MAP

Ask.Mkuu Fisichella kwa vijana:imani ni kukutana,lakini wa kwanza kuja kwetu ni Yesu

Katika misa ya makaribisho ya vijana mahujaji kutoka Ulimwenguni kote katika Uwanja wa Mtakatifu Petro,tarehe 29 Julai 2025 kwa kuongozwa na Askofu Mkuu Fisichella,alijikita kuelezea mapokezi ya Martha na Maria kwa Yesu:Yeye anakuja kwetu wakati anapotaka,kama apendavyo,kwa wakati uliowekwa na Yeye na sio sisi tunavyotaka.Tunaitwa kujibu tu.Mwisho wa Misa Papa Leo XIV alifika uwanjani na kuwazungukia wote na kutoa salamu akiwakaribisha Torvergata.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Wakati wa ufunguzi rasimi wa Jubilei ya Vijana, waliounganika katika Maadhimisho ya Misa Takatifu katika Uwanja wa Mtakatifu Petro mjini Vatican, jioni tarehe 29 Julai 2025, iliyoongozwa na Askofu Mkuu Rino Fisichella , Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la  Uinjilishaji, mhusika wa maandalizi ya Jubilei  akishirikiana miongoni mwa wengine, na  Makardinali Baldo Reina, Mkuu wa Jimbo kuu la Roma, yaani makamu wa Papa na Kardinali Marc Ouellet.  Kwa hiyo kwenye utangulizi Askofu Mkuu Fisichella  aliwakaribisha kwa niaba ya Papa Leo XIV na kujitambulisha. Askofu Mkuu Fisichella alisema kwa lugha mbali mbali kwamba: “Tumewangoja kuwasili kwenu kwa muda mrefu, na sasa mko hapa. Asante kwa kuitikia mwaliko wa Papa wa kushiriki katika Jubilei hii, iliyowekwa kwenu na kwa matumaini ambayo kila mtu anahusika nayo. Mmetoka pande zote za dunia. Miongoni mwenu kuna baadhi ya marafiki wanaotoka katika maeneo yenye vita, na hivyo ninaomba kuwakumbatia  kidugu kunakotuunganisha kama chombo kimoja kuwafikia wale kutoka Ukraine na Palestina, kwa kuhakikisha kuwaonesha ishara ya urafiki wenu."

Misa ya Makaribisho ya vijana katika Uwanja wa Mtakatifu Petro
Misa ya Makaribisho ya vijana katika Uwanja wa Mtakatifu Petro   (@Vatican Media)

Askofu Mkuu Fisichella aliendelea: “wengi miongoni mwenu mmejitoa sadaka sana ili kuwa hapa Roma. Bwana hatawakatisha tamaa. Anakuja kukutana nanyi, muendelea kuwa macho ili muweze kutambua uwepo wake. Kuishi siku hizi kwa furaha na kiroho, ili kugundua urafiki mpya. Zaidi ya yote, tafakarini Roma na kazi zake nyingi za sanaa, maonesho ya imani ambayo yamechochea uzuri mwingi. Tuko hapa kukabidhi imani na kuelewa thamani kuu ambayo Yesu Kristo analeta katika maisha yetu. Hebu tujibu kwa shauku katika siku hizi: Roma, pamoja na yote yanayowakilisha, yako mikononi mwenu.”

Misa ya makaribisho ya vijana wa Jubilei
Misa ya makaribisho ya vijana wa Jubilei   (@Vatican Media)

