MAP

Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, tarehe 16 Julai 2025 imeadhimishwa kwa uzito mkubwa. Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, tarehe 16 Julai 2025 imeadhimishwa kwa uzito mkubwa. 

Bikira Maria wa Karmeli, Miaka 100 ya Mt. Theresa wa Mtoto Yesu na Miaka 100 ya Shirika!

Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, tarehe 16 Julai 2025 imeadhimishwa kwa uzito mkubwa kama kilele cha kumbukumbu ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, O.C.D., alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu. Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, hapo tarehe 3 Julai 1925. Mahujaji wa Matumaini Kuelekea Utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Bikira Maria wa Mlima Karmeli ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazofumbatwa katika: maisha ya sala endelevu na dumifu; katika hali ya kimya kikuu na tafakari ya kina. Ni mfano bora wa kuigwa katika mchakato wa kufunga, kujinyima na kujisadaka kwa ajili ya jirani na umuhimu wa kudumisha ufukara kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani! Huu ni ufalme wa kweli na uzima, ufalme wa utakatifu na wa neema, ufalme wa haki, mapendo na amani. Kumbukumbu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, tarehe 16 Julai 2025 imeadhimishwa kwa uzito mkubwa kama sehjeemu mwendelezo wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, O.C.D., alipotangazwa kuwa ni Mtakatifu sanjari na Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, hapo tarehe 3 Julai 1925. Kilele cha maadhimisho ya Jubilei hii ni hapo tarehe 3 Julai 2026.

Kilele cha Jubilei ni hapo tarehe 3 Julai 2026
Kilele cha Jubilei ni hapo tarehe 3 Julai 2026

Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu na wa Uso Mtakatifu, O.C.D., Jina lake la kitawa ni Thérèse Françoise Marie Martin, maarufu pia kama Theresa wa Lisieux. Anaheshimiwa na Mama Kanisa kama Bikira na Mwalimu wa Kanisa aliyetangazwa na Papa Pio XI kuwa Mtakatifu tarehe 17 Mei 1925. Hata katika udogo wake Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alijitokeza kama mtaalam wa elimu ya upendo inayosimikwa katika unyofu wa hali ya juu na jinsi ambavyo kwa neema alivyoelewa na kutekeleza Injili ya Kristo Yesu katika maisha yake ndani ya monasteri ya Wakarmeli Peku. Mtakatifu Theresa alitamani sana kuwa mmisionari ili kuokoa roho za watu wengi. Alitamani awe mhubiri, mmisionari na shuhuda. Hata hivyo ilikuwa tu baada ya yeye kujitoa mwenyewe na kujikabidhi kwa upendo wenye huruma ndipo alipogundua wito ambao Mungu alimwitia. Katika mahubiri yake, tarehe 17 Mei 2025, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican alisema, Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu alikuwa ni mmisionari hodari kwa njia ya maisha ya sala, akakita maisha yake katika tunu msingi za Kiinjili.

Kardinali Tagle akiadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Shirika la Wakarmeli
Kardinali Tagle akiadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya Shirika la Wakarmeli

Kwa upande wake Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Shirika, alikazia umuhimu wa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya uaminifu kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao, ili kumfuasa Kristo Yesu aliye: njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya Kristo Yesu. Rej. Yn 14:6. Hii ni changamoto ya kujikita katika fadhila ya unyenyekevu, na hivyo kujiachilia mikononi mwa Kristo Yesu ili aweze kuwaongoza katika maisha yao yote, katika imani na mahusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu katika Sala, Neno na Sakramenti za Kanisa, ili kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kuendelea kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu wanaoteseka. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Toma, Mtume, hata Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu wanaitwa na kutumwa kuwa ni wafuasi na mitume wa Kristo Yesu katika medani mbalimbali za maisha na utume wao, hasa huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Shirika lilianzishwa tarehe 3 Julai 1925
Shirika lilianzishwa tarehe 3 Julai 1925

Kwa upande wake Askofu mkuu Filipo Iannone Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Tafsiri ya Sheria kanuni za Kanisa, katika maadhimisho ya Sikukuu ya Mwenyeheri Mama Maria Krochifissa Kurcio, anasema; kwa hakika alikuwa ni mwanamke wa kawaida, aliyekita maisha yake katika Injili ya upendo, Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kama mambo msingi ya kumsaidia kufikia upendo kwa Kristo Yesu na hatimaye, utakatifu wa maisha. Kumbe, watawa wake hawana budi kujibidiisha kumfahamu Kristo Yesu, Kumfuasa na hatimaye, kujenga mahusiano na mafungamano ya dhati na hasa katika Sakramenti ya Ekaristi Takatifu. Kama kilele cha matukio yote haya, Padre Benny Phang Khong Wing, O. Carm. Makamu mkuu wa Shirika la Wakarmeli Ulimwenguni, katika mahubiri yake, kwenye Sikukuu ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli na mwendelezo wa  wa maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu tawi la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu lilipounganishwa na Familia ya Karmeli Ulimwenguni, Jumatano tarehe 16 Julai 2025, amekita mahubiri yake kama shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa maisha ya watawa Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, waliopyaisha maisha yao kwa kumfuata Bikira Maria wa Mlima Karmeli kwa njia ya sala, mapambano ya maisha ya kiroho. Huu ni wito unaowasukuma watawa kuendelea kupyaisha maisha yao, kama walivyofanya wale wafuasi wa kwanza wa Shirika hili.

