MAP

Wamisionari wa Shirika ya Damu Azizi ya Yesu, Vyama vya Kitume pamoja na Familia ya Damu Azizi ya Yesu, wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Wamisionari wa Shirika ya Damu Azizi ya Yesu, Vyama vya Kitume pamoja na Familia ya Damu Azizi ya Yesu, wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. 

Mahujaji wa Matumaini Katika Damu Azizi ya Yesu, Uhai na Wokovu wa Ulimwengu!

Wamisionari wa Shirika ya Damu Azizi ya Yesu, Vyama vya Kitume pamoja na Familia ya Damu Azizi ya Yesu, wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa matumaini katika Damu Azizi ya Yesu, uhai na wokovu wa ulimwengu.” Maadhimisho haya yameanza, Jumatatu tarehe 30 Juni 2025 kwa Mkesha wa kimataifa wa sala ukiongozwa na Kardinali Baldassare Reina na kilele chake ni tarehe Mosi Julai 2025 kwa Ibada ya Misa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo yanayonogeshwa na kauli mbiu: Mahujaji wa matumaini “Peregrinantes in spem” ni muda muafaka wa kupyaisha imani, matumaini na mapendo thabiti, kwa kuishi kama ndugu wamoja, sanjari na kusikiliza pamoja na kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha Maskini. Ni muda wa toba na wongofu wa ndani na wa kiikolojia, tayari kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Ni muda muafaka kwa waamini kujikita katika kutangaza na kushuhudia imani na matumaini yanayomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kukazia umoja na utofauti wa wateule watakatifu wa Mungu. Jubilei ni muda uliokubalika na Mwenyezi Mungu wa kuhakikisha kwamba, waamini wanajitahidi kumwilisha karama na mapaji yao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Lengo ni kutangaza na kushuhudia imani na furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa.

Mahujaji wa Matumaini Katika Damu Azizi ya Yesu, Uhai na Wokovu wa Ulimwengu
Mahujaji wa Matumaini Katika Damu Azizi ya Yesu, Uhai na Wokovu wa Ulimwengu

Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu; kwa kuweka kando mizigo ya zamani, na kupyaisha msukumo kuelelea siku zijazo; ili kusherehekea uwezekano wa mabadiliko katika maisha, kwa kujitahidi kupyaisha utambulisho wa waamini na kuwa jinsi walivyo, kwa njia ya imani, tayari kushuhudia ubora wao katika maisha ya kila siku. Huu ni mwaliko kwa Wakristo wote kuwa ni mahujaji wa matumaini yasiyo danganya; umoja unaopaswa kuimarishwa; kukuza na kujenga haki, amani na furaha ya kweli katika Kristo Yesu. Kristo Yesu ndiye Lango la maisha ya uzima wa milele, anayewashirikisha waja wake Fumbo la upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na mipaka; huruma inayowakumbatia binadamu wote pasi na ubaguzi, changamoto na mwaliko wa kuambata toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha. Kristo Yesu ni mlango unawaohamasisha waamini kujikita katika upendo kwa Mungu na jirani kwa kuambata Injili ya furaha, daima wakimwangalia Kristo Yesu waliyemtoboa kwa mkuki ubavuni, kimbilio la wakosefu na wadhambi; watu wanaohitaji msamaha, amani na utulivu wa ndani. Kristo Yesu ni mlango wa huruma na faraja, wema na uzuri usiokuwa na kifani. Huu ndio mlango wanamopita watu wenye haki. Kristo Yesu ni mlango wa mbingu, unaowaalika wote kushiriki furaha ya uzima wa milele. Yesu anawasubiri kwa moyo wa huruma na mapendo, wale wote wanaomwendea kwa toba na wongofu wa ndani.

Maadhimisho ya Jublei ya Mwaka 2025 ya Ukristo: Wamisionari wa Damu Azizi
Maadhimisho ya Jublei ya Mwaka 2025 ya Ukristo: Wamisionari wa Damu Azizi

Ni katika muktadha wa Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Wamisionari wa Shirika ya Damu Azizi ya Yesu, Vyama vya Kitume pamoja na Familia ya Damu Azizi ya Yesu, wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo kwa kunogeshwa na kauli mbiu: “Mahujaji wa matumaini katika Damu Azizi ya Yesu, uhai na wokovu wa ulimwengu.” Maadhimisho haya yameanza, Jumatatu tarehe 30 Juni 2025 kwa Mkesha wa kimataifa wa sala ukiongozwa na Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Roma na kilele chake ni tarehe Mosi Julai 2025 kwa Ibada ya Misa Takatifu inayoongozwa na Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Mahujaji wa matumaini 57 kutoka Tanzania, ambamo wamo Mapadre 7, Watawa 5 pamoja na idadi kubwa ya waamini walei, wanaendelea kushiriki katika maadhimisho haya, kama sehemu ya hija maalum ya Damu Azizi ya Kristo Yesu. Padre John Maria Greyson, Mratibu wa mahujaji wa matumaini kutoka Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, tayari mahujaji wamekwisha kutembelea sehemu muhimu za kihistoria za mji wa Roma na Vatican katika ujumla wake. Wametembelea Makanisa ya hija na kwamba, kwa sasa wanajiandaa kutembelea kwenye Madhabahu ya Mtakatifu Rita wa Cascia, Kisima na chemchemi ya amani kwani wale wote waliovunjika na kupondeka moyo wanaweza kujichotea nguvu na kuanza tena kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, huku wakifuata ile njia ya ukweli inayowaweka huru!

Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha
Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha

Wanatarajia kutembelea kwenye Makaburi ya Watakatifu: Gaspari Del Bufalo, mwanzilishi wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Maria De Mattias, Muasisi wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu ya Yesu pamoja na Kaburi la Mwenyeheri Giovanni Merlini, aliyekuwa mtu wa vitendo na utume, hasa katika mahubiri ya kimisionari ambayo kwa ajili yake aliheshimiwa sana na Mtakatifu Gaspari na pia alikuwa mwenye ujuzi wa kutawala na zaidi, aliyetajirishwa na wema wa busara.” Mwenye busara ni yule anayejua jinsi ya kuamua nini cha kufanya kwa uthabiti na kufanya hivyo kwa hekima.

Jubilei ni kipindi cha kujitakasa na kujitakatifuza
Jubilei ni kipindi cha kujitakasa na kujitakatifuza

Padre Achileus Mutalemwa, Makamu mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania, kwa niaba ya Mkuu wa Shirika Kanda ya Tanzania anasema, anamshukuru Mungu kwa mwitikio wa idadi kubwa ya mahujaji wa matumaini kutoka Tanzania, waliojiandaa vyema ili kupata neema, rehema na baraka katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025. Hiki ni kipindi cha kujitakasa na kujitakatifuza. Huu ni mwaliko wa kutambua nguvu ya Damu Azizi ya Kristo Yes una thamani yake katika mchakato wa kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Waamini waendelee kujikita katika hija ya matumaini. Kwa upande wake Sr. Bernadetta, ASC anamshukuru Mungu kwa kushiriki katika hija hii ya neema na baraka. Kwa kutembelea sehemu mbalimbali za Italia, wameweza kutambua imani yao ya Kikristo na ukuaji wao na hivyo kuendelea kushikamana katika imani, ili kutembea pamoja katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa la Kimisionari na Kisinodi. Sr. Maria Fatima na Sr. Adriana William, wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 ya maisha na wito wa kuwekwa wakfu. Wanamshukuru Mungu kwa kuwezesha kujionea maeneo ya historia ya Kanisa. Mama Beata Matemu, Mwenyekiti wa Chama cha Utume wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Dar es Salaam na Tanzania katika ujumla wake, anasema hiki ni Chama cha kitume ambacho kilianzishwa miaka kumi na mitano iliyipita, leo hii kimeenea sehemu mbalimbali za Tanzania.

Askofu Salutaris  Libena akiwa na hujaji wa matumaini
Askofu Salutaris Libena akiwa na hujaji wa matumaini

Vyama na Mashirika mbalimbali ya Kitume yaliyoibuka baada ya Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ni zawadi kubwa kwa Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Vyama na mashirika haya yanapaswa kupokelewa kwa imani na moyo wa shukrani, kama rasilimali kwa Kanisa, ili hatimaye, viweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, kwa kutambua kwamba, Kristo Yesu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika maisha yao. Ikumbukwe kwamba, vyama vya kitume ni kama shule ya imani, matumaini na mapendo. Hapa ni mahali ambapo waamini wanaweza kusaidiana katika: imani, maisha ya kisakramenti, maadili na sala. Karama ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa waamini ndani ya Kanisa, tukio ambalo ni endelevu linalowapatia changamoto wahusika, kuzitumia karama hizi kwa ajili ya mafao, ustawi na maendeleo ya Kanisa kadiri ya busara na hekima ya viongozi wa Kanisa. Vyama na mashirika ya kitume yanapaswa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutambua kwamba, waamini walei wana mchango mkubwa katika ujenzi wa Kanisa la Kristo kwa kushirikiana na wakleri pamoja na watawa. Mama Beata Matemu ni Mwenyekiti wa Chama cha Utume wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Dar es Salaam na Tanzania katika ujumla wake anasema, kwa hakika wanachama wake wanajitahidi kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu, ili Mwenyezi Mungu atukuzwe. Wamejitahidi kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma na upendo kwa maskini na wahitaji na kwamba, bado wanaendelea kujitoa bila ya kujibakiza. Huu ni utume ambao umewakomaza na kuwaimarisha kiimani. Umewafundisha tunu msingi za Kiinjili, kiutu na Kikanisa.

Jubilei ya Damu Azizi
30 Juni 2025, 15:40