Askofu Mapunda kwa VIWAWA:Kijana ukilisikiliza Kanisa,utafanikiwa Duniani na Mbinguni
Na Angella Rwezaula -Vatican.
Askofu Edward Elias Mapunda, wa Jimbo Katoliki la Singida, na Mwenyekiti wa Idara ya Utume wa Kichungaji kwa ajili ya Walei ya Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania(TEC), wakati akiongoza Ibada ya Misa Takatifu ya kufunga Kongamano la VI Kitaifa, la Vijana Wakatoliki wafanyakazi(VIWAWA) tarehe 23 Agosti 2025, lililofanyika katika Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya nchini Tanzania akidadavua masomo yalisomwa kwa vijana: alitoa kipaumbele cha kutoa ushuhuda wa Kristo. Kutumwa na kuhubiri Injili, na kuelewa vema Mafundisho ya Kanisa. Na mengine mengi.
Katika somo la kwanza Yesu anatupatia wajibu sisi vijana, tunaohitimisha hija yetu, Kongamano letu la sita Kitaifa na viwawa. Yesu anatuambia mtakuwa mashahidi wangu, Yesu anatupatia utume sisi vijana maujaji wa matumaini, anatualika tuwe mashahidi wake. Hakika hii ni heshima kubwa, Mungu anapotualika sisi kuwa mashahidi wake. Leo tunapo hitimisha Kongamano letu Kitaifa tujiulize Je, mimi nishahidi wa Kristo? Tujiulize kila mmoja wetu ajiulize. Je, mimi ni shahidi wa Kristo? Lakini pia ninaomba umuulize jirani yako. Je, wewe nishahidi wa Kristo?... Yesu anatualika vijana kuwa mashahidi wake kwa sababu anatupenda na kutuamini. Yesu anawaamini vijana, anawapenda vijana, na ndiyo maana anawaalika muwe mashahidi. Mashahidi wa kifo chake, mashahidi wa upendo wake, mashahidi wa imani. Muwe mashahidi wa ukweli, muwe mashahidi wa haki, muwe mashahidii wa matumaini, maneno na matendo, ushuhuda wa maisha.
Ndugu zangu, Mungu anatupenda na kutuamini, akatufanya sisi binadamu kuwa mashahidi wake, kufanya ninyi vijana kuwa mashahidi wake. Ni waulize: Je, wale wanaochukuana wawili, kijana wa kiume na kijana wa kike, wanaoishi pamoja hao ni mashahidi wa Kristo? Ni akina nani hao?…. Wale ambao wakiambiwa wafunge ndoa, wanasema, nitafunga mwaka kesho, hao ni mashahidi wa Kristo? Na wakiulizwa, mwaka ule ukisha malizika, wanasema nitafunga mwaka kesho. Mwaka kesho haufiki, hao ni mashahidi wa Kristo? ni mashahidi wa nani?... Je, Wale wanaotoa na kupokea rushwa ni mashahidi wa Kristo? Ni mashahidi wa nani?... Je, wale wanaotoa mimba ni mashahidi wa kristo?... Ni mashahidi wa nani?- (jibu ni shetani)... Wakitoa mimba watarudisha lini?... Ukitoa kiti ndani, ukikitoa nje, unaweza kurudisha.., Je, mimba utawaza kurudisha?... Je, wale vijana ambao hawataki kufanya kazi, ni mashahidi wa Kristo?... Kwa hiyo, tunafahamu nani ni shahidi wa Kristo, si ndiyo?... Sasa tunawaalika ambao mnasema ni mashahidi wa ‘shetani,’ wabadilike na wawe mashahidi wa kristo.
Tuwaombee, kuwa shahidi wa Kristo ni kujitahidi kuishi maisha matakatifu, ni kujitahidi kuishi maisha ya upendo, ni kujitahidi kushika amri za mungu, kujitahidi kuishi mapendo na kujitahidi kuishi amri za Mungu, Kuishi maisha ya haki, kuishi maisha ya amani. Ndugu zangu, leo tunaalikwa tukawe mashahidi kama tulivyo sikia katika somo hili: “Mtakuwa mashahidi wangu” na ni agizo! Twendeni tukawe mashahidi wa Kristo. Tuwe mashahidi pia wa ukweli, kuongea ukweli. Yule anayeongea uongo ni shahidi wa Kristo?... Mtu mmoja alisema aheri usulibishwe kwa ajili ya kusema ukweli, kuliko kusulibisha ukweli. Wanao wapa wenzao ujauzito na kukataa…., ni mashahidi wa Kristo hao? Ni mashahidi wanani…?(shetani). Wale wanaozaa watoto na kuwatupa kwenye majalala….! Yeyote anayekataa uhai, siyo shahidi wa Kristo. Yeyote anayekataa uhai, anayekataa zawadi kutoka kwa Mungu, huyo siyo shahidi wa Kristo. Kwa hiyo tunaalikwa kuwa mashahidi, tunaalikwa kuishi imani yetu.
Somo na Pili, Mtakatifu Paulo, Mtume wa Mataifa, anatualika sisi vijana kuhubiri Injili, kuhubiri njili ni wajibu wa kila mbatizwa, tena Paulo anatumia lugha kali kidogo, anasema “Ole wangu nisipo hubiri.” Na wewe sema: ‘ole wangu nisipo hubiri Injili,’… Mwambie mwanzako ‘Ole wako usipo hubiri njili,” hiyo ni laana hiyo. Umebatizwa, unatumwa, kuhubiri Injili. Mjitahidi kuhubiri Injili wakati bado mna nguvu.
