MAP

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 7 Julai inaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 7 Julai inaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani   (Tanzania State House)

Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani 2025: Kiswahili Kwa Amani na Mshikamano

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 7 Julai inaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa Lugha ya Kiswahili katika kuimarisha mawasiliano, utamaduni na mshikamano wa kijamii. Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani mwaka huu kitaifa nchini Tanzania yamefanyika Kisiwani Zanzibar yakiongozwa na kauli mbiu “Kiswahili kwa Amani na Mshikamano’. Kiswahili ni lugha inayozungumzwa na watu wengi duniani.

 Sarah Pelaji, Vatican.

Lugha ni chombo muhimu sana cha mawasiliano kilichoundwa na sauti za nasibu za kusemwa na kutumiwa na jamii ya utamaduni fulani. Jinsi ambavyo zipo jamii nyingi za tamaduni mbalimbali duniani, vivyo hivyo ziko lugha mbalimbali zilizoundwa kukidhi haja ya mawasiliano ya tamaduni mbalimbali. Maingiliano ya jamii zenye tamaduni na lugha mbalimbali yanayotokana na mashirikiano katika shughuli za biashara na nyinginezo za kijamii, huzusha haja ya kuwepo kwa lugha moja itakayoweza kuwaungaanisha watu hao wenye tamaduni na lugha mbalimbali. Maingiliano kama hayo yanaweza kuwa katika viwango mbalimbali. Kiwango cha kwanza ni kile cha mtu binafsi ambapo mtu hutoka kwenye jamii yake na kwenda kuishi kwenye jamii inayozungumza lugha tofauti na ile ya kwao. Katika hali kama hiyo, mtu huyo itabidi ajifunze lugha ya jamii ile ya pili ili aweze kuwasiliana nao. Kiwango cha pili ni kile kinachohusisha mkusanyiko wa watu waliotoka kwenye tamaduni mbalimbali na hawana hata lugha moja ya kuwaunganisha. Watu kama hawa wakikaa pamoja huweza kuzusha lugha ya kati ambayo katika hatua za mwanzo zijulikanazo kama Pijini na baadaye kama Krioli. Kiwango cha tatu ni kile ambacho maingiliano ya watu wenye tamaduni na lugha mbalimbali husababisha kuteuliwa kwa lugha moja miongoni mwa lugha zao na kutumika kama chombo cha mawasiliano na cha kuziunganisha jamii zote husika. Kiwango hiki chaweza kujitokeza katika ngazi ya wilaya, mkoa, nchi, kanda, bara na hata ulimwengu mzima.

Maadhimisho ya Siku ya IV ya Kiswahili Duniani 2025
Maadhimisho ya Siku ya IV ya Kiswahili Duniani 2025   (Tanzania State House)

Ni katika muktadha huu, Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO katika mkutano wake wa 41 uliofanyika mjini Paris, Ufaransa, tarehe 23 Novemba 2021 uliamua kwamba, tarehe 7 Julai ya kila mwaka itakuwa ni Siku ya Kiswahili Duniani. Azimio hili lilipitishwa na wanachama wote wa UNESCO bila kupingwa. Waswahili kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wakafurahia sana tamko hili, kwa Umoja wa Mataifa kuamua kutoa kipaumbele cha pekee kwa Lugha ya Kiswahili. Hii ni lugha ya kwanza ya mawasiliano kutoka Barani Afrika kutambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa na kutengewa siku maalum ya kuadhimishwa Kimataifa. Kiswahili kinatambulikana kuwa ni lugha rasmi kwenye Umoja wa Afrika, Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na Bunge la Afrika. Lakini, ikumbukwe kwamba, Kiswahili ni kati ya lugha zinazozungumzwa na watu wengi duniani. Kumbe, kila mwaka Julai 7, dunia inaadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani kwa lengo la kutambua na kuenzi mchango wa Lugha ya Kiswahili katika kuimarisha mawasiliano, utamaduni na mshikamano wa kijamii. Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani mwaka huu kitaifa nchini Tanzania yamefanyika Kisiwani Zanzibar yakiongozwa na kauli mbiu “Kiswahili kwa Amani na Mshikamano’ huku Mgeni rasmi akiwa ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah ambaye amemwakikisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi. Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka pande zote mbili za Muungano, akiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Palamagamba Aidan Kabudi, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Gerson Msigwa pamoja na viongozi wengine kutoka Zanzibar na Tanzania Bara.

