MAP

Siku ya Mtoto wa Afrika: Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2025 ni "Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tuendako.” Siku ya Mtoto wa Afrika: Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2025 ni "Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tuendako.”  

Siku ya Mtoto wa Afrika 2025: Haki ya Mtoto: Tulipotoka, Tulipoo Na Tuendako!

Chimbuko ni mauaji ya watoto takribani 2,000 yaliyofanywa na Utawala wa Makaburu, nchini Afrika Kusini tarehe 16 Juni, 1976, wakati wa maandamano ya wanafunzi kwa lengo la kupinga mfumo wa elimu ya kibaguzi iliyokuwa inatolewa na Utawala wa Afrika Kusini. Mwaka 1991 Umoja wa Nchi za Afrika walifanya uamuzi wa kuenzi siku hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya watoto hao. Kaulimbiu kwa mwaka 2025 ni "Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tuendako!

Na Dkt. Dorothy Gwajima (Mb), - Dodoma, Tanzania.

Ndugu Wanahabari, tarehe 16 Juni ya kila mwaka, Tanzania huungana na Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika katika maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika. Chimbuko la maadhimisho haya ni mauaji ya watoto takribani 2,000 yaliyofanywa na Utawala wa Makaburu katika Kitongoji cha Soweto, nchini Afrika Kusini tarehe 16 Juni, 1976. Mauaji hayo yalitokea wakati wa maandamano ya wanafunzi kwa lengo la kupinga mfumo wa elimu ya kibaguzi iliyokuwa inatolewa na Utawala wa Afrika Kusini. Mwaka 1991 viongozi wa Umoja wa Nchi za Afrika walifanya uamuzi wa kuenzi siku hiyo ikiwa ni kumbukumbu ya mauaji ya watoto hao. Ndugu Wanahabari, Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika kwa mwaka 2025 ni "Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tuendako.” Kaulimbiu inatutaka kutafakari upatikanaji wa haki za watoto tangu zilipoainishwa na Sera ya Maendeleo ya Mtoto mwaka 2008. Aidha, Maadhimisho yanalenga kuwaelimisha na kuwakumbusha wazazi au walezi na watoa huduma wote wajibu wao katika kutekeleza haki tano za msingi za mtoto ambazo ni haki ya kuishi kwa mtoto bila kukatisha uhai wake, haki ya kuendelezwa kielimu, kiutamaduni na vipaji vya mtoto, haki ya kulindwa dhidi ya ukatili wa aina yoyote, haki ya kushiriki kutoa maoni katika masuala yanayomuhusu mtoto kulingana na umri wake na haki ya kutobaguliwa kwa mtoto kutokana na hali yake.  Ndugu Wanahabari, kwa mujibu Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya watoto wote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni milioni 30.3 (wavulana milioni 15.1 na wasichana 15,2) sawa na asilimia 49 ya watanzania Milioni 61.7. Kwa takwimu hizo inaonyesha kwamba nusu ya Watanzania ni watoto chini ya miaka 18 ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa katika siku za usoni. Hivyo, ni muhimu kuwekeza katika nyanja zote za malezi, makuzi na ulinzi wao ili waweze kukua na kufikia ukuaji timilifu kwa faida yao binafsi, Familia na Taifa kwa ujumla.

Kauli mbiu: Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tunapokwenda
Kauli mbiu: Haki za Mtoto: Tulipotoka, Tulipo na Tunapokwenda   (ANSA)

Ndugu Wanahabari, katika kuhakikisha kundi hili kubwa kwenye jamii yetu linaendelezwa na kufikia malengo yao, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwapa huduma za afya na lishe bora, kuwaendeleza kielimu na kiutamaduni, kuwalinda dhidi ya vitendo vya ukatili na kuwashirikisha katika maamuzi mbalimbali yanayowahusu watoto bila ubaguzi. Aidha, Serikali imekuwa ikiandaa na kutekeleza programu, mipango na mikakati mbalimbali kwa lengo la kuhakikisha kwamba huduma bora na zenye tija zinawafikia watoto wote nchini ikiwa ni sehemu ya haki zao za msingi. Ndugu Wanahabari, katika kutekeleza haki ya kuishi ya mtoto, Serikali imejenga mbiundombinu ya kutolea huduma za afya ya mama na mtoto kote nchini ambapo jumla ya Hospitali za kanda 6, Hospitali za Rufaa 28, Hospitali za Wilaya 129, Vituo vya Afya 345 na Zahanati 1,158. Lengo likiwa ni kufikisha huduma za Afya ikijumuisha huduma za mama na mtoto jirani na wananchi. Mbiundombinu hiyo imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya watoto wadogo hapa nchini. Kwa mujibu wa Taarifa ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania ya mwaka 2022, idadi ya vifo vya watoto chini ya miaka 5 vimepungua kutoa vifo 147 kwa vizazi hai 1,000 hadi vifo 43 kwa vizazi hai 1,000. Aidha, udumavu wa watoto chini ya miaka 5 umepungua kutoka asilimia 32 hadi 30. Serikali kwa kushirikiana na Wadau inaendelea kutoa elimu ya afya na lishe bora kwa watoto ili kuboresha afya za watoto hapa nchini. Ndugu Wanahabari, katika eneo la haki ya kuendelezwa ya mtoto, Serikali imeimarisha miundombinu ya shule za msingi na sekondari ili kuongeza wigo wa idadi ya watoto wanaopata elimu hapa nchini.