Askofu Mkuu Fisichella kwa upande wa mahubiri yake akitafakari juu ya Injili ya Siku, ambapo Mama Kanisa amefanya siku kuu ya Mtakatifu Marta, alisema, “Vijana wapendwa, ni kwa wazo fupi la kushirikishana nanyi kifungu hiki kutoka katika Injili ya Mtakatifu Yohane,  ambayo tumesikia hivi punde. Inazungumza nasi kuhusu Martha, ambaye tunaadhimisha siku kuu yake ya kiliturujia leo hii. Martha, kwanza kabisa ni  ishara ya imani. Mwinjili anatuonesha hili kwa uwazi sana: anatuambia, kwanza kabisa, kuwa imani ni kukutana. Mkutano, hata hivyo, ambao hatuunzi. Katika kifungu kilichotangulia, Mwinjili Yohane anatuambia kwamba Martha na Maria walikuwa wamemwambia Yesu kwamba Lazaro ni mgonjwa. Naye Yesu alichelewesha ziara yake, akikaa siku chache zaidi kabla ya kuondoka. Inaweza kuonekana kuwa ya kushangaza: unapoambiwa mtu ni mgonjwa, jambo la kwanza unalofanya ni kuondoka mara moja. Yesu hakuwa na haraka. Yesu aliwaambia wanafunzi wangoje. Hii inatufundisha jambo muhimu: imani ni kukutana, lakini wa kwanza kuja kwetu ni Yesu.”

Misa ya mapokezi ya vijana wanahija
Misa ya mapokezi ya vijana wanahija   (@Vatican Media)

Askofu Mkuu aliendelea kusema: “anakuja kwetu wakati anapotaka, kama apendavyo, kwa wakati uliowekwa na Yeye, na sio  sisi tunavyotaka. Tunaitwa  kujibu tu. Mara  tunapoona tu kwamba anakuja kukutana nasi, sisi pia tunaitwa kwenda kwake. Maria anakimbia, hatembei; anahisi shauku kubwa ya kukutana na Bwana kiasi kwamba anakimbia kumwelekea. Hii ndiyo sababu Martha ni ishara ya imani yetu. Ishara kwamba Bwana anapotaka kukutana nasi, lazima atafute ndani yetu watu walio macho, walio tayari; tayari kukimbilia Kwake, bila kusita, kwa sababu ya imani, na hii ni tabia ya pili ambayo ni uchaguzi wa uhuru, uhuru ambao tunataka kufuata, kumfuata Bwana. Tunamfuata pale anapotaka kutuongoza. Tunamfuata ambapo ameweka furaha ya kweli kwa kila mmoja wetu. Ni uchaguzi wa uhuru ambao unaoneshwa pia katika mtazamo wa Martha na Maria.”

Misa ya makaribisho ya vijana wa Jubilei
Misa ya makaribisho ya vijana wa Jubilei   (@Vatican Media)

Askofu Mkuu alikazia zaidi kwamba walimwambia Yesu kuwa: “Lazaro ni mgonjwa!” hawakusema, "Njoo ufanye muujiza!" Hapana! Ni lazima Yesu aamue kile kinachofaa kufanya. Sio tu kwa wakati, lakini pia mbinu, njia ambazo Yeye huja kukutana nasi, kwa sababu ni lazima tuheshimu uhuru wa Mungu. Tuna wivu sana juu ya uhuru wetu, lakini ni lazima tujue kwamba Mungu anapokuja kukutana nasi, ni lazima tuheshimu uhuru wake, uhuru wa Mungu asiyetuacha kamwe, Mungu ambaye hawezi kamwe kuwaacha wale anaowapenda. Na tunapendwa na Mungu. Hii ndiyo sababu hatutakuwa peke yetu kamwe, hatuwezi kuachwa kamwe, kwa sababu Yesu ni mwenzetu katika safari.

Misa ya Mapokezi ya vijana
Misa ya Mapokezi ya vijana   (@Vatican Media)

Askofu Mkuu aliendelea kusema kuwa  "tumfuateni  Bwana kweli. Tukumbuke kijana ambaye pia alitamani wokovu. Alikwenda kwa Yesu, lakini kila kitu kilikuwa kinamhusu yeye mwenyewe: "Nitapataje uzima wa milele?" Yesu anamjibu. Lakini anapotaka kufanya jambo zaidi, kulingana na uamuzi wake mwenyewe, hana uwezo tena wa ishara ya uhuru wa kweli; hawezi kujinyima, na kwa hiyo hawezi kufanya tendo la uhuru. Tunakuwa huru kweli kweli tunapotoa sadaka fulani, lakini hasa pale sadaka hii inapolenga kukutana na Bwana na kumfuata. Imani, pia inasikiliza. Mtume Paulo anatufundisha jambo hilo. Imani huja kwa kusikiliza. Marta alisikiliza yale ambayo Yesu alikuwa akimwambia na pia aliweza kufanya ungamo lake la imani: "Ninaamini kwamba Wewe ndiwe Kristo. Ninaamini katika Ufufuko kwa sababu Wewe ni  Yesu, Wewe ni Ufufuko na Uzima!" Hakuna mahali pengine popote ambapo tunaweza kupata furaha isipokuwa Kwake, maana ya maisha yetu isipokuwa Kwake.