Kuyaelewa Mafundisho ya Kanisa
Lakini pia nawaalika vijana leo tunapo hitimisha Kongamano letu kwamba vijana mjitahidi sana kuyaelewa mafundisho ya Kanisa. Vijana, ninarudia tena, mjitahidi sana kuyaelewa, kuyafahamu mafundisho ya Kanisa. Hata mafundisho msingi ya Kanisa, lazima kujua Kanisa linafundisha nini? Lazima mfanye bidi ya kuyafahamu mafundisho msingi ya Kanisa. Lazima kijana ufahamu Kanisa linafundisha nini, kwa mfano, kuhusu Bikira Maria Mama wa Mungu. Lazima ufahamu Kanisa linafundisha nini kuhusu Mama Maria, Mama wa wote. Mama Maria...! lazima kijana mfahamu Kanisa linafundisha nini kuhusu Sakramenti mbalimbali katika Kanisa, Kanisa linasema nini kuhusu Ubatizo. Kanisa ni linasema nini kuhusu Ekaristi Takatifu? Kanisa ni linasema nini kuhusu Sakramenti ya Kipaimara? Kanisa ni linasema nini kuhusu Sakramenti ya Kitubio? Kanisa linasema nini kuhusu Mpako wa wagonjwa? Lazima uyafahamu Mafundisho ya Kanisa. Msipo yafahamu Mafundisho ya Kanisa, mtayumba yumba na mtatanga tanga, mnanielewa?
Msipofahamu vizuri Mafundisho ya Kanisa, mtatanga tanga, kama wengine wanavyo tanga tanga, leo wapo hapa, kesho wapo pale, mpaka viatu vimeisha, wanatembea tembea huko na huko kutangatanga. Kwa sababu hawana mizizi. Ni mti wenye mizizi tu ndiyo unaweza kustahimili upepo. Ni mti wenye mizizi imara. Ndiyo huo unaweza kupambana na upepo, lakini usiyo kuwa na mizizi unafanyaaje? Unaanguka si ndiyo?... Sasa mizizi ni kufahamu mafundisho ya Kanisa vizuri, fahamuni mafundisho ya Kanisa vizuri. Kanisa lina sema nini? Kuhusu Sakramenti, hasa Sakramenti mbalimbali, ndiyo maana watu wanaingia kwenye ndoa kwa mfano bila kujua Sakramenti ya ndoa nini? Si ndiyo?...
Kwa sababu mwingine anakwenda kuoa kwa sababu jirani yake, kuolewa kwa sababu ya jirani yake kaoa, au kwa sababu ya presha ya wazazi na mambo mengine, lakini hajui ndoa ni nini; ndoa ya kikristo, ndoa katika Kanisa Katoliki. Ni lazima tufahamu, lazima kuwa na bidii. Roho Mtakatifu anawashukia Mitume tumwombe Mungu atujalie kuwa na bidii, tuwe na bidii katika dini. Na bidii katika dini ni pamoja na kufahamu Mafundisho msingi ya Kanisa letu, huwezi kuhubiri Injili bila kujua mafundisho, utahubirije, utapelekaje ujumbe, wakati hujui Mafundisho ya Kanisa. Utaweza kuwambia watu kuna Sakramenti ya Ubatizo wakati wewe hujui Ubatizo, au Ekaristi Takatifu, wewe mwenye hujui Ekarista Takatifu ni nini…! Lakini pia vijana naomba mjitahidi kununua vitabu mbali mbali. Kuna vitabu vingi vimeandikwa kuhusu Sakramenti mbali mbali na Mafundisho mbali mbali katika Kanisa. Mnunue vitabu hivyo, viwasaidie. Someni vitabu. Vitawasaidia sana!
Kusikiliza Kanisa Katoliki ambalo ni Mama na Mwalimu
Lakini pia nawaomba vijana, mlisikilize Kanisa Katoliki, Kanisa Katoliki ni Mama na Mwalimu. Sema Kanisa Katoliki ni Mama na Mwalimu wa imani…. Kwa hiyo mlisikilize Kanisa. Ukipata changamoto fulani katika maisha ujiulize Kanisa linasema nini kuhusu jambo hili? Kanisa linataka nifanye nini? Kanisa ni linasema nifanye nini? Katika jambo hili, katika tukio hili, Kanisa ni linaniambia nini? Kama Mama na Mwalimu. Hao walimu wengine bandia, wanaweza kukupeleka mahali, alafu usitoke huko. Kwa hiyo, msikilize Mama Kanisa, linasema nini? Ukilisikiliza Kanisa, utafanikiwa duniani na Mbinguni. Ukilisikiliza Kanisa Katoliki, utafanikiwa na maisha yatakunyokea duniani na Mbinguni. Kwa sasa, sio watu wa kwanza, watu wengi wamenyokewa kwa sababu ya kulisikiliza Kanisa. Vijana kadhaa wameharibikiwa kwa sababu ya kutolisikiliza Kanisa; kusikiliza pembeni pembeni watu flani flani, ambao wamewapotosha na kuwaangusha maisha yao yote. Lisikilize Kanisa, wewe kijana, wewe kiwawa.