MAP

Katika hafla ya kipekee na ya kihistoria ya kuadhimisha miaka 72 tangu kufariki kwa Mtumishi wa Mungu Mar Ivanios, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher aliongoza Ibada ya Misa Takatifu. Katika hafla ya kipekee na ya kihistoria ya kuadhimisha miaka 72 tangu kufariki kwa Mtumishi wa Mungu Mar Ivanios, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher aliongoza Ibada ya Misa Takatifu. 

Ziara ya Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher Nchini India: Yaliyojiri

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, aliongoza Ibada ya Misa Takatifu mbele ya maelfu ya waamini waliokusanyika katika mji wa Trivandrum, Kerala India mnamo tarehe 15 Julai 2015. Katika mahubiri yake Askofu mkuu Gallagher alisisitiza kuwa, maisha, mafundisho na utume wa Mar Ivanios ni hazina ya kiroho yenye thamani kwa Kanisa na kwa dunia nzima.: Muhimu: Umoja na huduma!

Na Sarah Pelaji, -Vatican

Katika hafla ya kipekee na ya kihistoria ya kuadhimisha miaka 72 tangu kufariki kwa Mtumishi wa Mungu Mar Ivanios, Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, aliongoza Ibada ya Misa Takatifu mbele ya maelfu ya waamini waliokusanyika katika mji wa Trivandrum, Kerala India mnamo tarehe 15 Julai 2015. Katika mahubiri yake Askofu mkuu Gallagher alisisitiza kuwa, maisha, mafundisho na utume wa Mar Ivanios ni hazina ya kiroho yenye thamani kubwa kwa Kanisa na kwa dunia nzima. Akizungumza kwa niaba ya Baba Mtakatifu Leo XIV Askofu mkuu Gallagher alitoa salamu za upendo na baraka kutoka Roma, akimwelezea Mar Ivanios kama Mtumishi mwaminifu wa Mungu ambaye alisimama kama taa ya matumaini na mshikamano wa Kikristo. Kwa mujibu wa ujumbe wa Papa Leo XIV, maisha ya Mar Ivanios yalijengwa na kusimikwa juu ya misingi mitatu: umoja, utakatifu, na huduma: misingi inayobeba ujumbe wa kina kwa dunia ya leo iliyojaa migawanyiko, chuki na tabia ya kutaka kulipizana kisasi. Mtumishi wa Mungu Mar Ivanios alizaliwa mwaka 1882 katika eneo la Mavelikara, Kerala. Alibatizwa kwa jina la Zakariya lakini baadaye alijulikana kama Geevarghese. Katika kipindi cha changamoto za kijamii na kidini, alisimama kama mtu mwenye maono aliyeamini kwamba Kanisa linaweza kuwa chombo cha umoja na upendo. Katika mwaka wa 1930, Mar Ivanios alichukua hatua ya kihistoria ya kuleta sehemu ya Kanisa la Malankara la Waorthodox wa Siria kuingia katika ushirika kamili na Kanisa Katoliki hatua iliyochukuliwa si kwa sababu za kisiasa, bali kama ushuhuda wa kiroho wa umoja wa Wakristo wote. “Umoja wa kweli hautokani katika kufanana au kuwa sawa bali unajengwa juu ya msingi wa upendo, heshima na majadiliano ya dhati,” alisema Askofu Mkuu Gallagher. Aliongeza kuwa dunia ya leo ina kiu ya mifano hai ya umoja na maisha ya Mar Ivanios ambayo ni mwanga wa matumaini unaotufundisha kuishi katika mshikamano na kutafuta njia za maelewano.

Askofu mkuu Gallagher akiwa na Maaskofu wa India
Askofu mkuu Gallagher akiwa na Maaskofu wa India

Elimu na Utume wa Maendeleo: Mbali na juhudi zake za kidini, Mar Ivanios alijitolea kwa dhati kukuza elimu kama njia ya kuimarisha maadili na kuendeleza jamii. Alianzisha shule na vyuo mbalimbali chini ya falsafa kwamba elimu haina budi kuwa ya kiroho na ya kijamii, ikigusa akili, moyo na roho. Alisisitiza pia elimu kwa wanawake jambo ambalo liliashiria ujasiri wake wa kuvunja mila na desturi za wakati ule.  “Alitamani kuunda kizazi cha waamini walioelimika, walio na huruma na walio tayari kulitumikia taifa lao na Kanisa kwa moyo wa sadaka,” alieleza Askofu Mkuu Gallagher huku akiongeza kuwa urithi huu wa kielimu ni zawadi ya kudumu kwa Kerala na India kwa ujumla. Uaminifu, Sala na Huduma: Katika hotuba yake, Askofu Mkuu Gallagher alikumbusha kuwa msingi wa maisha ya Mar Ivanios ulikuwa sala ya kina na maisha ya kijumuiya katika Bethany Ashram, ambayo aliianzisha kama mahali pa malezi ya kiroho na tafakari ya Injili. “Hakuna utume bila sala. Maisha ya Mar Ivanios yanatufundisha kwamba nguvu ya kweli ya kuleta mabadiliko inatokana na ushirika wa ndani na Mungu,” alisema. Aidha, alisisitiza kuwa maisha ya Mar Ivanios yalikuwa mfano wa mtumishi mwaminifu kama ilivyofundishwa katika Injili ya siku hiyo. Aliishi kwa tahadhari, uaminifu na kujitoa hata alipokumbana na upinzani na kutokueleweka. Alibeba msalaba wa migawanyiko kwa matumaini, akijitahidi kuwa daraja la upatanisho katika Kanisa.