Sr. Maria Lilian Kapongo
Sr. Maria Lilian Kapongo

Wakati huo huo, Mheshimiwa Sr. Maria Lilian Kapongo, Mama mkuu wa Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Therisia wa Mtoto Yesu anasema: Familia yetu ya kitawa inatambulika rasmi katika Kanisa kama Shirika la Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Shirika hili lilianzishwa tarehe 3 Julai mwaka 1925 katika mji wa Santa Marinella-Roma Italia, na Mwenyeheri Mama Maria Krochifissa Kurcio pamoja na Padre Lorenzo van den Eerenbeemt ambaye alikuwa Mtawa Mkarmeli (O.Carm). Baada ya safari ya mwaka mmoja ya kubadilishana mawazo kati yao kwa njia ya barua na hatimaye kufahamiana, waanzilishi hawa wawili waliweza kuuganisha nia na jitihada zao. Kwa kujikita katika tasaufi ya ukarmeli, lengo kuu la Shirika jipya likawa ni kuishi maisha ya kimisionari ili kuzipeleka roho za watu kwa Mungu, kutoa elimu na malezi hasa kwa watoto na vijana wenye uhitaji zaidi. Chimbuko la roho yao ya kimisionari lilitokana na upendo walokuwa nao kwa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, mtawa wa mkarmeli, Mwalimu wa Kanisa na Msimamizi wa Misioni zote. Walipenda kuishi njia yake ndogo ya Upendo na kujiaminisha kabisa kwa Mungu kama mtoto mchanga anavyojiachilia mikononi mwa mama au baba yake.  Moja ya hamu kubwa alizokuwa nazo mtakatifu Theresia ilikuwa ni kwenda duniani kote ili kumfanya Yesu ajulikane na kupendwa na watu wote, kama tunavyoweza kusoma katika maandiko yake mweneyewe.” Lo! licha ya udogo wangu, ningependa kuziangazia roho za watu, kama vile walivyofanya manabii na waalimu wa Kanisa. Nasikia ninao wito wa kuwa Mtume. Nami ningependa kusafiri duniani kote, nikalihubiri jina lako, na kuusimika msalaba wako mtukufu katika nchi za wapagani. Lakini, Ee Mpenzi wangu, misheni moja tu, hainganiridhisha mimi; kwani, ningependa kuihubiri habari njema katika Mabara yote matano, kwa wakati uleule na hata katika visiwa vya mbali kabisa. Isitoshe ningependa kuwa mmisionari, sio tu kwa miaka michache, bali tangu kuumbwa kwa ulimwengu “Naam mpaka mwisho wa nyakati...”

Kumbukumbu angavu na endelevu
Kumbukumbu angavu na endelevu

Padre Lorenzo katika barua yake ya kwanza kwa Mama Krochifissa aliandika: “kiwa nasikia msukumo kwa ajili ya Taasisi hii mpya, ni kwa sababu Mtakatifu Theresa na Theresia mdogo walikuwa na hamu kubwa ya kumtumikia Mungu katika misioni na hasa kwa sababu, katika nchi za misioni kunahitajika kweli mioyo mitakatifu. (…) kazi hii takatifu inapaswa kuenea duniani kote na kuwafikia watu wote (…)” Mama Krochifissa kwa upande wake alijibu “Wewe, Mheshimiwa Padre, ni kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa unaandika na kumuomba Mungu ili Kazi hii takatifu iweze kufika duniani kote, lakini mimi ni tangu utoto wangu nimekuwa nikiota juu ya wazo hili kubwa.” Maadhimisho ya Jubilei ya miaka mia moja ya kuanzishwa Shirika na kutangazwa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu. Kadiri ya Maadiko Matakatifu, Jubilei ni mwaka maalum wa neema, mwaka Mtakatifu na wa kujitakatifuza, mwaka wa Huruma, toba, msamaha, upatanisho na ukombozi kutoka aina zote za utumwa, hivyo ni mwaka wa Furaha. (Law 25: 8-17; Isa 61: 1-2; Luka 4: 18-19.) Shirika letu kama tulivyoona hapo juu, lilianza rasmi tarehe 3 Julai 1925 mara baada ya Mtakatifu Theresia kutangazwa kuwa Mtakatifu tarehe 17 Mei 1925. Tukio hili lilikuwa na umuhimu wa pekee kwa Waanzilishi wa Familia yetu ya kitawa ambao tangu mwanzo kabisa wa Wazo hili walijiweka chini ya ulinzi na usimamizi wa Mtakatifu Theresia. Ndiyo, ilikuwa katika siku hiyo maalum, ambapo Waanzilishi wetu, walimuomba Mungu kupitia maombezi yake ili Wazo lao la kuanzisha Shirika jipya la Karmeli ya Kimisionari liweze kuwa uhalisia baada ya kupitia mahangaiko mengi yenye kukatisha tamaa na kuvunja moyo.

