Kard.Koovakad:Viongozi wa Kidini lazima wapoze migawanyiko na kuendeleza amani
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kardinali George Jacob Koovakad, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mazungumzo ya Kidini katika hotuba yake aliyoitoa tarehe 28 Agosti 2025 nchini Malaysia wakati wa Mkutano wa Pili wa Kimataifa wa Viongozi wa Dini alisisitiza kuwa: “ kupaza sauti zetu dhidi ya unyanyasaji na ubaguzi usio wa haki, kushughulikia kwa ujasiri sababu kuu za migogoro, na kusimama kidete kulinda nyumba yetu ya pamoja. Huu ndio wajibu mkubwa” walionao viongozi wa kidini katika ulimwengu wa sasa.” Hafla hiyo iliyofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo, Kuala Lumpur,kwa kuongozwa na kaulimbiu "Nafasi ya Viongozi wa Kidini katika Utatuzi wa Migogoro" ambayo iliandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Malaysia, kwa ushirikiano na Jumuiya ya Ulimwengu ya Waislamu. Kardinali Koovakad kwa njia hiyo aliendelea kubainisha kuwa: “Tumeunganishwa, tunategemeana, na hakuna taifa, hakuna dini, hakuna kiongozi anayeweza kukabiliana na changamoto za sasa peke yake." Kwa kushirikiana na serikali, mashirika ya kiraia, na vyombo vya habari, na kusikiliza sauti zinazopuuzwa mara nyingi sana za wanawake, watoto, vijana, na wengine, kufufua nguvu ya kiroho ya jumuiya zetu, kuongoza mioyo kuelekea huruma na uelewa."
Kardinali George Jacob Koovakad katika Mkutano wa Kimataifa wa Viongozi wa Kidini
Katika hotuba yake, alibainisha njia tatu ambazo viongozi wa kidini wanaweza kuchangia katika kuzuia, kutatua, na kuponya mizozo. Ya kwanza ni kujitahidi kuwa "sauti za amani, si vurugu." Hebu tuseme wazi: viongozi wa kidini hawapaswi kamwe kuchochea chuki. Hatupaswi kamwe kukuza, kuhalalisha, au kuunga mkono vurugu. Wito wetu ni wa juu zaidi: kuzuia uovu, kutatua mizozo, na kuponya migawanyiko. Ni lazima kila wakati tuhimize suluhisho zisizo na vurugu kwa mizozo. Ni hapo tu ndipo tunaweza kujenga ulimwengu unaostahili ubinadamu wetu wa kawaida.” Kardinali alikazia jinsi dini “hulaumiwa mara nyingi kuwa chanzo cha migogoro au hutumiwa vibaya kuwa chombo kinachofaa cha kuchochea migawanyiko au kuhalalisha uchokozi.”
Badala yake, alisisitiza kwamba "mizizi ya migogoro kwa kawaida huwa katika umaskini, ukosefu wa usawa, chochezi za kisiasa, kutengwa, na majeraha makubwa ya ukosefu wa haki, na mgawanyiko hutokana na matumizi mabaya ya mamlaka, mvunjiko wa kijamii ambao haujaponywa, na moyo wa mwanadamu unapopotea kutoka katika haki, huruma, na kutafuta ukweli." Hata hivyo, alisema kwamba katika kipindi chote cha historia, viongozi fulani wa kidini wamechangia, moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja, katika kuchochea au kuanzisha mizozo,” hasa wakati wa kuzingatia matukio “kama vile misimamo mikali ya kidini, vuguvugu la kisiasa la kidini, na misingi ya kidini. Ni lazima tukiri kwa unyoofu, kwamba ndani ya tamaduni zetu kuna watu binafsi na vikundi ambao, kwa jina la dini, wamepanda migawanyiko, wamefanya vurugu, na kusababisha uharibifu, au hata wametafsiri upya au kupotosha maandiko, mila, na historia ili kuhalalisha vurugu, wakiendeleza ubaguzi na kuwanyima uhuru wa dini nyinginezo zao halali.
