MAP

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu ya Shukrani imekuwa ni ushuhuda wa mshikamano, upendo na umoja wa Kitaifa, tunu msingi zinazowatambulisha watanzania sehemu mbalimbali za dunia. Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu ya Shukrani imekuwa ni ushuhuda wa mshikamano, upendo na umoja wa Kitaifa, tunu msingi zinazowatambulisha watanzania sehemu mbalimbali za dunia.  (@Vatican Media)

Padre Erick Mgombera Aadhimisha Misa ya Shukrani: Umoja, Upendo

Haki, umoja na amani ni nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Kinzani, migogoro, vita na mipasuko ya kijamii inayojionesha sehemu mbalimbali za dunia ni changamoto kwa watanzania kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja wa kitaifa na amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Padre Erick Francis Mgombera aliyepewa Daraja Takatifu ya Upadre na Papa Leo XIV ameadhimisha Misa ya Shukrani!

Na Sarah Pelaji, -Vatican

Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo inanogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani: “Mahujaji wa Matumaini.” Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, tangu tarehe 23 hadi tarehe 27 Juni 2025 kumeadhimishwa matukio makuu matatu, yanayowashirikisha: Majandokasisi, Mapadre na Maaskofu kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ijumaa tarehe 27 Juni 2025 Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu ambaye kwa huruma, upendo, upole na unyenyekevu wa Moyo wake Mtakatifu, aliinuliwa pale juu Msalabani, akawa ni chemchemi ya huruma, upendo na uzima kwa watu wote wa Mungu. Kristo Yesu anatufahamu na anatupenda sisi sote, na kila mmoja wakati wa maisha yake. Hofu yake ya kifo katika bustani ya Mizeituni, na mateso yake yametolewa kwa ajili ya kila mmoja wetu: “Mwana wa Mungu… ambaye alinipenda akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” Ametupenda wote kwa moyo wa kibinadamu. Kwa sababu hiyo, Moyo Mtakatifu wa Yesu, uliotobolewa kwa sababu ya dhambi zetu, na kwa ajili ya wokovu wetu, unachukuliwa kama alama na ishara kuu ya mapendo yake yasiyo na mipaka ambayo kwayo Mkombozi, ambaye ni Mungu, anampenda Baba wa milele na watu wote bila kikomo.” KKK 478. Mtakatifu Yohane Paulo II kunako Mwaka 2002 alitenga Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, kuwa ni Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, ili waweze kujisadaka bila ya kujibakiza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wakleri watambue kwamba, wao ni viongozi na wachungaji wa watu wa Mungu. Wanatumwa kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Wamepakwa mafuta ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili na faraja inayobubujika kutoka katika upendo na huruma ya Mungu.

Padre Erick Francis Mgombera akitoa baraka kwa waamini
Padre Erick Francis Mgombera akitoa baraka kwa waamini

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu, Siku ya kuombea: toba, wongofu na utakatifu wa mapadre, Baba Mtakatifu Leo XIV ametoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 32 kutoka sehemu mbalimbali za dunia.Kanisa Barani Afrika limepata Mapadre wapya 13 na Kanisa Afrika Mashariki limebahatika kuwapata Mapadre 3 nao ni: Padre John Baptist Matovu kutoka Jimbo Katoliki la Masaka, Uganda, Padre Joseph Mutisya kutoka Jimbo Katoliki la Kitui, Kenya pamoja na Padre Erick Francis Mgombera kutoka Jimbo Katoliki la Ifakara, Tanzania. Baba Mtakatifu Leo XIV katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Ekaristi Takatifu ni chanzo na kilelel cha maisha na utume wa Kanisa; Mapadre wajitahidi kuishi upendo wa shughuli za kichungaji; Upadre ni huduma ya kuwatakatifuza watu wa Mungu, Upatanisho na Umoja katika upendo. Kwa kuwekewa mikono na kushukiwa na Roho Mtakatifu, Mashemasi wanakuwa ni Mapadre, changamoto na mwaliko wa kuwa ni Mapadre wenye upendo kwa Mungu na jirani; waadhimishaji waaminifu wa Mafumbo ya Kanisa, watu wa Sala na hasa Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Hekima, umoja na amani ni ngao muhimu za watanzania mahali popote pale walipo ili kuweza kudumisha uhuru na umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Haki, umoja na amani ni nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Kinzani, migogoro, vita na mipasuko ya kijamii inayojionesha sehemu mbalimbali za dunia ni changamoto kwa watanzania kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja wa kitaifa na amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Jumuiya ya Watanzania katika ubora wake
Jumuiya ya Watanzania katika ubora wake

