ĐÓMAPµĽş˝

Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mt. Theresia wa Mtoto Yesu, linaadhimisha Jubilei ya Miaka Mia moja tangu kuanzishwa kwa Karmeli ya Kimisionari ya Mama Krochifisa na Miaka 100 ya Utakatifu wa Theresia wa Mtoto Yesu Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mt. Theresia wa Mtoto Yesu, linaadhimisha Jubilei ya Miaka Mia moja tangu kuanzishwa kwa Karmeli ya Kimisionari ya Mama Krochifisa na Miaka 100 ya Utakatifu wa Theresia wa Mtoto Yesu 

Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mt. Theresia wa Mtoto Yesu: Mahujaji wa Utakatifu

Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, linaadhimisha Jubilei ya Miaka Mia moja tangu kuanzishwa kwa Karmeli ya Kimisionari ya Mama Krochifissa na Padre Lorenzo sanjari na kutangazwa kwa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu kuwa ni Mtakatifu kwa kuongozwa na kauli mbiu: "Mahujaji wa matumaini kuelekea utakatifu wa maisha." Hii ni changamoto kwa wanashirika kujikita katika kutafuta utakatifu wa maisha, wito wa wote!

Na Sr M. Lilian Kapongo, Mama Mkuu wa Shirika duniani, Roma, Italia.

Taifa la Mungu Tumsifu Yesu Kristo ”Roho wa Bwana yu juu yangu, kwani ameniweka wakfu niwaletee maskini Habari Njema. Amenituma kutangaza mwaka wa neema ya Bwana” (Lk 4: 18-19.) Katika Muktadha ya Maadhimisho ya Jubilei kuu ya miaka 2025 ya Ukristo, kwa moyo wa shukrani ninayofuraha kubwa kuwashirikisha Neema Maalum tuliyonayo kama Shirika la kitawa, linalotimiza karne moja tangu kuzaliwa kwake, hivyo kusherehekea Jubilei ya miaka mia moja ya maisha na utume wake katika Kanisa na ulimwengu kwa ujumla. Mwanzo wa Shirika na uwepo wake duniani: Familia yetu ya kitawa inatambulika rasmi katika Kanisa kama Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Kwa sasa lipo katika nchi kumi na mbili duniani kama ifuatavyo: bara la Ulaya tupo Italia, Malta na Romania, Amerika ya kusini tupo nchini Brazili, Amerika ya kaskazini tupo nchini Canada. Barani Afrika tupo Tanzania Bara na visiwani, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Katika Bara la Asia tupo Ufilipin, Vietnam na Indonesia. Shirika hili lilianzishwa tarehe 3 Julai mwaka 1925 katika mji wa Santa Marinella -Roma Italia, na Mwenyeheri Mama Maria Krochifissa Kurcio pamoja na Padri Lorenzo van den Eerenbeemt ambaye alikuwa Mtawa Mkarmeli (O.Carm).

Wakarmeli wanaotekeleza utume wao Jimbo kuu la Dar es Salaam
Wakarmeli wanaotekeleza utume wao Jimbo kuu la Dar es Salaam

Baada ya safari ya mwaka mmoja ya kubadilishana mawazo kati yao kwa njia ya barua na hatimaye kufahamiana, waanzilishi hawa wawili waliweza kuuganisha nia na jitihada zao. Kwa kujikita katika tasaufi ya ukarmeli, lengo kuu la Shirika jipya likawa ni kuishi maisha ya kimisionari ili kuzipeleka roho za watu kwa Mungu, kutoa elimu na malezi hasa kwa watoto na vijana wenye uhitaji zaidi. Chimbuko la roho yao ya kimisionari lilitokana na upendo walokuwa nao kwa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, mtawa wa mkarmeli, Mwalimu wa Kanisa na Msimamizi wa Misioni zote. Walipenda kuishi njia yake ndogo ya Upendo na kujiaminisha kabisa kwa Mungu kama mtoto mchanga anavyojiachilia mikononi mwa mama au baba yake.  Moja ya hamu kubwa alizokuwa nazo mtakatifu Theresia ilikuwa ni kwenda duniani kote ili kumfanya Yesu ajulikane na kupendwa na watu wote, kama tunavyoweza kusoma katika maandiko yake mweneyewe.” Lo! licha ya udogo wangu, ningependa kuziangazia roho  za watu, kama vile walivyofanya manabii na waalimu wa Kanisa. Nasikia ninao wito wa kuwa Mtume. Nami ningependa kusafiri duniani kote, nikalihubiri jina lako, na kuusimika msalaba wako mtukufu katika nchi za wapagani. Lakini, Ee Mpenzi wangu, misheni moja tu, hainganiridhisha mimi; kwani, ningependa kuihubiri habari njema katika kontinenti zote tano, kwa wakati uleule na hata katika visiwa vya mbali kabisa. Isitoshe ningependa kuwa mmisionari, sio tu kwa miaka michache, bali tangu kuumbwa kwa ulimwengu “ Naam mpaka mwisho wa nyakati...”

