Rais wa Lebanon Joseph Aoun Akutana na Papa Leo XIV Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 13 Juni 2025 alikutana na kuzungumza na Rais Joseph Aoun, wa Lebanon, baadaye alibahatika pia kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambata na Monsinyo Mirosław Stanisław Wachowski, Katibu mkuu msaidizi wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na mgeni wake katika mazungumzo yao, wamepongeza mahusiano mazuri ya kidiplomasia kati ya nchi hizi mbili sanjari na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Viongozi hawa wawili wameonesha matumaini yao kutokana na mchakato wa mageuzi yanayoendelea nchini Lebanon kwamba, yatawezesha Lebanon kukita mizizi yake katika msingi wa amani na utulivu wa kisiasa; sanjari na jitihada za kufufua uchumi, ili kukuza na kudumisha maendeleo. Wamezungumzia pia umuhimu wa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano huko Mashariki ya Kati.