Baba Mwasekaga Godfrey, asante sana! Asante Mapadre wa Mbeya. Asante Watawa, asante Waamini kwa upendo na ukarimu.
Ninaomba tuwashangilie tena wanambeya…. Asante ni Mapadre wote, asanteni watawa, asanteni watoa mada, asanteni wanahabari, asanteni kamati, asante Profesa Haule na wote, asanteni sana kwa upendo na ukarimu Mungu aendelee kuwabariki asanteni.
Ndpo tumefikia mwisho wa Mahubiri marefu ya Mwashamu Askofu Edward Elias Mapunda wa Jimbo Katoliki la Singida, Tanzania, Mwenyekiti wa Idara ya Walei ya Baraza la maaskofu katoliki nchini Tanzania (TEC) aliyofanya tarehe 23 Agosti 2025, wakati wa Kufunga Kongamano la 6 Kitaifa la Vijana wakatoliki wafanyakazi(VIWAWA). Shukrani kwako Baba Askofu kwa tafakari hii, ambayo Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican, imependa kuyachapisha jinsi ilivyo yahubiri kwa vijana ili kila kijana aliyeshiriki na ambaye hakuweza kushiriki wa leo hii na kesho ajifunze kutoka katika mafundisho yako na mafudisho ya Kanisa Katoliki la Ulimwengu wote. Mahubiri haya yanapatikana katika podcast na kusoma Makala hizi.
Asante kwa kutufuatilia: /sw/church.html