Marekani Inaadhimisha Kumbukizi ya Miaka 249 ya Uhuru Wake
Na Sarah Pelaji, -Vatican
Ijumaa tarehe 4 Julai 2025, Rais wa Jamhuri ya Italia, Sergio Mattarella, amemtumia Rais wa Marekani, Donald J. Trump, ujumbe maalumu katika Maadhimisho ya Miaka 249 Uhuru wa Marekani akieleza kuridhishwa na umoja na mshikamano kati ya nchi hizo mbili na kukiri kuwa, Marekani imekuwa mshirika wa kipekee kwa Italia hasa katika mchakato wa kujenga amani na usalama duniani. Salamu hizo za pongezi amezituma kutoka kwa Jamhuri ya Italia na kwake binafsi akimpongeza Rais wa Marekani Trump na watu wa Marekani, akieleza kuwa, misingi imara ya uhusiano wa pande hizi mbili na ukaribu wa kipekee wa mazungumzo ya kisiasa ni kielelezo cha uhusiano wa karibu na wa kweli uliopo baina ya Mataifa hayo mawili.
Ushirikiano wa kiuchumi, kitamaduni na kijamii unaochangiwa kwa kiwango kikubwa na Jumuiya hai ya Wamarekani wenye asili ya Italia unaleta mchango mkubwa katika ushirikiano wa kihistoria wanaodhamiria kuuendeleza kwa misingi ya usawa, ustawi na maendeleo ya wengi. Katika hali ya sasa ya kimataifa iliyojaa changamoto nyingi na ngumu hasa hali mbaya ya kivita inayoendelea nchini Ukraine na huko Mashariki ya Kati ambapo nchi ya Marekani na Italia zinashirikiana katika kujenga usalama wa Kimataifa kwa lengo la kuleta uthabiti na amani ambazo leo zimeathirika sana.
Katika muktadha huu mgumu wa mivutano baina ya Mataifa nchi hizo mbili zinaona umuhimu wa kufanya juhudi za pamoja na endelevu ili kujenga mshikamano wa nchi za pande zote za Bahari ya Atlantiki ili zibaki kuwa msingi mkuu wa kukabiliana na changamoto hizo kisha kuleta mafanikio ya amani na usalama duniani. “Katika siku hii muhimu ya maadhimisho ya Uhuru wa Marekani, napenda kukutakia tena mafanikio mema binafsi na ustawi kwa raia wote wa Marekani," amesema Rais Mattarella.