Misa ya makaribisho ya vijana wa Jubilei
Misa ya makaribisho ya vijana wa Jubilei   (@Vatican Media)

Kwa upande mwingine, alipenda kuelezea zaidi kwamba sisi ni wajinga bila silaha tunapoamini; tunaweza kusema tu kwamba tunaamini wafu wamefufuliwa. Haya ndiyo tunayotangaza; kwa hilo sisi ni mashuhuda: kwamba ufufuko ni maisha mapya kwa kila mmoja wetu. Kwa njia hiyo msiogope kamwe kuwa mashuhuda wa Kristo mfufuka, kwa sababu hii ndiyo inatufanya kuwa waamini, Wakristo. Kristo amefufuka, nasi tumemwona; tunamwamini. Lakini ushuhuda huu pia unakuwa vitendo. Martha ni kielelezo cha mwanamke ambaye amefanya mambo mengi sana maishani mwake, hivi kwamba anastahili hata karipio la fadhili kutoka kwa Yesu: “Martha, Martha, unahangaika kwa ajili ya mambo mengi! Maria, aketiye hapa karibu nami, aisikiaye sauti yangu...  badala yake ndiye aliyechagua sehemu iliyo bora zaidi.” Lakini leo hii  Martha anatuambia kwamba imani inakuwa matendo, inakuwa ushuhuda halisi, inakuwa maisha! Maisha yanayotembea sawa sawa na mafundisho ya Yesu, kwa maneno aliyotuachia."

Misa ya makaribisho ya vijana wa Jubilei
Misa ya makaribisho ya vijana wa Jubilei   (@Vatican Media)

Ni lazima kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwapo wakati mtu anatuhitaji, wakati mtu ni mgonjwa, gerezani. Uwepo ili kurejesha utu wakati mtu hajavaa tena utu wake; wawe tayari kujitolea kumrejesha kila mtu aliyekosa haki msingi ya utu katika maisha yake; tunaitwa kutoa ujasiri, kutoa faraja, kutoa tabasamu kwa wale wote wanaolia. Heri ni ushuhuda ambao Bwana anatutaka tutoe kwa ulimwengu wa leo, kwa sababu hili ndilo tumaini linalotungoja. Anangoja kutoka kwetu tumaini ambalo ni hakika kwamba mafundisho Yake ni kweli kwa ajili yetu sote. Tunaishi katika wakati wa vurugu kubwa. Na jeuri, haliko katika maeneo ya vita tu. Vurugu ziko katika mitaa yetu, katika miji yetu, iko karibu nasi, katika shule zetu."

Misa ya makaribisho ya vijana wa jubilei
Misa ya makaribisho ya vijana wa jubilei   (@Vatican Media)

Ili kutoa uhakika wa tumaini, upendo daima hushinda, kwamba wema hushinda vurugu, na kwamba tunahitaji kuwa wapatanishi kila siku, katika urahisi wa maisha yetu. Tukijenga amani, dunia itakuwa na amani. Na kwa hivyo, katika hitimisho la wakati huu wa tafakari, tujitengenezee maneno ambayo Papa Leo alituambia Dominika  iliyopita kutokea katika dirisha lake, akitusalimia, ambayo inatungoja sisi sote Tor Vergata, Jumamosi na Jumapili. Papa alituambia: "Kukutana na Kristo, hii ndiyo sababu ninawangoja. Kukutana na Kristo na kuimarishwa naye katika imani na katika kujitolea kumfuata daima." Marta anatupa mfano halisi wa hii leo. Kila mmoja wetu na awe na uwezo wa kuimarisha imani yetu, ya kumfuata Bwana na ushuhuda unaostahili wa maisha. Na iwe hivyo.

Misa ya kukaribisha vijana Julai 30
29 Julai 2025, 20:58