MAP

Dominika ya tarehe 7 Septemba 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV anamtangaza Mwenyeheri Carlo Acutis kuwa Mtakatifu kijana wa nyakati zetu, matendo makuu ya Mungu. Dominika ya tarehe 7 Septemba 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV anamtangaza Mwenyeheri Carlo Acutis kuwa Mtakatifu kijana wa nyakati zetu, matendo makuu ya Mungu.  (ANSA)

Mwenyeheri Carlo Acutis Ameugusa Sana Moyo Wangu Kama Mzazi!

Nilijikuta nawatamani mno wazazi wa Carlo. Carlo ni Mwenyeheri wa kwanza wa kizazi cha sasa ''Millennials''; Mwenyeheri wa kwanza kutumia mtandao wa intaneti na kuwa na simu ya mkononi. Mwenyeheri wa kwanza katika historia ya Kanisa ambaye amezikwa kwa mavazi ya kawaida: (Jeans, T-shirt, na Hoodie na Raba), mavazi ambayo yanavaliwa sana na vijana wa kizazi kipya. Carlo ameyaishi maisha ya sasa. Ni mfano bora wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya!

Na Grace Patricia Kabogo, - Bonn, Ujerumani

Dominika ya tarehe 7 Septemba 2025 Baba Mtakatifu Leo XIV anamtangaza Mwenyeheri Carlo Acutis kuwa Mtakatifu kijana wa nyakati zetu, matendo makuu ya Mungu. Tarehe hiyo hiyo pia, Papa Leo XIV atamtangaza Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati kuwa Mtakatifu. Awali Mwenyeheri Carlo Acutis alikuwa atangazwe Mtakatifu Aprili 27, 2025, wakati wa kilele cha Jubilei ya Vijana Wadogo. Hata hivyo, tukio hilo kubwa liliahirishwa kutokana na kifo cha Baba Mtakatifu Francisko kilichotokea Aprili 21, 2025. Aidha, Mwenyeheri Pier Giorgio Frassati alikuwa atangazwe kuwa Mtakatifu Agosti 3, 2025, wakati wa kilele cha Jubilei ya Vijana. Hatimaye Papa Leo XIV aliamua kuichagua Septemba 7, kuwatangaza pamoja wenyeheri hawa vijana, kuwa watakatifu katika mkesha wa Sikukuu ya kuzaliwa kwa Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Tunaweza kusema safari ya Carlo Acutis kuelekea kuwa Mtakatifu imaunganishwa na Baba Watakatifu wanne. Mtakatifu Yohane Paulo II, Benedikto XIV, Francisko na hatimaye Papa Leo XIV. Carlo anayejulikana kuwa na Ibada ya kina kwa Ekaristi Takatifu, na matumizi yake ya mtandao wa intaneti katika kueneza imani yake, alivutiwa na kuongozwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Hata alikwenda kuhiji kwa ajili ya kumwona. Carlo aliyatoa mateso yake ya kuugua saratani ya damu kwa nia za Baba Mtakatifu Benedikto XIV. Carlo alitangazwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mwenyeheri, na sasa anasubiri kutangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Leo XIV.

Mwenyeheri Carlo Acutis alikuwa na Ibada ya pekee kwa Ekaristi Takatifu
Mwenyeheri Carlo Acutis alikuwa na Ibada ya pekee kwa Ekaristi Takatifu

Tukio la Mwenyeheri Carlo Acutis kutangazwa kuwa Mtakatifu linalotokea baada ya kushuhudiwa kwa muujiza wa pili unaohusishwa kupitia maombezi yake na kuthibitishwa mnamo Mei, 2024, na Hayati Baba Mtakatifu Francisko akatoa kibali Mei 2024 kuendelea na mchakato wa kumtangaza Carlo kuwa Mtakatifu. Muujiza wa pili uliotambuliwa na Papa Francisko ni uponyaji wa Valeria Valverde, msichana mwenye umri wa miaka 21 kutoka Costa Rica, ambaye alikuwa anakaribia kufa baada ya kupata ajali mbaya ya baiskeli na kuumia vibaya wakati akisoma mjini Florence, Italia kunako mwaka 2022. Mnamo Oktoba 10, 2020, Papa Francisko alimtangaza Carlo Acutis kuwa Mwenyeheri. Muujiza wa kwanza unaohusishwa na Carlo Acutis, hatua iliyosababisha atangazwe kuwa Mwenyeheri, ni kupona kwa mvulana mwenye umri wa miaka mitatu nchini Brazil mwaka 2013, ambaye aligunduliwa kuwa na tatizo la kuharibika kwa kongosho tangu alipozaliwa. Siku hii ilikuwa ya kipekee, sio tu kwa kwa wazazi na ndugu wa Carlo, bali kwa vijana wengi, wazazi, waamini wa Kanisa Katoliki, na hata wasio Wakatoliki, ambapo walishuhudia: Utakatifu na Ukuu wa Mungu kupitia maisha ya Carlo Acutis. Nilibahatika kuishudhuia siku hii kupitia runinga, ambapo Ibada ya Misa Takatifu ya Carlo ya kutangazwa kuwa Mwenyeheri ilifanyika katika Kanisa kuu la Mtakatifu Francisko wa Assisi, mjini Assisi, Italia. Mwili ulinisisimka sana. Nilijikuta nawatamani mno wazazi wa Carlo. Carlo ni Mwenyeheri wa kwanza wa kizazi cha sasa ''Millennials''; Mwenyeheri wa kwanza kutumia mtandao wa intaneti na kuwa na simu ya mkononi. Mwenyeheri wa kwanza katika historia ya Kanisa ambaye amezikwa kwa mavazi ya kawaida tuliyoyazoea: (Jeans, T-shirt, na Hoodie na Raba), mavazi ambayo yanavaliwa sana na vijana wa kizazi kipya. Carlo ameyaishi maisha ya sasa.

