Askofu Nyaisonga,VIWAWA:Vijana muwe na hekima kama Bernardo na msitumike kufanya uovu
Na Angella Rwezaula –Vatican na Sarah Pelaji, Dar Es Salaam.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Mbeya, Mhashamu Gervas Nyaisonga, katika Ufunguzi wa Kongamano la VI la Kitaifa la Vijana Wakatoliki Wafanyakazi(VIWAWA), linalofanyika huko Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mbeya (CUoM) nchini Tanzania kuanzia tarehe 20 hadi 24 Agosti 2025 aliongoza ibada ya Misa Takatifu ya tarehe 20 Agosti 2025 katika ufunguzi wa Kongamano hilo linalowaona vijana zaidi ya 4,200 kama wawakilisha wa vijana wote kutoka Majimbo Katoliki ya Tanzania pia waamini waliowaunga mkono kutoka Jimbo Kuu Katoliki la Mbeya. Mama Kanisa akiwa anaadhimisha kumbukizi ya Mtakatifu Bernardo- wa Clairvaux kila 20 Agosti Askofu Mkuu alipata fursa ya kuelezea historia ya sifa ya Mwalimu huyo wa Kanisa ili kuwafikia vijana maisha yao ya kila siku kwa kila ngazi: familia, kazi, shule, na kijamii kwa ujumla. Akianza aliwalekea wanajimbo Kuu wote wa Mbeya na kuwakaribisha katika kongamano hilo. Radio Vatican inayo furaha ya kukuletea mahubiri haya muhimu kwa vijana wote walioudhuria na wengine kufutatilia katika mitandao au ambao hawakuweza kuwa na fura hiyo.
Makaribisho na sura ya Mtakatifu Bernardo
Kwaya ya wanajimbo kuu la Mbeya. Tunawakaribisheni nyote Mbeya, kwenye Kongamano hili la sita la Viwawa. Tuna furahi kuwa na ugeni mkubwa hivi. Maskofu, Mapadre watawa, vijana, wazee, watoto, wote viongozi wa Kanisa na wa kijamii. Wote mnaonekana mmetambua thamani ya Kongamano hili. Karibuni mjisikie mahali pazuri. Ndugu zangu wapendwa, leo katika kalenda ya Kanisa ni Siku kuu ya Mtakatifu Bernardo. Tunamuita Bernardo wa Clairvaux huko Ufaransa ndiyo alipoishi. Mwishoni mwa karne ya XI, kuanzia 1160 -1153. Huyu Bernardo alipoishi, alipitia hatua za malezi na makuzi kama sisi sote tunavyopitia au tulivyopitia. Hata hivyo maisha yake yana mambo mengi ya kukumbuka. Na nimependa tuzingatie kidogo juu ya Mtakatifu huyu, kwani naona anayo mengi ya kutusaidia, hasa ya kuwasaidia ninyi vijana. Katika mengi aliyokuwa nayo nimechagua machache “manne” ambayo yanaweza kutuangaza katika tafakari zetu.
Jambo la kwanza Bernardo: kujiuliza maswali
Tunaambiwa Bernardo alipokuwa akiishi hakuacha kujiuliza maswali. Na swali moja alilopenda kujiuliza mara nyingi lilikuwa hili: “Bernardo Bernardo, umekuja kufanya nini hapa?” Alizoea kujiuliza swali hili, na alikuwa anajiita jina lake , na kujiuliza swali. Ninaamini alikuwa anajiuliza akiwa mahali ambapo palikuwa panampatia mashaka, hata mahali ambapo alikuwa na uhakika, hapo hakuacha kujifanyia tathmini. Ninaamini alijiuliza mbele ya kinywaji, mbele ya chakula, kwenye mikutano, kwenye sherehe na shughuli nyingine ambazo alishiriki kibinadamu. Swali hili lilimjia mara, kuwa umekuja kufanya nini hapa.? Na alipojitahidi kulijibu kwa dhati, alijikuta amepata nguvu ya kushinda maelekeo mabaya. Ninaweza kusema kwa swali hili alikuwa anajiubiria yeye mwenyewe. Bernardo alizoea kujiubiria.