Watoto wana haki ya kuishi katika mazingira bora na salama
Watoto wana haki ya kuishi katika mazingira bora na salama   (ANSA)

Kwa mujibu wa Taarifa ya OR- TAMISEMI idadi ya shule za msingi zimeongezeka kutoka shule 16,406 mwaka 2021 hadi kufikia shule 17,986 kwa mwaka 2024/2025. Aidha, idadi ya shule za sekondari zimeongezeka kutoka 3,863 mwaka 2020/2021 hadi shule 4,894 kwa mwaka 2024/2025. Vilevile, Serikali imeongeza bajeti ya elimu bila malipo kutoka Shilingi Bilioni 249.66 mwaka 2020/2021 hadi Shilingi Bilioni 484.27 kwa mwaka 2024/2025 sawa na ongezeko la asilimia 93.97. Jitihada hizi zimechangia kuongezeka kwa idadi ya watoto walioandikishwa kujiunga na shule mbambali hapa nchini. Kwa upande wa shule za msingi takwimu zinaonyesha kuwa; katika kipindi cha mwaka 2023/24 hadi 2024/25 idadi ya wanafunzi walioandikishwa katika shule za msingi za umma iliongezeka kutoka watoto 10,460,785 hadi watoto 10,739,975 sawa na ongezeko la asilimia 2.7. Pia, idadi ya watoto katika shule za sekondari iliongezeka kutoka watoto 2,172,257 hadi 2,999,530 sawa na ongezeko la asilimia 38. Ndugu Wanahabari, Serikali pia imefanya juhudi kubwa za kumlinda mtoto dhidi ya vitendo vya ukatili nchini. Katika kudhihirisha hilo, Mei, 2024 umezinduliwa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA 2024/25 – 2028/29 wa awamu ya pili). Aidha, marekebisho ya baadhi ya Sheria yamefanyika ikiwemo Sheria ya Mtoto Sura ya 13, Sheria ya Makosa ya Mtandao Sura ya 443 na Sheria ya Msaada wa Kisheria Sura ya 23 kwa 2 kuingiza masharti yatakayoimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto. Viel vile, Serikali imeweka mifumo imara ya ulinzi na usalama wa mtoto katika ngazi ya familia kwa kutoa elimu ya malezi kwa wazazi na walezi ambapo jumla ya vikundi vya malezi chanya 4,890 vimeanzishwa kwa ajili ya kuendeleza elimu hiyo katika jamii.

Watoto wanapaswa kuendelezwa kielimu, kiafya, kiutu na kimaadili
Watoto wanapaswa kuendelezwa kielimu, kiafya, kiutu na kimaadili

Ndugu Wanahabari, Serikali imeweka mifumo imara ya ulinzi na usalama wa mtoto katika jamii. Jumla ya Madawati 420 ya Jinsia na Watoto katika vituo vya Polisi, Madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto Shuleni na Nje ya Shule 4,082, Nyumba salama 15 kwenye Mikoa 13 kwa ajili ya watoto manusura wa ukatili na Vituo 32 vya Huduma ya mkono kwa mkono vimeanzishwa. Aidha, kuanzia Februari, 2024 Serikali kwa kushirikiana na Wadau imetekeleza kampeni ya usalama wa mtoto mtandaoni kwa ajili ya kuwaelimisha wazazi, watoto wenyewe na walimu kuhusu usalama wa watoto wanapotumia mitandao ikiwa pamoja na uwezekano wa kufanyiwa vitendo vya ukatili. Kampeni hiyo imefanyika katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara na kufikia jumla ya watoto 786,901, wazazi/walezi 821,098 na Maafisa wa Serikali 516 kutoka katika Mikoa na Halmashauri nchini. Ndugu Wanahabari, Watoto pia wanayo haki ya kushiriki katika masuala mbalimbali yanayowahusu kulingana na umri wao. Katika kuimarisha ushiriki wa watoto, Serikali imeingiza masuala ya uanzishaji na uendeshaji wa mabaraza ya watoto nchini katika Sheria ya Mtoto Sura ya 13 na hivyo kuwa ni suala la kisheria katika kuanzisha mabaraza hayo katika ngazi ya Vijiji au Mitaa hadi ngazi ya Taifa. Hadi kufikia Aprili, 2025 kulikuwa na Mabaraza ya Watoto 1,460 yaliyoanzishwa katika Mikoa mbalimbali. Kupitia mabaraza hayo watoto wanapata fursa ya kujifunza stadi mbalimbali za maisha ikiwa ni pamoja na kujikinga na maambukizi ya VVU, usafi na uhifadhi za Mazingira, uzalendo, maadili mema na kukabiliana na mabadiliko ya Tabia Nchi na masuala mengine mtambuka. Ndugu Wanahabari, katika kuhakikisha kuwa kuwa watoto wanashiriki kutoa maoni kwenye masuala ya kitaifa, mwezi Septemba, 2024 jumla ya watoto 411 kutoka Mikoa 4 ya Tanzania waliwakilisha watoto wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kutoa maoni katika maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050. Mikoa iliyoshiriki ilikuwa Dar es salaam, Mwanza, Kigoma na Unguja ambapo maoni ya watoto yalikusanywa na kukabidhiwa kwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango na hatimaye kujumuishwa katika Dira ya Taifa ya 2050.

