MAP

Kamati Tendaji Halmashauri ya Walei Taifa, Tanzania: Roho Mtakatifu na Ujasiri wa Kutangaza Habari Njema (Rej. Mdo 4:23–31) Kamati Tendaji Halmashauri ya Walei Taifa, Tanzania: Roho Mtakatifu na Ujasiri wa Kutangaza Habari Njema (Rej. Mdo 4:23–31) 

TANZANIA: Ujumbe wa Pentekoste Kwa Mwaka 2025: Jubilei Kuu & Uchaguzi Mkuu

Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Roho Mtakatifu awashushie Mapaji yake na hivyo kuwasaidia waamini kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wawe wanyenyekevu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu; wamwombe mwanga na nguvu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ujumbe wa Pentekoste: Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025; Uchaguzi mkuu 2025: Ushuhuda wa: Ukuhani, Unabii na Ufalme!

Kamati Tendaji Halmashauri ya Walei Taifa, - Dar Es Salaam.

Roho Mtakatifu na Ujasiri wa Kutangaza Habari Njema. Rej. Mdo 4:23–31. Baada ya kifo cha Kristo Yesu Mitume na wafuasi waliingiwa hofu, walihofia wao pia kukamatwa na kusulubiwa kama alivyofanywa Yesu. Siku ya Pentekoste Roho Mtakatifu anawashukia kama ndimi za moto anawaimarisha kwa mapaji yake nao wanaondokana na hofu yao wanatoka nje na kuanza kumshuhudia Kristo Mfufuka na kuhubiri Injili. Ni kwa sababu hii Pentekoste huitwa pia siku ambapo Kanisa lililazaliwa. Hii ilikuwa ni siku ambapo kwa mara ya kwanza Mitume walianza kumhubiri Kristo. Katika Kanisa la Tanzania, Pentekoste ni Sherehe pia ya Halmashauri ya Walei. Hii ni Sherehe inayolenga kuamsha katika kundi hili kubwa la familia ya Mungu ari ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu katika mazingira yao ya kila siku. Waamini walei ni mhimili wa Kanisa kwani, wanaitwa kutekeleza: Ukuhani, Unabii na Ufalme wa Kristo Yesu katika maisha yao, kama sehemu ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Roho Mtakatifu awashushie Mapaji yake na hivyo kuwasaidia waamini kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu. Waamini wawe wanyenyekevu kwa nguvu ya Roho Mtakatifu; wamwombe mwanga na nguvu katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu
Waamini walei wanaitwa na kutumwa kuyatakatifuza malimwengu   (TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Ufuatao ni Ujumbe wa Sherehe ya Pentekoste kutoka katika Kamati Tendaji Halmashauri ya Walei Taifa, nchini Tanzania. Ndugu waamini wapendwa, Tunamshukuru Mungu aliye hai kwa neema ya kuadhimisha tena Sherehe ya Pentekoste, siku takatifu ambayo Kanisa lilijaliwa zawadi kuu ya Roho Mtakatifu, ambaye ni Mfariji (Yoh. 14:16), Mshauri wa kweli (Yoh. 16:13), na Chanzo cha nguvu ya utume wa Kikristo (Mdo 1:8). Pentekoste siyo tu kumbukumbu ya kihistoria, bali ni uzoefu hai wa Kanisa katika kila kizazi, tunapojazwa tena na Roho Mtakatifu ili kuishi na kutangaza Injili kwa ujasiri, upendo na hekima. Pentekoste ya mwaka 2025 inaadhimishwa katika mwanga wa Jubilei Kuu ya Kanisa Katoliki, chini ya kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini.” Jubilei ni kipindi cha neema na toba, cha kuanza upya na kutembea pamoja kama Kanisa katika safari ya Kisinodi na Kimisionari tukisikia, tukishirikiana, na tukiambatana katika Kristo, aliye Njia, Ukweli na Uzima (Yn 14:6). Katika dunia ya leo iliyojaa hofu, migawanyiko ya kijamii na kisiasa, mmomonyoko wa maadili, na kupungua kwa matumaini, sauti ya Roho Mtakatifu inatuita kwa nguvu mpya. Roho Mtakatifu Anatualika tuwe vyombo vya Injili ya matumaini, tukijitokeza si kwa fujo wala mabishano yasiyo ya Kikristo, bali kwa ujasiri wa kiinjili, ule unaojengwa juu ya ukweli, upendo na unyenyekevu (Rej. Ef 4:15).

