Rais wa Zamani wa Zambia Lungu afariki dunia
Na Sarah Pelaji na Angella Vatican.
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Zambia, Bwana Edgar Chagwa Lungu, amefariki dunia, tarehe 5 Juni 2025, akiwa na umri wa miaka 68. Taarifa rasmi za kifo chake zimetolewa na chama chake cha Patriotic Front (PF)kikithibitisha kuwa Lungu alifariki dunia akiwa katika matibabu maalum katika Hospitali ya Mediclinic Medforum mjini Pretoria, Afrika Kusini. Bwana Lungu alilitumikia taifa la Zambia kama Rais kwa miaka sita kuanzia 2015 hadi Agosti 2021. Alichukua uongozi baada ya kifo cha Rais Michael Sata na alichaguliwa tena kwa muhula kamili mwaka 2016. Katika uchaguzi wa mwaka 2021, alishindwa na mpinzani wake wa muda mrefu, Hakainde Hichilema. Baada ya kushindwa katika uchaguzi huo alijiondoa kwenye siasa lakini baadaye akarejea na kuonekana kuwa na nia ya kugombea tena urais.
Bwana Lungu alitembelea mjini Vatican 2016
Akiwa katika uongozi wake mwaka mmoja tangu kuchaguliwa, pamoja na safari zake za ndani na Nje, ilikuwa ni tarehe 5 Februari 2016 ambapo Baba Mtakatifu Francisko alikutana naye katika Jumba la Kitume ambapo mara baada ya Mkutano huo Rais Lungu pia alikutana na Kardinali Pietro Parolin, Katibu Mkuu wa Vatican akiambatana na Askofu Mkuu Paul R. Gallagher, Katibu wa Mahusiano, Ushirikiano na Mataifa na Mashirika ya kimataifa. Katika mazungumzo yao na Sekretarieti ya Vatican walionesha uhusiano mzuri uliopo kati ya Vatican na Jamhuri ya Zambia. Mchango wa Kanisa Katoliki kupitia taasisi zake za kielimu, kijamii na kiafya ulijadiliwa, bila kukosa kurejea ushirikiano katika mapambano dhidi ya umaskini na kukosekana kwa usawa wa kijamii na uendelezaji wa kuishi pamoja kwa amani kijamii na kidini kwa njia ya utamaduni wa mazungumzo na kukutana. Katika muendelezo wa mazungumzo hayo, mada za maslahi ya pamoja zilishughulikiwa, ikiwa ni pamoja na uhamiaji, mabadiliko ya tabianchi na ulinzi wa mazingira. Hatimaye walirejea kuhusu hali ya kimataifa, kwa kuzingatia zaidi migogoro inayoathiri baadhi ya maeneo ya Afrika na dhamira ya nchi katika mchakato wa amani katika Kanda.”
Kabla ya Urais
Kabla ya kuwa Rais, Bwana Lungu alihudumu katika nyadhifa mbalimbali serikalini, ikiwa ni pamoja na Waziri wa Ulinzi na Waziri wa Sheria. Alikuwa mwanachama wa chama cha Patriotic Front na alichaguliwa kuwa Mbunge wa Chawama mwaka 2011. Ikumbukwe kuwa Mahakama ya Katiba nchini mwaka 2024 iliamua kuwa kwamba Rais wa zamani Edgar Lungu hawezi kugombea tena katika uchaguzi wa mwaka 2026 kwa sababu tayari amehudumu mihula miwili ya urais. Pia Mahakama hiyo iliamua kuwa kipindi ambacho Lungu alihudumu kama rais wa taifa hilo la Afrika Kusini kati ya mwaka 2015 hadi 2016 baada ya kifo cha Michael Sata akiwa madarakani, kinahesabiwa kama muhula kamili. Lungu alishinda uchaguzi kwa muhula wa pili kutoka mwaka 2016 hadi 2021.
Mapendeleo ya kurudi katika kinyang’anyiro cha uchaguzi 2026
Wakati Bwana Lungu alitangaza kurejea kwenye siasa mwaka 2024 na alikusudia kumkabili Rais wa sasa Hakainde Hichilema katika uchaguzi mkuu ujao wa 2026, kuliibuka uhasama katika yake na Rais wa sasa. Uhasama huo umeifanya kesi hiyo kuvutia watu wengi nchini Zambia, na uamuzi wa jopo la majaji saba ulitangazwa moja kwa moja kwenye runinga na Radio ya Taifa. Kesi hiyo iligubikwa na madai ya kuingiliwa kwa mahakama baada ya Hichilema kuwafuta kazi majaji watatu wa Mahakama ya Katiba ambao hapo awali walikuwa wametoa uamuzi kwa niaba ya Lungu katika kesi iliyohusiana na uchaguzi wa 2016. Hata hivyo Lungu alisema kwamba hukumu hiyo imeendeshwa kwa mikono ya ushawishi wa kisiasa. Zambia ni moja ya wazalishaji wakubwa wa shaba duniani lakini imeathiriwa vibaya na ukame wa kikanda uliosababisha mazao kuharibika na mamilioni ya watu kuwa katika hatari ya kukumbwa na baa la njaa.