Mahujaji wa matumaini kuelekea utakatifu wa maisha
Mahujaji wa matumaini kuelekea utakatifu wa maisha

Padri Lorenzo katika barua yake ya kwanza kwa Mama Krochifissa aliandika: ”kiwa nasikia msukumo kwa ajili ya Taasisi hii mpya, ni kwa sababu mtakatifu Teresa na Theresia mdogo walikuwa na hamu kubwa ya kumtumikia Mungu katika misioni na hasa kwa sababu, katika nchi za misioni kunahitajika kweli mioyo mitakatifu. (…) kazi hii takatifu inapaswa kuenea duniani kote na kuwafikia watu wote (…)” Mama Krochifissa kwa upande wake alijibu ”Wewe, Mheshimiwa Padri, ni kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa unaandika na kumuomba Mungu ili Kazi hii takatifu iweze kufika duniani kote, lakini mimi ni tangu utoto wangu nimekuwa nikiota juu ya wazo hili kubwa.” Maadhimisho ya Jubilei ya miaka mia moja ya kuanzishwa Shirika na kutangazwa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Kadiri ya Maadiko Matakatifu Jubilei ni mwaka maalum wa neema, mwaka Mtakatifu na wa kujitakatifuza, mwaka wa Huruma, toba, msamaha, upatanisho na ukombozi kutoka aina zote za utumwa, hivyo ni mwaka wa Furaha. (Law 25: 8-17; Isa 61: 1-2; Luka 4: 18-19.) Shirika letu kama tulivyoona hapo juu, lilianza rasmi tarehe 3 Julai 1925 mara baada ya Mtakatifu Theresia kutangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 17 Mei 1925. Tukio hili lilikuwa na umuhimu wa pekee kwa Waanzilishi wa Familia yetu ya kitawa ambao tangu mwanzo kabisa wa Wazo hili walijiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Theresia. Ndiyo, ilikuwa katika siku hiyo maalum, ambapo Waanzilishi wetu, walimuomba Mungu kupitia maombezi yake ili Wazo lao la kuanzisha Shirika jipya la Karmeli ya Kimisionari liweze kuwa uhalisia baada ya kupitia mahangaiko mengi yenye kukatisha tamaa na kuvunja moyo.

Kumpenda Kristo Yesu na kumfanya apendwe kwa kupyaisha ubinadamu wao
Kumpenda Kristo Yesu na kumfanya apendwe kwa kupyaisha ubinadamu wao

Mwanzilishi wetu Padri Lorenzo aliandika hivi juu ya kuanza kwa Shirika: ”Mtakatifu Theresia, mtakatifu wa Misioni, (…) ni yeye ambaye katika mwaka wa kutangazwa kwake kuwa mtakatifu aliongoza kikundi kidogo kutoka Modika na kutoka Roma, hadi Santa Marinella katika njia za ajabu na za Rehema ya Mungu.” Kutoka katika maandiko haya ya waanzilishi, tunaelewa sababu za kwa nini Mtakatifu Theresia wa Lisieux ni wa muhimu sana kwa Shirika letu, hivyo kuuanganisha Jubilei yake ya miaka mia moja tangu kutangazwa Mtakatifu na Jubilei ya miaka mia moja tangu kuanzishwa kwa Shirika. Theresia wa Mtoto Yesu, kwa hakika, ni mtakatifu anayependwa na kufuatwa na watu wengi, kwa usahili maisha yake ya Kiinjili na mafundisho ya njia ndogo ya upendo, uaminifu na kujiachilia kabisa katika Moyo wa Mungu uliojaa Upendo na Huruma.

Wote wanaitwa kuchuchumalia utakatifu wa maisha
Wote wanaitwa kuchuchumalia utakatifu wa maisha   (Vatican Media)

Sote tumeitwa katika utakatifu, ni wito wa kila Mkristo kama Baba Mtakatifu Francisko alivyotukumbusha katika Waraka wake wa Kitume "Gaudete et exsultate" juu ya wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo." "Anataka tuwe watakatifu na hatarajii tutosheke na maisha ya hivi hivi tu, yasiyo na maji na yasiyo aminifu.” (GE n.1). Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Watakatifu wanatutia moyo na kutusindikiza”, na wale ambao tayari wamefikia uwepo wa Mungu wanadumisha vifungo vya upendo na ushirika pamoja nasi. Mwaka huu pia, tarehe 13 Novemba, tutakuwa na kumbukizi ya miaka ishirini tangu mwanzilishi wetu Mama Krochifissa atangazwe kuwa Mwenyeheri. Kwa hivyo Jubilei hii ya Shirika kwetu sisi na kwa Taifa zima la Mungu ni kichocheo cha kuishi na kuimarika katika wito wetu msingi wa “kuwa watakatifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu”. Tunataka kupyaisha maisha yetu ya kiroho, mahusiano yetu ya kindugu na wito wetu wa kimisionari, kwa mfano na mafundisho ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu na waanzilishi Mwenyeheri Mama Krochifissa na Padri Lorenzo.