Jambo la pili katika maisha yake: mlinzi shujaa wa maisha yake
Alikuwa mlinzi shujaa wa Kanisa, akikazia mafundisho ya kweli na akiwa mkali alipoona kwamba mambo hayapelekwi itakiwavyo kwani, aliweza hata kumkabili Papa mmoja ambaye aliamua kuishi Ufaransa badala ya Vatican. Na alimwambia kwa ukali akimkubusha mfumo wa Kanisa ambao Bwana Yesu mwenyewe aliuacha. Hapo Bernardo alikuwa anawahubiria wengine. Pamoja na kujihubiria yeye mwenyewe, lakini hakustahimili maelekeo mabaya ya wengine. Na hata walimpatia jina la kupanga, walimwita dhamiri ya karne yake. Dhamiri ni sauti ambayo Mungu ameweka ndani ya moyo wa mtu, inayomwambia ukweli. Ukifanya jambo mbaya, unaanza kupata hisia kwamba umekosea hata kabla ujakamatwa. Hiyo ndiyo dhamiri. Ukifanya jema pia itakupongeza. Yeye sasa aliitwa dhamiri ya karne yake. Tunaona hakuacha kamwe kuihamsha dhamiri yake mwenyewe kwa kujiubiria na hakuacha kamwe kuhamsha dhamiri za wengine walio kuwa na maelekeo mabaya. Hilo ni dhahiri katika maisha yake. Na hakuishia hapo.
Jambo la tatu: alipenda kusali na alimpenda Mama Bikira Maria
Bernardo alipenda kusali na alimpenda sana Mama Bikira Maria, alimuona ni Mama yake. Na aliweka ibada nzuri sana na kutunga sala na nyimbo nzuri zinazomsifia Mama Bikira Maria. Na mkitaka kuliamini hili mnaoifahamu ile sala ya kumbuka (memorare). Yaani sala ile ilitungwa na yeye ambamo katika sala anasema: “Haijasitirika kamwe, Mama Maria umewahi kumuacha mtu aliyekimbia ulinzi wako…”. Kwa sala ile inatosha kusema, “alikuwa na imani thabiti juu ya Mama Bikira Maria, neema alizopewa na alivyo msaada kwa Wakristo.” Huyo ni Bernardo. Katika ulimwengu wa Kiroho alifanya vizuri na anakumbukwa tangu karne ya kumi na moja mpaka leo hii. Bado karne na karne, Bernardo anabaki kuwa ni nuru inayoangaza katika maisha ya kiroho.
Jambo la nne na la mwisho.
Bernardo alikuwa mwalimu mzuri wa elimu ya Mungu. Mwalimu mzuri ambaye alijua haitoshi tu kusikia lakini yafaa kufundisha kwa kina yanayohusu Mungu ili watu wapate uongofu kikamilifu. Aliandika na kutoa mihadhara na kufundisha kwa kina na kwa majitoleo makubwa. Tunaambiwa alizunguka sehemu mbalimbali uko bara la Ulaya, huku akifundisha masuala ya imani, na masuala ya Mungu. Kwahiyo Bernardo alijaribu kuyavingilisha maisha yake na shughuli hizo kuu nne.
Kuiweka hai dhamiri yake mwenyewe, kuziweka hai dhamiri za wengine, kuweka hai mahusiano yake ya kiroho kwa sala akipitisha sala zake na maombi yake kwa Mama Bikira Maria, ambaye ni kikao cha hekima,na ambaye ni msaada wa daima. Na vile vile aliendelea kujifunza ili kuwafundisha wengine kupata elimu ya kutosha na uelewa wa kutosha juu ya Mungu. Kwa ufupi tuseme Bernardo alijaliwa paji kubwa la elimu, alijaliwa paji kubwa la hekima, alijaliwa paji kubwa la ufahamu. Bernardo alijaliwa hayo na anaweza kutajwa katika karne yake kuwa ni mmoja wa watu waliokuwa na hekima. Ni Shauku yetu Baraza la Maaskofu, ni shauku yetu vijana wote, muwe na paji hilo la hekima. Ni tamaa yetu muwe kama Bernardo. Ni tamaa yetu mfanane na yeye. Katika muktadha huo ningependa mzingatie mawaidha yafuatayo.
Kwanza, itafuteni hekima.
Itafutenie hekima kama Bernardo na ninyi muwe na dhamiri hai. Usichelewe kutambua kwamba hili ni jema na hili ni baya. Daima ujiulize uko wapi? Unafanya nini? Uko na nani? Unafanya nini? Na yeye uliye naye alikuwa wapi kabla hamjakutana? Na mtakuwa naye mpaka lini? Mjaliwe paji la Hekima kujiuliza uko wapi? Umetoka wapi? Unakwenda wapi? Hizo ndizo dalili na ishara kwamba nawe unapitia katika njia ya hekima. Unalifuatilia paji la hekima na unataka liwe sehemu ya utambulisho wako. Mfanane na Bernardo, kutonyamazia mwelekeo mbaya wa wenzenu, msinyamazie mwelekeo mbaya. Na ninyi muwe dhamiri ya wengine, mkisha lea dhamiri zenu, kazi haijaisha, bali mlee pia dhamiri za wengine. Na kulea dhamiri ya mwingine inahitaji ujasiri wa kusema hili si sawa. Hili ni kosa. Halipaswi kufanyika hivi. Linapaswa kufanyika vile, ili furaha tulioambiwa na Mungu iwe haki ya kila mtu. Nyinyi vijana, mnayo nafasi hiyo kubwa kwa kundi tu hili. Na hili ni tone la vijana tu wa Tanzania. Lakini kwa kundi hili, Mbeya kumetikisika! Kwa hiyo mlee dhamiri. Mlee dhamiri zenu na msiache kulea dhamiri za wengine. Sasa hivi mna haki zote, kama ni kupiga kura, mnayo haki, kama ni kupigana uhakika wa kushinda mnao. Kama ni mbio, uhakika wa kuwa wa kwanza mnao, Sawa? Kama tutashindana kuzaa watoto, nyinyi kwa vyovyote mnawezo kuzaa wengi zaidi.