Padre Erick Francis Mgombera ni Mtanzania wa Kwanza kupewa Daraja Takatifu ya Upadri na Papa Leo XIV ameadhimisha Ibada ya Misa ya Shukrani katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana kilichopo Mjini wa Roma mnamo tarehe 28 Juni 2025 ikiandaliwa na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi na kufanya Utume wao mjini Roma wakiwemo wazazi wake: Baba Francis Alfonce Mgombera na Mama Agatha Aghathon Lyabonga na Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara. Misa hiyo imeadhimishwa kwa heshima ya Moyo Safi wa Bikira Maria akiomba: Ulinzi, tunza na maongozi katika maisha yake ya upadre. Akitoa mahubiri katika Misa hiyo, Padre Edwin Lyanga wa Jimbo Katoliki Ifakara ambaye pia ndiye Baba wa Kiroho wa Padre Erick alimsihi kumwomba Bikira Maria amwongoze katika maisha yake ya upadre. “Hata ukipata changamoto kubwa kiasi gani mshirikishe Mama Bikira Maria na kuiga mfano wa maisha yake ambayo yaliongozwa na hekima ya kuhifadhi yote moyoni.,” alisema. Aidha afungamane na Kristo Yesu ambaye daima atamkuta Hekaluni yeye kama Kuhani analo jukumu la kuadhimisha Matakatifu ya Mungu, Kuongoza na kufundisha watu kweli ya Mungu.

Mahujaji kutoka Tanzania wakishiriki katika Ibada ya Misa Takatifu
Mahujaji kutoka Tanzania wakishiriki katika Ibada ya Misa Takatifu

Akitoa shukrani zake Katika siku yake hiyo ya   furaha Padre Erick alimshukuru Mungu kwa zawadi ya uhai, wito na kufanikisha maadhimisho ya kupata Daraja Takatifu ya Upadri.  “Ninamshukuru Papa Leo XIV kwa kunipa Daraja Takatifu la Upadre hapa Roma, si jambo la kawaida kupewa Daraja Takatifu la Upadre na Baba Mtakatifu Leo XIV hakika nimelichukulia kwa uzito mkubwa nikijawa na shukrani nyingi kwa haya Mungu aliyonitendea. Ninawashukuru wazazi wangu kwa malezi na kunisindikiza katika safari yangu ya wito. Hakika wao wameshiriki kunifanya hivi nilivyo. Pia ninamshukuru Askofu wa Jimbo Katoliki Ifakara Salutaris Melchior Libena kwa malezi ya kibaba na kutumia muda wake na majitolea makubwa kunipa nafasi ya kufika hapa Roma kupewa Daraja Takatifu ya Upadre na Baba Mtakatifu. Ni jambo la kipekee sana,” amesema Padri Erick huku akiwashukuru Watanzania wote walioko Roma waliompatia ushirikiano kufanikisha Upadrisho wake. Askofu Libena aliwashukuru Watanzania waliopo Roma kwa ushirikiano waliouonesha katika kufanikisha sherehe ya Daraja Takatifu ya Upadri kisha Misa ya shukrani ya Padre Erick Iliyofanyika Roma akieleza kwamba ameonja matunda ya umoja na mshikamano baina ya watanzania. “Umoja, upendo, amani na mshikamano ni nguzo zetu sisi Watanzania. Nilichokiona na kukishuhudia hapa Roma kimenistaajabisha na kutufanya sisi tuliomsindikiza Padre Erick kujiona tuko nyumbani. Safari yetu ilikuwa na watu watano tu, Mimi Askofu, Padri mmoja, wazazi wawili (baba na mama) na aliyekuwa Shemasi sasa ni Padre Erick. Tulikuja kama kundi dogo lakini wakati wa maadhimisho ya Daraja Takatifu ya Upadri nikaanza kuona kundi linaongezeka.

