MAP

Wanawake Wakatoliki kutoka Barani Afrika ni mahujaji wa matumaini, wanakita mizizi katika imani na kufumbatwa katika utume wa pamoja kwa ajili ya familia, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na wajenzi wa amani. Wanawake Wakatoliki kutoka Barani Afrika ni mahujaji wa matumaini, wanakita mizizi katika imani na kufumbatwa katika utume wa pamoja kwa ajili ya familia, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na wajenzi wa amani. 

Mkutano wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika: Mahujaji wa Matumaini

Kwa hakika Wanawake Wakatoliki kutoka Barani Afrika ni mahujaji wa matumaini, wanakita mizizi katika imani na kufumbatwa katika utume wa pamoja: kwa ajili ya malezi na makuzi ya familia; kwa kusimama kidete kulinda na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; kulinda na kuendeleza kazi ya uumbaji na amani. Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe Mosi, Agosti 2025 wanaadhimisha mkutano mkuu, Entebe!

Na Mama Evaline Malisa Ntenga, - WUCWO, Entebe, Uganda.

Umoja wa Wanawake Wakatoliki Duniani, WUCWO, “Unión Mundial de las Organizaciones Femeninas Católicas, UMOFC, ulianzishwa kunako mwaka 1910, na unashirikiana kwa karibu sana na Vatican mintarafu masuala ya kijamii, kiroho, na kitamaduni yanayohusu: Ustawi, maendeleo na mafao ya wanawake na familia zao. Umoja wa Wanawake Wakatoliki Kanda ya Afrika kuanzia tarehe 28 Julai hadi tarehe 1 Agosti 2025 unaadhimisha Mkutano wake mkuu, Jijini Entebe, Uganda kwa kunogeshwa na kauli mbiu “Wekeza katika Malezi ya familia kama Daraja la maisha ya Furaha na Utakatifu.” Mkutano umefunguliwa na Askofu mkuu Paul Ssemogerere, wa Jimbo kuu la Kampla, Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Walei Baraza la Maaskofu Uganda tarehe 29 Julai 2025 kwa Ibada ya Misa Takatifu, kwenye Madhabahu ya Namgongo, Uganda. Katika mkutano huu, Makamu wa Rais wa Uganda, Meja Jenerali Mstaafu Jesca Alupo, alimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni katika mkutano huu. Alitumia fursa hii, kuwakaribisha wajumbe kutoka sehemu mbalimbali za Afrika na akawatakia amani na utulivu wakati wote wa mkutano. Rais Yoweri Kaguta Museveni alitamani kuhudhuria mwenyewe, lakini kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, ikambidi kumtuma mwakilishi. Rais Yoweri Kaguda Museveni amewachangia wanawake hawa kiasi cha Fedha ya Uganda milioni tano, ili zisaidie katika maadhimisho ya mkutano huu.

Askofu mkuu Paul Ssemogerere wa Jimbo kuu la Kampala, Uganda
Askofu mkuu Paul Ssemogerere wa Jimbo kuu la Kampala, Uganda

Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na Mama Evaline Malisa Ntenga, Rais wa Umoja wa Wanawake Wakatoliki Barani Afrika ambaye ni pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Wakatoliki Taifa nchini Tanzania, WAWATA. Mheshimiwa Mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Uganda, Meja Jenerali Mstaafu Jesca Alupo, ukimwakilisha Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, Viongozi wote wa Serikali mliohudhuria, Mhashamu Askofu Mkuu Paul Ssemogerere, Askofu Mkuu wa jimbo kuu la Kampala na Mwenyekiti wa Walei Baraza la Maaskofu Uganda, Monsinyori John Baptist – Mkurugenzi Utume wa Walei UGANDA, Padre Frederick Tusingire, Mkurugenzi wa Utume wa Familia Baraza la Maaskofu Katoliki Uganda. Mapadre wote, Watawa wote wakike na kiume, Wageni wetu, wakiwemo: Bi Monica Santamarina – Rais Mkuu (PG), Bi Maria Assumpta Gidudu – Rais wa UCWA, Bi Florence Kevin Kwesigabo – Mratibu wa Utume wa Familia, Bi Florence Mawejje – Mjumbe wa Bodi ya WUCWO Uganda, Bi Beatrice Tavares – Senegal, Bi Lucy Joycelin – Malawi, Bi Marie Salome Biogla – Cameroon, Bi Mary Asibi Gonsum – Nigeria, Bi Titi Kamano – Guinea Conakry, Bi Cecilia Asoyabayire – Ghana, Bi Doris Makhubu – Eswatini, na kwa namna ya pekee mtangulizi wangu mpendwa, Mama Olive Damian Luena, Viongozi wote wa dini, waheshimiwa wageni waalikwa, na dada zangu wapenzi katika Kristo, Itifaki ikiwa imezingatiwa. Mungu ni mwema – Kila wakati!