Kipindi cha pili cha mahubiri: miito kwa vijana
Katika sehemu ya pili ya mahubiri yake, Askofu Mkuu Nyaisonga aligeukia muktadha mwingine kwa kutoa miito kadhaa na maonyo kwa vijana wa Kitanzania hasa kutokubali kutumiwa kutekeleza vitendo vya utekaji, mauaji na utesaji, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025. Alitoa mfano wa vijana wa Boada boda, au bajaji wanaojihusisha na madawa ya kulevya. Askofu Nyaisonga alisisitiza kuwa hakuna mtu aliye na haki ya kuondoa uhai wa mwingine. “Tunasikitishwa na mauaji ya wenye hatia, lakini sasa hali imekuwa mbaya zaidi, hata wasiokuwa na hatia wanauwawa. Mara nyingi si wazee wanaotekeleza uovu huu bali vijana wanaotii amri haramu. Msitii amri hizo. Utii wa namna hiyo ni utii kipofu.” Askofu Mkuu huyo alieleza kuwa vitendo hivyo huendeshwa na baadhi ya vijana waliokosa msimamo wa kiadili, akisisitiza kuwa vijana wanapaswa kujitambua na kuishi maisha ya hekima. Wengine wanafanya maovu kwa sababu tu ya ujinga, hawajapata fursa ya kusikia na kutafakari vya kutosha. Ombeni kwa busara. Kama Sulemani alivyoomba hekima na akapewa yote, nanyi ombeni kile kilicho sahihi.
Wito dhidi ya rushwa na uvivu kuelekea uchaguzi
Katika kuelekea uchaguzi mkuu, Askofu Mkuu Nyaisonga aliwakumbusha vijana kutojihusisha na rushwa, utapeli, wizi na ubaguzi wa aina yoyote. Alisema kuwa vitendo hivyvinachochewa na watu wenye maslahi binafsi wanaowatumia vijana kama vyombo vya kutekeleza uovu. “Kutakuwa na rushwa, utapeli na ushawishi wa kufanya maovu. Mara nyingi vijana ndiyo wanaotumwa kupeleka hongo. Msikubali kushiriki katika vitendo hivyo vinavyovuruga misingi ya haki na demokrasia,” aliongeza.
Maadili na siri za maisha marefu
Askofu Mkuu Nyaisonga aliwataka vijana kuelewa kuwa maisha ni zawadi kutoka kwa Mungu na yanapaswa kutumika kwa kumtukuza Muumba. Alibainisha kuwa maisha marefu yanapatikana kwa kuishi kwa kuzingatia maagizo ya Mungu. Akitoa mifano hai, alielezea jinsi vijana wengi, kama waendesha bodaboda, wanavyopoteza maisha kwa sababu ya kutofuata sheria za usalama barabarani, na wengine kujihusisha na biashara haramu za dawa za kulevya au ngono za kibiashara. “Tusishiriki au kushabikia ushoga, usagaji au vitendo vyovyote vinavyopingana na mpango wa Mungu. Haya ni mmomonyoko wa maadili unaowaumiza familia na jamii,” alisema kwa msisitizo.
VIWAWA 2025:Wito wa kumcha Mungu
Katika Kongamano hilo la VIWAWA, ambalo linawakutanisha vijana kutoka majimbo yote ya Kanisa Katoliki Tanzania, Askofu Mkuu Nyaisonga alihitimisha kwa kusisitiza kuwa vijana wasiegemee hekima ya dunia bali wategemee hekima ya Kimungu yenye nguvu ya kuokoa. “Msipanie mambo yasiyo na maana. Msikie neno la Mungu, mlipokee, mzae matunda mema. Fursa ni nyingi, kwanini neno la Mungu halikai ndani? Jibuni wito wa Mungu kwa maisha ya hekima na utakatifu,” alihimiza. Kongamano hilo la VIWAWA Kitaifa linatarajiwa kufikia kilele chake tarehe 23 Agosti 2025, huku likiwa limelenga kuwajengea vijana msingi wa kiroho, maadili na uzalendo katika mazingira ya sasa ya kijamii na kisiasa.