"Imani hapaswi kamwe kutumiwa kama silaha"
Kwa sababu hiyo Kardinali Koovakad, alisisitza kwa viongozi wa kidini kwamba "wanaitwa" kuzikumbusha jumuiya zao kwamba imani haipaswi kamwe kuwa silaha, bali "nguvu ya uponyaji. Pia alinukuu mawazo ya Papa Francisko katika ujumbe wake wa hivi karibuni wa Pasaka,wakati wa Pasaka wa Urbi et Orbi, ambamo alitoa wito kwa wale wote "walio na majukumu ya kisiasa kutokubali mantiki ya hofu." Kisha alipongeza mikutano na mipango inayokuza amani na mazungumzo, kama vile Mkutano wa Kimataifa wa Viongozi wa Kidini, Hati ya "Udugu wa Kibinadamu kwa Amani ya Ulimwengu na Kuishi Pamoja," na Azimio la Makka na Mkataba wa Makka.
Haiwezekani kutulia kwa amani wakati kuna kilio cha ubinadamu ulimwenguni
Kardinali Koovakad kisha alifafanua kwamba viongozi wa kidini hawawezi "kupumzika kwa utulivu au kulala kwa amani" mbele ya "ulimwengu ambao kilio cha wanadamu waliojeruhiwa na kilio cha dunia iliyojeruhiwa vinasikika," hasa kile cha "watoto, wanawake na maskini. Kama viongozi wa kidini, tumeitwa kupaza sauti zetu kwa niaba ya wale wanaoteseka isivyo haki katika migogoro," "kusema kwa haki na ujasiri," na "kuponya, kwani hatimaye tutahukumiwa kwa matendo yetu ya huruma na upendo. Dini ina uwezo wa kipekee wa kuponya majeraha kupitia msamaha, lakini pia kupitia matumizi ya haki na bila kuficha ukweli.Uponyaji ni mwaliko kwa waathirika, na kwa wale wanaohusika, kutafakari juu ya uwezekano wa ubinadamu mpya kwa njia ya upatanisho." Kwa hakika, amani ya kweli na ya kudumu huanza na kuponya majeraha ya ndani ya wanadamu. Ni wakati tu mioyo itaponywa ndipo ulimwengu unaotuzunguka unaweza kusitawi kwa amani na upatanisho."
Kardinali George Jacob Koovakad wakati wa Mkutano wa Kimataifa wa Viongozi wa Kidini
Hatimaye, pendekezo la mwisho la Kardinali kwa viongozi wa kidini “kutengeneza mustakabali wa amani na mshikamano katika ulimwengu uliojeruhiwa na kutoaminiana, chuki na misimamo mikali ni kuwa na ujasiri wa kubomoa kuta za zamani na kuacha kujenga nyingine mpya, pia kutengeneza madaraja mapya ya mshikamano. Hakika, mwakilishi wa Vatican alielekeza kwenye mazungumzo ya kidini kama njia ambayo kwa miongo kadhaa imevunja vizuizi vya woga, ujinga na chuki.” Kardinali aliakisi kwa mfano, ahadi ya Kanisa, ambayo tangu kuchapishwa kwa Hati ya Mtaguso ya Nostra Aetate,( Nyakati zetu) Azimio la Muungano kuhusu Mahusiano na Dini Zisizo za Kikristo, kupitia Mapapa mbalimbali kuanzia Paulo VI hadi Papa Francisko na sasa Papa Leo XIV," limefikia dini "kuanzia Waislamu hadi Wabudha, Wayahudi, Wahindu, Wajanseni, Masingasinga, Watao, na wafuasi wa dini za kijadi." Pia alikumbuka maneno ya kwanza ya Baba Mtakatifu Leo XIV kwa wawakilishi wa mapokeo mengine ya kidini, ambapo alisema kwamba “kila jumuiya huleta mchango wake wa hekima, huruma, na kujitolea kwa manufaa ya ubinadamu.