Waamini wasiogope kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao
Waamini wasiogope kumfungulia Kristo Yesu malango ya maisha yao

Waamini wapendwa, kwa njia ya Ubatizo na Kipaimara, tumepakwa kwa Roho Mtakatifu na kushiriki daraja la Kristo kama: Makuhani, Manabii na Wafalme (Rej. KKK 1268, 1546). Hii ni dhima ya kila Mlei — si kwa Wachungaji peke yao — ya kueneza Injili kwa maneno na matendo, ndani ya familia, katika jumuiya ndogo ndogo za Kikristo (JNNK), vigango, parokia, majimbo hadi taifa zima. Pentekoste hii inaangukia katika mwaka muhimu kwa taifa letu mwaka wa uchaguzi mkuu. Hili ni tukio la kihistoria linalohitaji tafakari ya kiroho na mshikamano wa kitaifa. Tunaitwa na Roho Mtakatifu kuombea Tanzania ipate viongozi waadilifu na uchaguzi wa haki, amani na usawa. Tunapaswa kushiriki mchakato huu si kwa jazba au matusi, bali kwa maadili ya Kikristo: kwa kutetea ukweli kwa hekima, kuheshimu maoni ya wengine, na kuepuka lugha ya chuki. Tukirejea Matendo ya Mitume 4:23–31, tunaona Kanisa la mwanzo likikusanyika kwa sala wakati wa misukosuko ya kijamii na kisiasa. Kwa maombi yao, Roho Mtakatifu aliwajalia ujasiri wa kutangaza Injili bila hofu. Nasi pia, katika mazingira yetu ya leo, tunaitwa kuwa mashahidi wa Injili ya amani na upatanisho (Mathayo 5:9), tukiwa watu wa sala, busara, na uwajibikaji wa kijamii. Hii ni fursa ya kutafakari kwa dhati wito wetu wa Kikristo: Je, ni kwa namna gani familia zetu ni Shule ya Imani na Upendo? Je, JNNK zetu ni chemchemi ya mshikamano? Je, sisi ni vyombo vya matumaini, hasa kwa maskini, waliopuuzwa, na vijana wanaohangaika kutafuta maana ya maisha? Roho Mtakatifu anatuita kuamka kutoka usingizi wa kutojali au kukata tamaa. Anatutia nguvu ili tuwe manabii wa matumaini katika kizazi hiki, tukikemea uovu kwa hekima, tukilinda utu wa binadamu, na kushiriki katika maisha ya kijamii kwa misingi ya Injili.

Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi
Pentekoste ni mwaliko wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi

Waamini wapendwa, uchaguzi si tu tukio la kisiasa bali pia ni mtihani wa maadili ya kitaifa. Tutumie zawadi ya uhuru wa kidemokrasia kwa busara na kwa moyo wa ujenzi wa taifa. Tujiepushe na chuki, uchochezi, au ushabiki usiozingatia haki na kweli. Amani ni zawadi ya Mungu lakini pia ni matunda ya juhudi zetu (Rej. KKK 2304). Pentekoste hii, tukiwa mahujaji wa matumaini na katika matumaini, tuungane na Kanisa zima katika sala hii ya Mitume: “Bwana, utujalie sisi watumishi wako kulisema Neno lako kwa ujasiri wote” (Mdo 4:29). Tuwaombee viongozi wetu wa sasa na wa baadaye, vyombo vya uchaguzi, na wananchi wote ili uchaguzi wa mwaka huu uwe njia ya neema na si chanzo cha vurugu. Kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa, na kwa neema ya Roho Mtakatifu, Tanzania ibaki kuwa nchi ya amani, haki na upendo. Tunatamani kila mmoja aweze kusema kama Mtume Paulo: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda” (2 Tim 4:7.) Ni sisi, Watumishi wenu katika Kristo, Kamati Tendaji – Halmashauri ya Walei Taifa.

Ujumbe wa Pentekoste
05 Juni 2025, 15:40