Maadhimisho ya Siku ya IV ya Kiswahili: Maonesho ya bidhaa mbalimbali
Maadhimisho ya Siku ya IV ya Kiswahili: Maonesho ya bidhaa mbalimbali   (Tanzania State House)

Katika hotuba yake, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdallah, ametoa wito kwa taasisi na idara mbalimbali za Serikali kuhakikisha zinazingatia matumizi sanifu na fasaha ya lugha ya Kiswahili katika shughuli zao za kila siku. Amesisitiza kuwa Kiswahili ni lugha adhimu inayotambulika kimataifa, hivyo ni wajibu wa kila Taasisi ya Serikali kuhakikisha kuwa matumizi ya lugha hiyo yanazingatia kanuni, miiko na matumizi sahihi. Aliweka mkazo kuwa lugha ya Kiswahili si tu chombo cha mawasiliano, bali pia ni sehemu ya utambulisho wa taifa na urithi wa utamaduni wa Watanzania. Amelihakikishia taifa kuwa, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kuhimiza matumizi ya Kiswahili katika nyanja zote, ikiwa ni pamoja na elimu, utawala na huduma za kijamii. Kwa upande wake, Waziri wa maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto Zanzibar mhe. Riziki Pembe Juma amewaomba Watanzania kutumia vizuri lugha ya kiswahili kama nyenzo ya kulinda amani nchini na kuleta maendeleo nchini kwani lugha ni chanzo cha kuboresha na kuleta maendeleo kwenye sekta mbalimbali nchini ikiwemo sekta ya afya “amani ndiyo kila kitu, amani ndiyo msingi wa maisha yetu, Amani ndiyo kichocheo cha maendeleeo ya taifa kwenye nchi yetu, ukiwa na amani utaishi vyema lakini kama hatuna amani hatuwezi kufanya chochote, hapatakuwa na maendeleo, kwenye jambo lolote sio kwenye afya miundombinu au jambo lolote.”

Kauli mbiu: Kiswahili kwa amani na mshikamano
Kauli mbiu: Kiswahili kwa amani na mshikamano   (Tanzania State House)

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) Bi Consolata Mushi, Amewaasa vijana kutoharibu Kiswahili kwa kudondosha au kuongeza irabu kwenye maneno wanapozungumza ili kulinda misingi na thamani ya lugha ya Kiswahili. Ameeleza kuwa, Lugha ya kiswahili imekuwa na mchango mkubwa katika kurahisisha mawasiliano katika Sekta ya Afya ikiwemo wagonjwa na wataalam wa Afya pamoja utoaji wa Elimu ya Afya kwa wananchi. Katika maadhimisho hayo Mhadhiri, mshtiti na mchambuzi wa Lugha ya Kiswahili kutoka Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Dkt. Ahmad Sovu, ametunukiwa tuzo ya uendelezaji wa Kiswahili kupitia ufundishaji na uchapishaji wa makala. Tuzo hiyo imetolewa kwa ushirikiano wa Baraza la Kiswahili la Zanzibar (BAKIZA) na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), na imekabidhiwa kwake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdallah. Dkt. Sovu ni mshtiti na mchambuzi mahiri wa Kiswahili ambaye, mbali na ufundishaji na kuandika makala nyingi, amekuwa mstari wa mbele katika kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili ndani na nje ya Tanzania. Tangu mwaka 2021 ilipotangazwa rasmi na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), tukio hili limeendelea kuhamasisha matumizi ya Kiswahili katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, biashara, diplomasia na sanaa, huku wadau wakihimiza juhudi za kukiendeleza na kukilinda dhidi ya kupotea au kudharaulika. Lugha ya Kiswahili, inayozungumzwa na mamilioni ya watu kote Afrika na duniani, imebaki kuwa nyenzo muhimu ya kuleta umoja na kukuza lugha ya Kiswahili. Tayari Mataifa mbalimbali yamewekeza katika lugha ya Kiswahili katika kuboresha Elimu na hata kudumisha umoja baina ya mataifa, ni vyema kusema lugha ya Kiswahili imehimiza umoja na msikamano baina ya Mataifa.

Kiswahili kinapaswa kuendelezwa na kudumishwa
Kiswahili kinapaswa kuendelezwa na kudumishwa   (Tanzania State House)

Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Nchini Sweden waadhimisha: Hata hivyo baadhi ya mataifa mbalimbali duniani yameadhimisha Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani ambapo Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Sweden ukishirikiana na Jumuiya za Watanzania waishio nchini humo, uliandaa na kufanikisha sherehe za maadhimisho makubwa ya Siku ya Lugha ya Kiswahili Duniani yaliyofanyika tarehe 5 Julai, 2025, jijini Stockholm. Maadhimisho haya hufanyika duniani tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuanzia mwaka 2022 kufuatia azimio lililopitishwa na Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO). Akizungumza katika maadhimisho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mhe. Mobhare Matinyi, alielezea namna    Serikali ilivyoazimia kueneza na kukienzi Kiswahili duniani kote huku akielezea namna kilivyosambaa na kuongeza kuwa kwa ushawishi wa Tanzania, Kiswahili sasa ni lugha ya kikazi Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC). Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo alikuwa Waziri wa zamani wa Usawa na Jinsia nchini Sweden, Mhe. Nyamko Sabuni, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) lakini aliyezaliwa Burundi na kukulia Tanzania kabla ya kuhamia Sweden. Mhe. Nyamko akitoa hotuba yake kwa Kiswahili alielezea namna kinavyoziunganisha nchi hizi akisema hata anapokuwa nchini Kenya kibiashara hutumia pia lugha ya Kiswahili. Sherehe hizo zilifana kwa wingi wa vyakula na vitu mbalimbali vinavyoitangaza Tanzania na utamaduni wa Mswahili kama viungo, maonesho ya mitindo ya mavazi, sanaa za mapambo, ngoma, nyimbo, mashairi na hadithi za watoto. Shughuli hii ya kipekee iliwakutanisha zaidi ya watu 500 ambao mbali ya Watanzania wengine walikuwa ni raia au wenye asili za nchi za Afrika Mashariki na Kati, Waswidi marafiki wa Tanzania na Mabalozi na wawakilishi wa nchi za Botswana, China, Eritrea, India, Japan, Kenya, Misri, Nigeria, Rwanda na Zimbabwe.