Carlo Acutis aliwainjilisha vijana wenzake kwa njia ya mtandao
Carlo Acutis aliwainjilisha vijana wenzake kwa njia ya mtandao   (@Vatican Media)

Wakati wa uhai wake, Carlo alivutiwa sana na Mtakatifu Dominic Savio msimamizi wa vijana, na Watakatifu Francisko na Yacinta (miongoni mwa Watoto Watatu wa Fatima) na pia Mtakatifu Francisko wa Assisi ambaye alikuwa kama mfano kwake wa kuigwa. Ni Mwenyeheri ambaye vijana wamepata mtu mwingine wa kumwangalia kama mfano wa kuigwa kwao na kumkimbilia, kama ilivyo kwa Mtakatifu Dominic Savio, Mtakatifu Somo wa Vijana aliyefariki akiwa na umri wa miaka 14 tarehe 09.03.1857. Carlo Acutis, alizaliwa Mei 3, 1991 London, Uingereza kwa wazazi Andrea Acutis na Antonia Salzano. Alijulikana sana kwa kuonesha mapenzi na ibada kwa Ekaristi Takatifu, ambayo ilikuja kuwa msingi mkuu wa maisha yake kabla ya kifo chake kilichotokea 12.10.2006 akiwa na umri wa miaka 15, huko Monza, Italia, baada ya kuugua Saratani ya damu (Leukemia). Mwaka 2013, mchakato wa kutangazwa Mtakatifu ulifunguliwa. Mwaka 2020 kaburi la Carlo lilifunguliwa na mwili wake ulikutwa haujaoza na uko katika hali nzuri kabisa. Lakini hivi sasa, miaka 34 baada ya kuzaliwa kwake, Mwenyeheri Carlo ameyagusa maisha ya watu wengi sana, kuliko ilivyokuwa kwa watakatifu wengine mashuhuri tunaowajua walivyofanya walipokuwa na umri wa miaka 34. Na ndiyo kwanza ameanza. Mwenyeheri huyu kijana alijitoa sana kwa kujaribu kuwashirikisha wengine zawadi ya imani. Tangu akiwa na umri wa miaka 11, alifundisha Katekesi na kuwatia moyo watoto na vijana kujitahidi kuchagua kuishi maisha adili na matakatifu. Nilipomfahamu, nilivutiwa na nia yake thabiti ya kutaka kumjua Mwenyezi Mungu; kwani alijitolea katika sala, ambapo alisali Rozari Takatifu kila siku tangu akiwa na umri mdogo. Tangu alipopokea Komunio ya Kwanza (Ekaristi Takatifu) alikuwa akihudhuria Misa kila siku. Aliwajali watu wasiojiweza, alivutiwa na kuwapenda watakatifu, alijifunza kompyuta kwa lengo la kubuni tovuti za kutangaza Neno la Mungu, Kueneza Ibada ya Ekaristi Takatifu na kumtangaza Bikira Maria. Aidha, alifundisha kuhusu maisha ya watakatifu. Hii ni changamoto kwetu sote ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu na Kanisa lake kwa njia ya maisha adili na matakatifu.