Majandokasisi kutoka Seminari kuu ya Mt. Bikira Maria, Malankara
Majandokasisi kutoka Seminari kuu ya Mt. Bikira Maria, Malankara

Ujumbe wa Papa Leo XIV: Utume wa Huduma Inaoishi: Katika sehemu ya mwisho ya hotuba hiyo Askofu Mkuu Gallagher alisoma maneno ya Baba Mtakatifu Leo XIV aliyoyasema tarehe 29 Juni 2025 kuwa,’ Umoja katika Kanisa na kati ya Makanisa unakuzwa kwa msamaha na kuaminiana kuanzia katika familia na jumuiya zetu.’ Maneno haya yaliangazia umuhimu wa kujenga jamii zenye mshikamano kupitia tendo dogo la huruma na upendo wa kweli. Aliendelea kusisitiza kuwa kama Wakristo, tunapaswa kuwa mashahidi wa Injili kupitia maisha yetu ya kila siku katika familia, shule, kazini na jamii kwa ujumla. Wito huu wa kuwa watumishi waaminifu hauishii kwa viongozi wa dini tu bali ni wito kwa kila Mkristo aliyepewa dhamana ya kuwa mwanga wa dunia. Wito Hai kwa Kizazi Kipya: Kwa kumalizia, Askofu Mkuu Gallagher alitoa changamoto kwa waamini wote kuendeleza urithi wa Mar Ivanios. “Urithi wake si kumbukumbu ya historia bali ni wito hai kwa kila mmoja wetu kuishi imani kwa ujasiri, kutafuta umoja katika tofauti na kujitoa huduma ya upendo kwa wengine. Katika hafla hiyo, sala mbalimbali ziliongozwa kwa ajili ya kuuombea mchakato wa kumtangaza Mar Ivanios kuwa Mtakatifu, huku maelfu ya waamini wakitoa ushuhuda wa jinsi maisha yake yamewasaidia kiroho na kijamii. Maadhimisho haya hayakuwa tu tukio la kumbukumbu, bali yalikuwa mwaliko wa kutafakari nafasi ya kila mmoja katika kujenga Kanisa na dunia yenye amani, umoja na huruma kwa kuishi mfano wa mtumishi mwaminifu Mar Ivanios.

Askofu mkuu Gallagher akihutubia kwa waseminari wakuu
Askofu mkuu Gallagher akihutubia kwa waseminari wakuu

Jiwe la Msingi la Taasisi ya Theolojia ya Malankara lawekwa Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa, ameongoza sherehe ya uwekaji wa jiwe la msingi la Taasisi ya Taalimhu ya Malankara katika Seminari Kuu ya St. Mary’s Malankara, jijini Trivandrum India. Sherehe hiyo, iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Kanisa, wakiwemo makardinali, maaskofu, mapadre, wahadhiri, wanafunzi pamoja na wanajumuiya mbalimbali wa Kanisa la Malankara. Katika hotuba yake, Askofu mkuu Gallagher alisisitiza kuwa siku hiyo si tu kumbukumbu ya kihistoria, bali ni hatua ya kimkakati katika safari ya Kanisa la Malankara kuendeleza elimu ya taalimungu, uongozi wa kiroho, na huduma kwa jamii. Aliipongeza historia tajiri ya Kanisa hilo, likiwa na mizizi ya kitume na urithi wa viongozi waliotangulia, huku akihimiza kizazi cha sasa kuwa watunzaji wa dhamana hiyo takatifu. “Leo, tunakumbushwa kuwa hatujarithi tu kazi yao muhimu na mfano wao, bali pia tunawajibika kuwa watunzaji wema wa kile walichotukabidhi,” alisema kwa msisitizo Askofu mkuu Gallagher. Alieleza kuwa Taasisi hiyo mpya haitakuwa tu taasisi ya kitaaluma bali ni patakatifu pa tafakari ya kina, tafiti madhubuti na ukuaji wa kiroho wenye kubadilisha maisha. Alisisitiza kuwa vijana watakaopata elimu katika taasisi hiyo hapo watatayarishwa kuwa viongozi wa kiimani na kijamii, wenye maono, huruma na ujasiri wa kuijenga dunia yenye haki na amani.

Umuhimu wa sala katika maisha na utume wa Kanisa
Umuhimu wa sala katika maisha na utume wa Kanisa

Akizungumzia maono ya taasisi hiyo, Askofu mkuu Gallagher alisema kwamba inatarajiwa kuwa wazi kwa kupokea watu wote bila kujali asili au hali na kuwa mahali ambapo waliotengwa wanapata nafasi kwani wanayo haki ya kupata elimu sahihi. “Haki na huruma vinatembea pamoja na ambapo kila mtu anatiwa nguvu kufikia ndoto zao kupitia karama walizopatiwa na Mungu,” alisema. Hotuba hiyo, iliyopokewa kwa makofi na heshima kubwa, ilihitimishwa kwa sala maalum ya kuombea mafanikio ya ujenzi na ustawi wa Taasisi hiyo, pamoja na wito wa ushirikiano baina ya makleri, waamini walei, walimu, wanafunzi na wafadhili. Kwa kuwekwa kwa jiwe hili la msingi, Kanisa la Malankara linachukua hatua kubwa kuelekea kuimarisha elimu ya theolojia inayojibu changamoto za dunia ya sasa, huku likidumisha mizizi yake ya kiimani na huduma.

Askofu mkuu Gallagher India
18 Julai 2025, 16:20