Watoto wa Afrika wanapaswa kuendelezwa kiroho pia
Watoto wa Afrika wanapaswa kuendelezwa kiroho pia   (AFP or licensors)

Ndugu Wanahabari, Serikali pia imekuwa ikifuatilia kwa karibu ushiriki wa watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalum katika shughuli zote zinazomhusu mtoto bila ubaguzi aina yoyote ambao unaweza kusababishwa na hali bora ya kipato, rangi, jinsi, utaifa wala ukabila. Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeandaa Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi ili kuwezesha watoto wote kupata fursa ya elimu kama ilivyoelekezwa katika Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2023. Aidha, Serikali imeandaa Mwongozo wa Utambuzi wa Mapema wa Watoto wenye Ulemavu wa mwaka 2022 ili kuwatambua na kuwahudumia Watoto mapema kwa lengo la kupunguza makali ya ulemavu wao. Vilevile, Serikali 3 imendaa Mpango wa Taifa wa haki na Ustawi wa Watu wenye Ulemavu wa ngozi kwa ajili ya kuimarisha afya na ulinzi wa kundi hilo nchini. Ndugu Wanahabari, maadhimisho ya mwaka huu, 2025 yanafanyika Kimkoa na Wizara itashirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kupeleka maelekezo mbalimbali kuhusiana na maadhimisho hayo. Aidha, Wizara inapendekeza shughuli zifuatazo zifanyike kulingana na uwezo na mazingira ya Mkoa husika: i. ii. iii. iv. Kuandaliwa kipindi maalum cha Redio au Runinga ambacho wataalam na viongozi wa Mkoa watajadili mada kuhusu Haki za Mtoto na kufanya tathmini kuhusu upatikanaji wa haki hizo katika Mkoa, Kufanya Midahalo na Makongamano katika Vyuo Vikuu na Vyuo vya Elimu ya Kati vikijumuisha jamii inayowazunguka vilivyopo katika Mikoa husika ili kujadili hali ya utoaji wa Haki za Watoto, Viongozi wa dini wahamasishwe kutumia nyumba za ibada kutoa ujumbe mahsusi kuhusu Haki na Wajibu wa Watoto katika familia na jamii, Watoto wahimizwe kusoma na kujifunza kwa bidii stadi za kazi na kujizuia kushiriki katika vitendo viovu na venye uvunjifu wa maadili katika jamii.

Watoto ni Baraka na Neeema kutoka kwa Mungu
Watoto ni Baraka na Neeema kutoka kwa Mungu

Ndugu Wanahabari, kabla ya kuamaliza maelezo yangu, napenda kutoa rai kwa wanahabari na wananchi wote wanaotekeleza afua za ulinzi na haki za mtoto kushirikiana na Serikali katika kutoa elimu kuhusu Sheria, Sera na Miongozo mbalimbali inayolinda haki za watoto nchini. Aidha, tunatamani kuona mtoto wa kitanzania anapata haki zake za msingi nilizoainisha ikiwa pamoja na salama wake wakati wote na kwamba ulinzi wa watoto wetu liwe ni jukumu letu sote.  Mwisho, nawaomba wanahabari muendelee kufichua vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hasa vitendo vya ubakaji, ulawiti na mimba za utotoni kwani ndio vitendo vinavyoongoza kufanyiwa watoto katika jamii kwa sasa.

Dkt. Dorothy Gwajima (Mb)

WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM.

Mtoto wa Afrika
16 Juni 2025, 06:49