Carlo Acutis alikuwa na Ibada kwa Bikira Maria
Carlo Acutis alikuwa na Ibada kwa Bikira Maria   (AFP or licensors)

Hayati Papa Francisko amemtangaza Mwenyeheri Carlo Acutis, kuwa msimamizi wa vijana, Somo wa mtandao wa Intaneti, na mtu mwenye ushawishi katika programu za Kompyuta. Mwenyeheri Carlo amekuwa chachu ya vijana wengi, na hata watu wazima, wakiwemo wazazi ambao wanamkimbilia kwa ajili ya kuwaongoza na kuwaonesha njia watoto wao. Ni mfano wa kuigwa kwa vijana na kwa hakika kwetu sote wa jinsi ya kutumia vizuri maenndeleo makubwa teknolojia ya mawasiliano ya jamii, na hasa matumizi makubwa yajayo ya teknolojia ya akili mnemba bila kupumbazwa na kuwa waraibu wa teknolojia hiyo. Kulingana na Antonia, mama yake, katika maisha ya kawaida, Mwenyeheri Carlo Acutis alipenda sana michezo ya video, kama vile Nintendo, PlaySation na hata Xbox. Ingawa wakati wa michezo hiyo, aliwahimiza rafiki zake umuhimu wa kwenda Kanisani na kuungama dhambi zao, na kudhibiti au kupunguza muda wa michezo hiyo. Nikiwa kama mzazi, nayaakisi maisha ambayo vijana wangu wawili wanayapitia kwa kupenda pia michezo ya aina hiyo. Matamanio ya kila mzazi ni kuwaona watoto wake wakienenda katika njia ya kumfuasa Yesu Kristo na kuyaishi mafundisho yake na hivyo kujikita katika: maadili, utu wema na utakatifu wa maisha. Tuwaombee vijana wetu watumie vizuri maendeleo makubwa ya teknolojia kwa kulitangaza na kulishuhudia Neno la Mungu kama alivyofanya Mwenyeheri Carlo. Nimebahatika kuwaona kupitia vyombo vya habari wakiwa hai, Mtakatifu Yohane Paulo II, Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta, na hata Mwenyeheri Lucia (miongoni mwa Watoto Watatu wa Fatima), na kushuhudia wakitangazwa Watakatifu na Wenyeheri, lakini naweza kusema Mwenyeheri Carlo Acutis ameugusa sana moyo wangu, na hili nalijua fika ni kutokana na kutamani awaongoze na kuwaonesha njia ya kuishi utakatifu watoto wangu Norman na Colman.

Mwenyeheri Carlo Acutis
Mwenyeheri Carlo Acutis

Punde tu niliposikia habari za Mwenyeheri Carlo, nilimtambulisha kwa wanangu, na amekuwa miongoni mwa Watakatifu na Wenyeheri ambao ni Somo wa familia yangu. “Nikiwa kama Mama wa familia nimevutiwa sana na maisha yako ya ajabu. Upendo wako kwa Mungu, familia yako, na wengine ni mfano mzuri kwangu na kwa watoto wangu. Ninapokutazama kama mfano kwa watoto wangu, ninaomba na wao pia waweze kuonesha upendo wa kina kwa Mungu na jirani, na wajitoe kwa huruma maisha yao katika kuwatumikia wengine. Asante sana Mwenyeheri Carlo, kwa kuwa mwanga wa matumaini na msukumo kwa akina Mama kama mimi. Tunaomba urithi uliouacha uendelee kuhamasisha vizazi vijavyo, ili waishi kwa imani, matumaini na upendo thabiti.” Tumwombe Mwenyezi Mungu atusaidie tufanikiwe kuishuhudia Septemba 07, 2025 ili tukawe chachu na mashuhuda katika kulieneza zaidi Neno lake Takatifu. Pia tumwombe asaidie kuwaongoa na kuwaongoza vijana na kizazi kipya katika Kanisa, maisha adili na matakatifu. “Mwenyeheri Carlo Acutis tunakukimbilia huku tukikuomba uzibariki na kuziongoza familia zetu kila siku. Zilinde dhidi ya uovu, washa ndani ya mioyo ya wanafamilia wote upendo uliokuwa nao, na waweke karibu na Kristo Yesu na Bikira Maria. Amina! Hizi ni miongoni mwa nukuu nazozipenda kutoka kwa Mwenyeheri Carlo Acutis: ''Kuungana na Yesu milele, ni mpango wangu wa maisha.'' ''Bikira Maria ndiye mwanamke pekee maishani mwangu.'' ''Kwa kusimama mbele ya Yesu wa Ekaristi, tunakuwa watakatifu.'' "Huzuni ni kujitazama sisi wenyewe, furaha ni kumtazama Mungu." ''Ekaristi ni njia kuu ya kwenda mbinguni.'' "Ni rahisi kujihusisha na ya ulimwengu, lakini sauti yako ni muhimu." Mwenyeheri Carlo Acutis, Utuombee! Beato Carlo Prega per noi!

Carlo Acutis Sept. 2025
12 Agosti 2025, 14:50