Lugha ya Kiswahili inazidi kukua na kupanuka
Lugha ya Kiswahili inazidi kukua na kupanuka

Japan waadhimisha siku ya Kiswahili Duniani: Tarehe 7 Julai 2025, Tanzania kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa lugha ya Kiswahili nchini Japan, iliadhimisha Siku ya Kiswahili Duniani katika Maonesho ya Dunia ya EXPO 2025 katika kisiwa cha Yumeshima, jijini Osaka, Japan. Maadhimisho haya yaliambatana pia na hafla rasmi ya kufunga Wiki ya Utamaduni na Kiswahili, iliyokuwa sehemu ya maonyesho hayo ya kimataifa chini ya Kaulimbiu: “Kiswahili kwa Amani na Mshikamano.” Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau wa Kiswahili kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Japan, wanataaluma, wanafunzi, wanadiaspora wa Kitanzania, wanadiplomasia kutoka nchi mbalimbali za nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), pamoja na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa kama vile UNESCO. Mgeni sasmi wa tukio hilo alikuwa Mheshimiwa Baraka Luvanda, Balozi wa Tanzania nchini Japan. Katika hotuba yake, Balozi Luvanda alisisitiza kuwa Kiswahili ni zaidi ya lugha; ni kiungo cha urithi wa utambulisho wa Taifa la Tanzania na Afrika kwa ujumla. Alieleza kuwa kukua kwa Kiswahili katika majukwaa ya kimataifa ni ushahidi wa nguvu ya lugha hiyo katika kujenga maelewano, mshikamano na amani baina ya mataifa. Aidha, aliipongeza UNESCO kwa kutambua rasmi tarehe 7 Julai kuwa Siku ya Kiswahili Duniani, pamoja na Serikali ya Japan kwa kuendeleza ushirikiano wa kiutamaduni na kitaaluma na Tanzania.

Lugha ya Kiswahili inaendelea kuimarisha urafiki na mshikamano
Lugha ya Kiswahili inaendelea kuimarisha urafiki na mshikamano   (AFP or licensors)

Katika kilele cha tukio hilo, Kamusi Ndogo ya Kiswahili-Kijapani ilizinduliwa rasmi kwa ushirikiano wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) na Chuo Kikuu cha Osaka, kama mojawapo ya hatua za kuimarisha tafsiri na mawasiliano baina ya jamii mbili. Aidha, Hati ya ushirikiano (MOU) kati ya SUZA na Chuo Kikuu cha Osaka ilisainiwa, ikishuhudiwa na Balozi Luvanda, ikiwa ni ishara ya kuimarika kwa ushirikiano wa kitaaluma baina ya Tanzania na Japan katika kukuza Lugha ya Kiswahili. Maadhimisho hayo pia yalipambwa na burudani mbalimbali za kitamaduni zikiwemo mashairi ya Kiswahili, ngonjera kutoka kwa wanafunzi wa Kiswahili wa Chuo Kikuu cha Osaka, wimbo maalum kutoka Shule ya Awali ya SANAE, na ngoma kutoka kikundi cha JT-STARS. Hafla hii ilikuwa jukwaa la kuonesha ushawishi wa Kiswahili si tu kama lugha ya mawasiliano, bali pia kama nyenzo ya kuendeleza utamaduni, utalii, diplomasia na elimu ya kimataifa. Katika kuwatambua wadau waliochangia kwa kiwango kikubwa katika kukuza Kiswahili nchini Japan, taasisi 11 na watu binafsi walitunukiwa Tuzo Maalum za BAKITA, zikitolewa na Mheshimiwa Balozi Luvanda. Waliopewa tuzo hizo ni pamoja na vyuo vikuu mashuhuri kama Osaka, Kyoto, TUFS, Waseda, Sophia, Soka, pamoja na Shirika la Utangazaji la Japan - NHK World (Idhaa ya Kiswahili), Bi. Midori Uno, na vikundi vya wanafunzi wa Kiswahili. Maadhimisho haya yameonesha kwa vitendo dhamira ya Tanzania kuendelea kueneza Kiswahili duniani kupitia ushirikiano wa kimataifa, hususan kwa washirika wa maendeleo kama Japan. Ni matarajio ya wengi kuwa maadhimisho haya yataendelea kuleta msukumo mpya katika kukiweka Kiswahili katika safu za juu za lugha za kimataifa, sambamba na kuimarisha urafiki wa muda mrefu kati ya Tanzania na Japan.

Lugha ya Kiswahili

 

09 Julai 2025, 16:17