Masista Wakarmeli Jimbo kuu la Dar es Salaam
Masista Wakarmeli Jimbo kuu la Dar es Salaam

Mwanzilishi wetu Padri Lorenzo aliandika hivi juu ya kuanza kwa Shirika: “Mtakatifu Theresia, mtakatifu wa Misioni, (…) ni yeye ambaye katika mwaka wa kutangazwa kwake kuwa mtakatifu aliongoza kikundi kidogo kutoka Modika na kutoka Roma, hadi “Santa Marinella” katika njia za ajabu na za rehema ya Mungu.” Kutoka katika maandiko haya ya waanzilishi, tunaelewa sababu za kwa nini Mtakatifu Theresia wa Lisieux ni wa muhimu sana kwa Shirika letu, hivyo kuuanganisha Jubilei yake ya miaka mia moja tangu kutangazwa Mtakatifu na Jubilei ya miaka mia moja tangu kuanzishwa kwa Shirika. Theresia wa Mtoto Yesu, kwa hakika, ni mtakatifu anayependwa na kufuatwa na watu wengi, kwa usahili maisha yake ya Kiinjili na mafundisho ya njia ndogo ya upendo, uaminifu na kujiachilia kabisa katika Moyo wa Mungu uliojaa Upendo na Huruma. Sote tumeitwa katika utakatifu, ni wito wa kila Mkristo kama Baba Mtakatifu Francisko alivyotukumbusha katika Waraka wake wa Kitume "Gaudete et exsultate" juu ya wito wa utakatifu katika ulimwengu mamboleo." "Anataka tuwe watakatifu na hatarajii tutosheke na maisha ya hivi hivi tu, yasiyo na maji na yasiyo aminifu.” (GE n.1). Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema, “Watakatifu wanatutia moyo na kutusindikiza”, na wale ambao tayari wamefikia uwepo wa Mungu wanadumisha vifungo vya upendo na ushirika pamoja nasi. Mwaka huu pia, tarehe 13 Novemba, tutakuwa na kumbukizi ya miaka ishirini tangu mwanzilishi wetu Mama Krochifissa atangazwe kuwa Mwenyeheri. Kwa hivyo Jubilei hii ya Shirika kwetu sisi na kwa Taifa zima la Mungu ni kichocheo cha kuishi na kuimarika katika wito wetu msingi wa “kuwa watakatifu kama Baba yetu wa mbinguni alivyo mtakatifu”. Tunataka kupyaisha maisha yetu ya kiroho, mahusiano yetu ya kindugu na wito wetu wa kimisionari, kwa mfano na mafundisho ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu na waanzilishi Mwenyeheri Mama Krochifissa na Padri Lorenzo.

Watawa na Walelewa wakiwa kwenye picha ya pamoja
Watawa na Walelewa wakiwa kwenye picha ya pamoja

Katika changamoto za ulimwengu wetu wa leo ambapo tunapatwa na kukandamizwa na hofu ya udhaifu wetu, Mtakatifu Theresia wa Lisieux anatuhimiza kuwa na tumaini, kujiaminisha kabisa kwa Mungu aliyejaa Upendo na Huruma. Katika utamaduni wa chuki na ubinafsi, wanatuelekeza kwenye upendo, wema na amani. Mada kuu ya Jubilei, malengo na utekelezaji wake: Kwa mwanga wa Maandiko matakatifu, wa Jubilei kuu ya Kanisa kiulimwengu, Jubilei yetu ya Shirika inaongozwa na kuhamasishwa na mada kuu ifuatayo: “Kumpenda Yesu na kumfanya Apendwe kwa Kukarabati Ubinadamu Uliojeruhiwa: Mahujaji wa matumaini kuelekea Utakatifu,”,ʺFadhili za Bwana nitaziimba milele, kwa kinywa changu, nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.” (Zab 89:2). Lengo kuu likiwa ni: Kusoma na kutafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa ari ya kimisionari na kisinodi, kuangalia yajayo kwa tumaini la kinabii. Ili kutekeleza malengo haya tumefanya safari ya miaka mitatu ya maandalizi ambapo mwaka wa kwanza tuliutolea kwa Mtakatifu Theresia ili kusoma na kutafakari nafasi yake katika maisha ya Waanzilishi na ya Shirika kwa ujumla, mwaka wa pili tuliutolea kwa Waanzilshi ili kusoma na kutafakari maandiko yao juu ya maongozi ya Roho mtakatifu na Karama maalum ya Shirika kwa ujumla. Katika Mwaka wa tatu, mwaka wa Jubilei yenyewe, tunaendelea kutafakari jinsi ya kuistawisha Karama ya Shirika katika ulimwengu wetu wa leo. Yote haya yameongozwa na kuhamishwa na Sala, ushirikishanaji wa fumbo la wito wa kila mwanashirika, mang’amuzi ya kimisionari, utunzi wa nyimbo, michezo mbalimbali, uandishi wa vitabu na makala mbali mbali juu ya Historia ya Shirika, Waanzilishi, Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, nk.

Wakarmeli 2025
16 Julai 2025, 16:02