Chimbindi,SADC:umoja na mshikamano ni silaha ya mtangamano imara wa SADC
Vatican News
Katika Kikao cha Maafisa Waandamizi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC) ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Biashara za Kimataifa wa Zimbabwe, Balozi Albert Chimbindi wakati wa kusoma hotuba ya ufunguzi ya kikao chao jijini Antananarivo tarere 6 Agosti 2025, alisema kuwa: "Umoja na mshikamano imeelezwa kuwa ni silaha pekee ya Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika(SADC), wa kuimarisha mtangamano imara na wenye nguvu, utakaowezesha kufikia malengo yaliyowekwa na jumuiya hiyo.
Kikao cha maafisa waandamizi ni moja ya vikao vya utangulizi kuelekea Kikao cha Baraza la Mawaziri kunako tarehe 12 Agosti 2025 na baadaye Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) itafanya Mkutano wa 45 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali katika Kituo cha Mikutano cha Ivato mjini Antananarivo, nchini Madagascar tarehe 17 Agosti 2025. Huu ni wakati wa kihistoria kwa Madagascar, ambayo ilikua Nchi Mwanachama wa SADC mnamo Agosti 2005. Ukiwa umeandaliwa chini ya kaulimbiu: "Kuendeleza Uendelezaji wa Viwanda, Mabadiliko ya Kilimo, na Mpito wa Nishati kwa SADC Imara," Mkutano huo utajikita katika kuharakisha utangamano wa kikanda kupitia nguzo muhimu: kuimarisha uwezo wa viwanda na mnyororo wa thamani wa kikanda, kufanya kilimo kiwe cha kisasa, na kukuza mpito wa nishati jumuishi, yote yakilenga kujenga kanda ya SADC yenye uthabiti, endelevu na yenye mshikamano.
Wakati wa Mkutano huo, Mheshimiwa Andry Rajoelina, Rais wa Jamhuri ya Madagascar, atashika rasmi Uenyekiti wa SADC, akimrithi Mheshimiwa Dk. Emmerson Dambudzo Mnangagwa, Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe. Kwa njia hiyo Mkutano huo utapitia maendeleo ya utekelezaji wa Mpango Elekezi wa Maendeleo ya Kikanda wa SADC (RISDP) 2020–2030, ukizingatia ripoti ya Mwenyekiti wa Chombo cha Ushirikiano wa Siasa, Ulinzi na Usalama, na kupitia mafanikio chini ya kaulimbiu ya Mkutano wa 44: "Kukuza Ubunifu wa Kufungua Fursa za Ukuaji Endelevu wa Uchumi na Maendeleo kuelekea SADC yenye Viwanda."
Kwa mujibu wa taarifa ya maadalizi inabainisha kwamba “kama chombo kikuu cha kutunga sera cha SADC, Mkutano huo unaweka vipaumbele vya kimkakati kwa ushirikiano wa kikanda, utangamano na maendeleo. Sherehe za Ufunguzi na Kufungwa kwa Mkutano huo zitaoneshwa moja kwa moja tarehe 17 Agosti 2025 kwenye majukwaa rasmi ya Jamhuri ya Madagascar na Sekretarieti ya SADC, ikijumuisha ukurasa wa Facebook wa SADC na chaneli ya YouTube.
Kwa njia hiyo katika kikao hicho cha Utangulizi wa Mkutano wa viongozi wakuu, kiliwaona hata ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Amina Khamis Shaaban ilishuhudiwa Zimbabwe kupitia Balozi Chimbindi akikabidhi uenyekiti wa kikao hicho kwa Madagascar ambapo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, Bwana Eric S. Ratsimbazafy alipokea na kuahidi kuendeleza yale yote mazuri yaliyoanzishwa na mtangulizi wake.
Kwa upande wa Balozi Chimbindi alisema kuwa katika kipindi cha uenyekiti wake, mtangamano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) umeendelea kuimarika na mafanikio makubwa yamepatikana katika nyanja za ulinzi na usalama, utawala bora, maendeleo ya rasilimali watu, viwanda na huduma za jamii. Hata hivyo aliongeza kusema kuwa licha ya Kanda ya SADC kukumbwa na changamoto mbalimbali kama vile, ugonjwa wa UVIKO-19, ukame, maradhi, mabadiliko ya siasa za kimataifa na mabadiliko ya tabianchi, bado eneo hilo limeendelea kuwa imara kiuchumi.
Balozi Chimbindi alitoa wito kwa nchi wanachama kuongeza jitihada za pamoja kujenga miundombinu ya barabara, reli, nishati na maji ili kuchochea shughuli za kiuchumi na biashara katika kanda. "Kanda yetu imebarikiwa kuwa na vijana wengi pamoja na maliasili za kutosha, hivyo ni jukumu letu kuzitumia ipasavyo kwa ajili ya kukuza uchumi na kuondoa tatizo la ajira kwa vijana", Balozi Chimbindi alisema.
Bohari Kuu ya Dawa ya Madagascar (MSD) watembelea na Taasisi mwenzia ya Madagascar
Watendaji wa Bohari Kuu ya Dawa (MSD) wakiongozwa na Meneja wa Masoko ya Kikanda, Bi. Nabila Hemed walitembelea Bohari Kuu ya Dawa ya Madagascar (SALAMA) na kuzungumza na uongozi wa bohari hiyo, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Bwana Claude Eric Ramanantoanina kuhusu njia bora za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi hizo muhimu kwa afya ya binadamu. Mazungumzo hayo yaliyofanyika Antananarivo tarehe 8 Agosti 2025, kando ya maandalizi ya Mkutano wa 45 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa kuakisi masuala masuala mbalimbali, ikiwemo namna bora ya kutumia mpango wa pamoja wa nchi za SADC wa kununua dawa, vifaa tiba na vitendanishi ambapo Tanzania kupitia Bohari Kuu ya dawa (MSD) ikukabidhiwa jukumu hilo kwa niaba ya nchi za SADC.
Bi. Nabila ambaye aliwasilisha mada kuhusu uwezo na ufanisi wa MSD alisema: “Ni muhimu nchi za SADC ikiwemo Madagascar zikautumia mpango huo ipasavyo, kwani pamoja na mambo mengine, unalenga kuzisaidia nchi wanachama kupata bidhaa bora za afya kwa gharama nafuu na kuhamasisha uzalishaji wa ndani wa bidhaa hizo ili Kanda ya SADC iweze kujitegemea.” Viongozi hao pia walijadiliana kwa kina kuhusu: “umuhimu wa kubadilishana uzoefu katika utekelezaji wa majukumu yao hususan katika maeneo ya uzalishaji, uhifadhi na usambazaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi.”
Katika maelezo yao walisemakuwa hayo “ni maeneo nyeti yanayohitaji ufanisi na ubunifu ili kuepuka changamoto ambazo zinaweza kuzorotesha mfumo wa utoaji wa huduma za afya katika nchi.” Hivyo, walisisitiza umuhimu wa nchi za SADC kupitia taasisi zilizokasimiwa kutekeleza majukumu hayo, kubadilishana uzoefu na taarifa ili ziweze kujikwamua. Viongozi hao walihitimisha mazungumzo yao kwa MSD kuualika uongozi wa Bohari Kuu ya Dawa ya Madagascar (SALAMA) kutembelea Tanzania ili kupanua wigo wa majadiliano na kujifunza zaidi. Mazungumzo hayo pia yalihudhuriwa na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kasiga na Afisa Sheria Mkuu wa MSD, Bi. Ukundi Domenic.