Mahujaji wa matumaini: Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo
Mahujaji wa matumaini: Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo

Tulivyomaliza Misa Takatifu nikaona kundi la Watanzania, Mahujaji kutoka Tanzania bila kujali masuala ya kufahamiana wao walithamini Utanzania wetu wakaanza kuimba na kupiga vigelegele, huku wengine wakiwa wamefanya maandalizi ya mapokezi, chakula nk. Leo tena katika Ibada ya Misa ya shukrani tumekutana na watu wengi wanatupa ushirikiano. Jambo hili limetupa nguvu nami nawasisitiza Watanzania kuendelea kudumisha umoja, udugu na amani,” alisema Askofu Libena. Aidha ametìsisitiza Watanzania kuendelea kuliombea Taifa la Tanzania linapoendelea kujiandaa na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 ili ufanyike kwa haki, amani na utulivu. Inafahamika kuwa katika hekaheka za uchaguzi kunatokea mivutano ya hapa na pale ya kisiasa ambayo inaweza kusababisha ukosevu wa utulivu na hatimaye uvunjifu wa amani hivyo Watanzania waendelee kumwomba Mwenyezi Mungu ili: Haki, amani na utulivu uendelee kudumu na uchaguzi ufanyike kwa amani.

Padre Erick Francis Mgombera akiwa na wazazi wake
Padre Erick Francis Mgombera akiwa na wazazi wake

Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara ameelezea namna ambavyo alipata nafasi ya kumpeleka Roma Shemasi wa Jimbo Katoliki Ifakara ili kupewa Daraja Takatifu ya Upadre akisema kuwa ulikuwa ni mwaliko wa Baba Mtakatifu Leo XIV katika kuadhimisha Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo na kwamba angalau kila Baraza la Maaskofu lipeleke mwakilishi mmoja (shemasi) ili apate Daraja Takatifu kwa Mkono wa Baba Mtakatifu. Hivyo TEC ikalipatia fursa Jimbo Katoliki Ifakara kupeleka mwakili ambapo tayari walikuwa na Shemasi aliyekuwa amekamilisha masomo yake katika Seminari Kuu ya Peramiho iliyopo Jimbo kuu la Songea. Hivyo Jimbo likamchagua ili awakilishe wengine katika maadhimisho hayo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Jubilei ya Majandokasisi, Mapadre na Maaskofu. Hata hivyo amempongeza Padre Erick kwa kupata nafasi hiyo adhimu ambayo hutokea mara chache sana, kwamba hata kama imetokea bahati lakini anaamini katika mpango wa Mungu kwamba alikuwa tayari ameshaandaliwa na Mungu kufikia maadhimisho hayo.

Askofu Salutaris Melchior Libena akiwa na Mapadre wa Ifakara.
Askofu Salutaris Melchior Libena akiwa na Mapadre wa Ifakara.

Baba Mzazi wa Padre mpya Mzee Francis Alfonce Mgombera alimshukuru Mungu kwa zawadi ya wito aliyomkirimia mtoto wake huku akimshukuru Askofu Libena kwa ushirikiano wake tangu kumchagua, kuratibu safari na maadhimisho hayo. Aliwashukuru Watanzania wote waliotoa ushirikiano kwao wakati wote wakiwa Roma. “Mimi na familia yangu ni wageni kabisa Roma na kwa kweli kuna wakati nilikuwa ninawaza namna itakavyokuwa kwani ni nchi ya ugenini, hatujui lugha lakini tulivyofika hapa mambo yalikuwa kinyume kutokana na ushirikiano tulioupata kutoka kwa Watanzania wanaoishi hapa Roma na mahujaji ambao walithamini utanzania wetu tu. Alielezea namna walivyopata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Papa Leo XIV na hatimaye kusalimiana naye. “Kwa kuwa hatujui lugha yake tulimsalimia kwa Kiswahili tukisema: Tumsifu Yesu Kristo, naye Papa Leo XIV akaitika “Milele amina’ tukafurahi sana huku akituambia kuwa anaifahamu Tanzania na anaipenda kwani alishawahi kufika Morogoro, Njombe na Songea. Alichukua muda kidogo kuzungumza nasi, basi tukafurahi sana,” alisema Mzee Mgombera.

Misa ya Shukrani
04 Julai 2025, 16:12