Waziri Mkuu wa Italia Giorgia Meloni Akutana na Papa Leo XIV Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV Jumatano tarehe 2 Julai 2025 amekutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Italia, Giorgia Meloni mjini Vatican; ambaye baadaye alikutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa. Baba Mtakatifu Leo XIV na Waziri mkuu wa Italia katika mazungumzo yao wameridhishwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kati ya Vatican na Italia.
Kwa pamoja wamekazia umuhimu wa kujizatiti kikamilifu kwa ajili ya kutafuta na kudumisha amani nchini Ukraine, Ukanda wa Mashariki ya Kati pamoja na kuhakikisha kwamba, misaada ya kiutu inawafikia waathirika walioko Ukanda wa Gaza. Katika mazungumzo yao, viongozi hawa wawili wamekazia zaidi uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili bila kusahau mchango unaotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Italia.