Fadhili za Bwana nitaziimba milele, nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wa Mungu
Fadhili za Bwana nitaziimba milele, nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wa Mungu

Katika changamoto za ulimwengu wetu wa leo ambapo tunapatwa na kukandamizwa na hofu ya udhaifu wetu, Mtakatifu Theresia wa Lisieux anatuhimiza kuwa na Tumaini, kujiaminisha kabisa kwa Mungu aliyejaa Upendo na Huruma. Katika utamaduni wa chuki na ubinafsi, wanatuelekeza kwenye upendo, wema na amani. Mada kuu ya Jubilei, malengo na utekelezaji wake: Kwa mwanga wa Maandiko matakatifu, wa Jubilei kuu ya Kanisa kiulimwengu, Jubilei yetu ya Shirika inaongozwa na kuhamasishwa na mada kuu ifuatayo: ”Kumpenda  Yesu  na  kumfanya  Apendwe  kwa  Kukarabati Ubinadamu  Uliojeruhiwa: Mahujaji wa matumaini kuelekea Utakatifu», ĘşFadhili  za Bwana nitaziimba milele, kwa kinywa changu, nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.” (Zab 89:2). Lengo kuu likiwa ni: Kusoma na kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa ari ya kimisionari na kisinodi, kuangalia yajayo kwa tumaini la kinabii. Ili kutekeleza malengo haya tumefanya safari ya miaka mitatu ya maandalizi ambapo mwaka wa kwanza tuliutolea kwa Mtakatifu Theresia ili kusoma na kutafakari nafasi yake katika maisha ya Waanzilishi na ya Shirika kwa ujumla, mwaka wa pili tuliutolea kwa Waanzilshi ili kusoma na kutafakari maandiko yao juu ya maongozi ya Roho mtakatifu na Karama maalum ya Shirika kwa ujumla. Katika Mwaka wa tatu, mwaka wa Jubilei yenyewe, tunaendelea kutafakari jinsi ya kuistawisha Karama ya Shirika katika ulimwengu wetu wa leo. Yote haya yameongozwa na kuhamishwa na Sala, ushirikishanaji wa fumbo la wito wa kila mwanashirika, mang’amuzi ya kimisionari, utunzi wa nyimbo, michezo mbalimbali, uandishi wa vitabu na makala mbali mbali juu ya Historia ya Shirika, Waanzilishi, Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, nk.

Kupyaisha ubinadamu uliojeruhiwa!
Kupyaisha ubinadamu uliojeruhiwa!

Kuanzia tarehe 24 Juni, tumeanza Novena maalum ya kumshukuru Mungu na kujiandaa kwa ufunguzi rasmi wa mwaka wa Jubilei hii ya Shirika utakao fanyika tarehe 5 Julai 2025 kwa adhimisho la Ekaristi Takatifu litakoloongozwa na Askofu wa Jimbo letu la ”Porto e Santa Rufina” Mhashamu Askofu Gianrico Ruzza. Tarehe 3 Julai 2025 kumbukizi ya maika 100 tangu kuanza kwa Jumuiya ya kwanza ya Shirika, tutakuwa na Misa ya Shukrani itakayoongozwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu na tarehe 4 Julai 2025 Sikukuu ya mwenyeheri Mama Krochifissa Kurchio mwanzilshi wa Shrika, tutakuwa na adhimsho la Misa Takatifu itakayoongzwa na Baba Askofu Filippo Iannone, mkarmeli (O.Carm). Tukitambua matunda mengi katika nyakati mbalimbali za maisha na utume wa Shirika, mchango wa watu wengi, viongozi wa kiroho na wa kiserikali, wafadhili mbalimbali Wote tunakaribishwa kumwimbia Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa Matendo makuu aliyotutendea sisi pamoja na watu wengi duniani waliofikiwa na huduma zetu za kiroho, kimwili na za kijamii kwa njia mbalimbali. TUMSIFU YESU KRISTO.

Vyombo na mashuhuda wa upendo, wema na amani
Vyombo na mashuhuda wa upendo, wema na amani   (s. Lidija Vuksanović)

Ni mimi Sr M. Lilian Kapongo, Mama Mkuu wa Shirika duniani.

Wakarmeli Jubilei

 

02 Julai 2025, 17:13