ĐÓMAPµĽş˝

Kanisa Katoliki nchini Ethiopia limempokea kwa furaha Askofu mkuu Brian Ngozi Udaigwe kama Balozi mpya wa Vatican nchini Ethiopia, Kanisa Katoliki nchini Ethiopia limempokea kwa furaha Askofu mkuu Brian Ngozi Udaigwe kama Balozi mpya wa Vatican nchini Ethiopia,   (© ETHIOPIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Askofu Mkuu Brian Udaigwe Aanza Utume Wake Nchini Ethiopia

Askofu mkuu Brian Udaigwe alizaliwa tarehe 19 Julai 1964 huko Tiko, nchini Cameroon. Tarehe 2 Mei 1992 akapewa Daraja takatifu ya Upadre. Kunako tarehe 22 Februari 2013, Hayati Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Benin. Tarehe 27 Aprili 2013 akawekwa wakfu na Kardinali Tarcisio Evasio Bertone, SDB. Amewahi kufanya utume wake nchini Zimbabwe, Pwani ya Pembe, Haiti, Bulgaria, Thailand na Uingereza!

Na Bezawit Assefa, Addis Ababa na Sarah Pelaji, -Vatican

Kanisa Katoliki nchini Ethiopia limempokea kwa furaha Askofu mkuu Brian Ngozi Udaigwe kama Balozi mpya wa Vatican nchini Ethiopia, kufuatia uteuzi uliofanywa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 12 Aprili 2025. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Brian Ngozi Udaigwe, alikuwa Balozi wa Vatican nchini Sri Lanka. Askofu mkuu Udaigwe alipokelewa rasmi hivi karibuni alipowasili mjini Addis Ababa kupitia Shirika la Ndege la Ethiopia, na baadaye katika Ubalozi wa Vatican, ambako watu wa Mungu nchini walikusanyika ili kumkaribisha na kuonesha furaha yao kwa ujio wake. Askofu mkuu Udaigwe ni mzaliwa wa Jimbo Katoliki la Orlu nchini Nigeria, akiwa na uzoefu mkubwa katika huduma ya kidiplomasia ya Vatican kwa zaidi ya miongo mitatu.

Askofu mkuu Brian Udaigwe akikaribishwa na viongozi wa Kanisa Ethiopia
Askofu mkuu Brian Udaigwe akikaribishwa na viongozi wa Kanisa Ethiopia   (© ETHIOPIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Alipewa Daraja Takatifu ya Upadri tarehe 2 Mei 1992, na baadaye aliendelea na masomo katika Taasisi ya Kipapa ya Diplomasia ya Kanisa “Pontificia Accademia Ecclesiastica, PAE.” Tarehe Mosi Julai 1994 akaanza huduma ya diplomasia ya Kanisa mjini Vatican na kubahatika kutumwa na kuhudumia: Zimbabwe, Pwani ya Pembe, Haiti, Bulgaria, Thailand na Uingereza.Tarehe 22 Februari 2013 akateuliwa na Hayati Papa Benedikto XVI kuwa Balozi wa Vatican nchini Benin na Togo na kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu tarehe 27 Aprili 2013 na Kardinali Tarcisio Bertone, aliyekuwa Katibu mkuu wa Vatican wakati ule. Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe 13 Juni 2020 akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Sri Lanka hadi alipohamishiwa nchini Ethiopia.

Watu wa Mungu wakimkaribisha Balozi wa Vatican nchini Ethiopia
Watu wa Mungu wakimkaribisha Balozi wa Vatican nchini Ethiopia   (© ETHIOPIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Wakati wa sherehe ya mapokezi, Monsinyori Massimo Catterin, Katibu wa Ubalozi wa Vatican nchini Ethiopia alitoa pongezi za dhati kwa Askofu Mkuu Udaigwe na kumkaribisha nchini Ethiopia. Pia alitaja uteuzi huo kuwa maalum kwa sababu Papa Francisko, aliyefariki hivi karibuni, ndiye aliyemteua Askofu mkuu siku tisa kabla ya kifo chake ishara ya upendo wa kudumu wa Hayati Baba Mtakatifu Francisko kwa Kanisa nchini Ethiopia. Monsinyori Catterin alimhakikishia Askofu mkuu umoja na ushirikiano kamili kutoka kwa timu ya Ubalozi wa Vatican nchini Ethiopia akisema kwa maneno haya: “Hakika wewe ni baba yetu, sisi ni wanao ambao tuko tayari kusikiliza na kutiwa moyo na ujuzi pamoja na uzoefu wako.”

Askofu Mkuu Brian Udaigwe
Askofu Mkuu Brian Udaigwe   (© ETHIOPIA EPISCOPAL CONFERENCE)

Katika hotuba yake, Askofu mkuu Udaigwe alieleza shukrani zake za dhati kwa umuhimu wa kihistoria na kiroho wa Ethiopia, akisisitiza nafasi yake kama kitovu cha Mataifa mengi Barani Afrika. Alilisifu Kanisa Katoliki nchini Ethiopia kwa juhudi zake na kusisitiza umuhimu wa kusaidiana na kushirikiana “kwa ajili ya utukufu wa Mungu.” Katika maelezo yake, aligusia upekee wa uteuzi wake, akieleza kuwa mchakato ulianza chini ya uongozi wa hayati Papa Francisko na kukamilishwa na Baba Mtakatifu Leo XIV. Alisema kuwa hilo linafanya utume wake nchini Ethiopia kuwa safari ya kipekee na yenye maana katika huduma kwa Kanisa. Kwa uteuzi wake huu mpya, Askofu mkuu Udaigwe analeta uzoefu mkubwa wa kidiplomasia na kichungaji katika eneo la Pembe ya Afrika, akiendeleza wajibu wake wa kumwakilisha Baba Mtakatifu na kuimarisha uhusiano kati ya Vatican na Kanisa la Ethiopia.

Nuncio Ethiopia
23 Juni 2025, 16:44