Wanawake Barani Afrika ni mahujaji wa matumaini
Wanawake Barani Afrika ni mahujaji wa matumaini

Mhashamu Baba Askofu mkuu, kabla sijaendelea na salamu, naomba uniruhusu nitambulishe wanawake walioshiriki kwa kutaja nchi zao: Eswatini, Ghana, Afrika Kusini, Nigeria, Senegali, Mali, Ivory Coast, Gabon, Guinea Conakry, Equatorial Guinea, Kenya, Malawi, Cameroon – pamoja na wawakilishi kutoka Marekani, Ujerumani na Uingereza, Tanzania, na mwenyeji wetu Uganda. Mhashamu Askofu Mkuu, Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kutuendeshea Ibada ya Misa Takatifu na kwa kuwa nasi leo. Tunalishukuru Kanisa Katoliki la Uganda kwa kuturuhusu sisi wanawake Wakatoliki kushiriki kikamilifu katika wito wetu kama Wakristo waliobatizwa. Ahsante kwa sala na maongozi yako. Kwa mioyo iliyojaa shukrani na imani, tumekusanyika hapa Namugongo – Uganda, Lulu ya Afrika, kwa ajili ya Mkutano wa Kanda ya Afrika wa Mashirika ya Jumuiya ya Umoja wa wanawake wakatoliki duniani, (WUCWO – world Union of catholic women organisation) 2025. Mkutano huu muhimu unawaleta pamoja wanawake Wakatoliki kutoka kila kona ya bara letu wakiwakilisha nchi 15 za Afrika na baadhi ya wajumbe kutoka Amerika, Uingereza na Ujerumani.

Madhabahu ya Namgongo, Uganda: Mashuhuda wa imani
Madhabahu ya Namgongo, Uganda: Mashuhuda wa imani

Tumekuja hapa Uganda kama Mahujaji wa matumaini, tukiwa na mizizi ya imani, tukiwa tumeunganishwa na dhamira ya pamoja: kulea familia, kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu, kulinda mazingira, na wajenzi wa amani. Tunafanya mkutano huu chini ya ulinzi wa Mama Bikira Maria, Mama wa Mungu na Malkia wa Amani, Msimamizi wetu. Kama alivyokaa thabiti chini ya Msalaba, nasi tunaitwa kusimama imara – katika imani, katika huduma, na katika tumaini. Mama Bikira Maria ni mfano wetu kamili: mnyenyekevu lakini mwenye nguvu, mkimya lakini mwenye sauti ya kinabii, mpole lakini asiyetikisika. Ndani yake tunauona ukamilifu wa mwanamke, mfuasi wa Kristo, na mwenye ujasiri na unyenyekevu wa kimama. Kaulimbiu yetu ya mwaka huu, “Wekeza katika Malezi ya familia kama Daraja la maisha ya Furaha na Utakatifu,” inatuita turudi katika moyo wa maisha ya kifamilia, na kuutambua tena wito wa ubaba na umama kama wito mtakatifu. Familia si tu shule ya kwanza ya maadili—ni Kanisa la kwanza la nyumbani. Tunapaswa kuwalea watoto waliojengwa katika ukweli, wanaoongozwa na imani, na wanaoiga mfano wetu.

Wanawake Barani Afrika ni mahujaji wa imani, matumaini na mapendo
Wanawake Barani Afrika ni mahujaji wa imani, matumaini na mapendo

Tunauthibitisha tena wito wetu wa kulinda mazingira yetu nyumba yetu ya pamoja, tukiongozwa na Waraka wa Kitume wa hayati Baba Mtakatifu Francisko, “Laudato si”, yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote.” Sisi kama wanawake wa Afrika tunaendelea na kazi ya uongofu wa kiekolojia kama sehemu ya mpango kazi wetu wa muda mrefu. Tulianza kazi hii—kupitia upandaji miti katika kampeni yetu ya Kupanda Tumaini – ‘Planting Hope,” kutunza mazingira kwa kusafisha maeneo yetu na kupinga matumizi ya plastiki, na kulinda vyanzo vya maji. Hata hivyo tunatambua wakati uliopo unatutaka tufanye zaidi. Kama anavyotukumbusha Baba Mtakatifu Leo wa kumi na nne, anaema: “Katika Kristo, sisi pia ni mbegu—mbegu za amani na tumaini.” Ndiyo, sisi ni mbegu hizo. Tunachanua katikati ya changamoto. Tunasimama kwa uvumilivu. Tunaleta tumaini mahali penye kukata tamaa. Kama wanawake hatupaswi kunyamaza tunapokutana na ukatili na ubaguzi dhidi ya wanawake. Kupitia Taasisi ya Ufuatiliaji wa changamoto za manyanyaso na ubaguzi kwa Wanawake Duniani (World Women’s Observatory) na mtandao wetu barani Afrika unaofanya kazi katika nchi 22, tunaendelea kukemea mifumo ya unyanyasaji na kujenga njia za uponyaji na kuwawezesha wanawake waliopitia changamoto hizo kujikwamua kiuchumi.

Wekeza katika malezi ya familia kama daraja ya maisha ya furaha na utakatifu
Wekeza katika malezi ya familia kama daraja ya maisha ya furaha na utakatifu

Tunaamini, kila maisha yaliyoinuliwa, kila sauti iliyosikika, kila msichana aliyelindwa/kuokolewaa kutoka katika biashara haramu ya binadamu—ni ushindi wa imani. Dada wapendwa, sisi wanawake wa Afrika tunabeba neema ya kipekee. Sisi ni mama wa mataifa, nguzo za Kanisa, walinzi wa utamaduni, na wajenzi wa mafungamoano ya udugu wa kibinadamu kwa dunia ya amani. Tunapotoka Uganda, turejee katika familia zetu tukiwa na nguvu mpya, huku tukiongozwa na Mama Bikira Maria, na tumejitoa kupanda mbegu za amani, kukuza upendo, na kueneza tumaini katika kila pembe ya bara letu. Sala zetu zipae kama uvumba, Ushuhuda wetu ung’ae kama jua, Na dhamira yetu idumu kama upendo wa Mungu. Sisi ni Wanawake Wakatoliki. Sisi ni Wanawake wa Imani. Sisi ni Mbegu za Amani na Tumaini. Asanteni sana kwa kunisikiliza. Mungu ibariki Afrika.

Wanawake Wakatoliki Namgongo
30 Julai 2025, 15:47