Watawa: Maisha ya Wakfu: Matumaini Yanayoleta Mageuzi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Tangu mwanzoni mwa Kanisa walikuwepo watu, wanaume na wanawake, ambao kwa kutekeleza mashauri ya kiinjili walinuia kumfuata Kristo kwa hiari zaidi na kumwiga kwa karibu, na walienenda, kila mmoja kwa jinsi yake, katika maisha ya wakfu kwa Mungu. Wengi miongoni mwao, kwa kufuata msukumo wa Roho Mtakatifu, waliishi maisha ya upweke, au walianzisha familia za kitawa, ambazo Kanisa kwa mamlaka yake lilizikubali kwa moyo na kuziidhinisha. Hivyo, kwa mpango wa kimungu, wingi wa ajabu wa mashirika ya kitawa ukasitawi, nayo yamechangia sana ili Kanisa lisiwe tu limekamilishwa lipate kutenda kila tendo jema (taz. 2Tim 3:17), na liwe limeandaliwa hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe (taz. Efe 4:12), bali pia, liwe linapendeza kwa wingi wa karama mbalimbali za wanae, nalo lionekane pia kama bibiarusi aliyekwisha kupambwa kwa mumewe (taz. Ufu 21:2), na kwa njia yake hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane (taz. Efe 3:10.) Katika wingi huu wa karama, wale wote wanaoitwa na Mungu kutekeleza mashauri ya kiinjili na kuyatimiza kiaminifu, wanajiweka wakfu kwa Bwana kwa namna ya pekee, kwa kumfuasa Kristo ambaye, akiwa bikira na maskini (taz. Mt 8:20; Lk 9:58), aliwakomboa wanadamu na kuwatakatifuza kwa njia ya utii wake mpaka kufa msalabani (taz. Flp 2:8). Vivyo hivyo nao watu, walihimizwa na pendo ambalo Roho Mtakatifu amemimina mioyoni mwao (taz. Rum 5:5) wanaishi zaidi na zaidi kwa ajili ya Kristo na kwa ajili ya Mwili wake ulio Kanisa (taz. Kol 1:24). Kwa hiyo, kama wanavyojiunga kwa ari na Kristo kwa njia ya kujitolea kwao maisha yote, ni kadiri hiyohiyo maisha ya Kanisa yananufaika na utume wake unazidi kuwa na nguvu za kuleta matunda.
Shirikisho la Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume kutoka katika nchi 75 ulimwenguni, linalowahusisha wakuu wa Mashirika 900, kuanzia tarehe 5 Mei 2025 hadi tarehe 9 Mei 2025 wanakusanyika mjini Roma, katika mkutano wao unaonogeshwa na kauli mbiu “Maisha ya Wakfu: Matumaini Yanayoleta Mageuzi.” Huu ni muda muafaka kwa watawa hawa kutafakari kwa kina na mapana dhamana na wito wao wa kukoleza matumaini kwa watu wa Mungu waliovunjika na kupondeka moyo, kama alivyofanya Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha miaka kumi na miwili ya uongozi wake, na hasa katika kipindi hiki ambacho Makardinali wamekusanyika kwa ajili ya uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro: “Conclave.” Mababa wa Kanisa wanasema, matumaini ni fadhila ya kimungu inayotuwezesha kutamani heri ya Ufalme wa mbinguni na uzima wa milele, kwa kutumainia ahadi za Kristo na kutegemea, siyo nguvu zetu, bali msaada wa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini wanahimizwa kulishika kikamilifu ungamo la matumaini yao kwa sababu Kristo Yesu ni mwaminifu daima.
Ni Roho ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Kristo Yesu Mwokozi wetu, ili tukihesababiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu. Fadhila ya matumaini yajibu tamaa ya heri ilivyowekwa na Mungu katika moyo wa kila mtu. Yachota matumaini yanayovuvia matendo ya watu. Huyatakasa ili kuyapanga kwa ajili ya ufalme wa mbinguni nyakati za upweke. Hufungua moyo katika kungoja heri ya milele. Akielekezwa na matumaini anakingwa na ubinafsi na anaongozwa kwenye furaha itokanayo na upendo. Matumaini ya Kikristo huchukua na kukamilisha matumaini ya Taifa Teule lililo na chanzo na mfano katika matumaini ya Ibrahimu, aliyebarikiwa kwa wingi wa ahadi za Mungu zilizotimilizwa katika Isaka na aliyetakaswa kwa majaribu ya sadaka. Alitumaini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa ni Baba wa Mataifa mengi. Heri za Mlimani ni muhtasari wa matumaini ya Kikristo, kwa kuonesha majaribu wanayoweza kukutana nayo katika hija ya maisha yao. Lakini kwa mastahili ya Yesu Kristo, Mwenyezi Mungu anawalinda katika tumaini lisilotahayarisha. Matumaini ni nanga ya roho hakika na thabiti, ni pia silaha inayowalinda waamini katika mapambano ya wokovu. Matumaini huleta furaha hata katika majaribu na ni muhtasari wa Sala ya Baba yetu. Kila mtu anaweza kutumaini kwa msaada wa neema ya Mungu. Katika tumaini Kanisa linasali ili watu wote waokolewe. Latamani kuungana na Kristo Yesu, Mchumba wake katika utukufu wa mbinguni. Rej. KKK 1817-1821.
Watawa wanataka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini katika maeneo yenye changamoto nyingi kama Sudan ya Kusini, Myanmar, pamoja na Amerika ya Kusini. Maadhimisho ya Jubilei Kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Mahujaji wa Matumaini.” Watawa wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, haki na amani. Wakuu wa Mashirika kutoka Barani Ulaya ni 1046, Barani Asia ni 184, kutoka Barani Afrika ni 166, Oceania 28 na Amerika wako 479. Karama na maisha ya wakfu ni chemchemi ya unabii wa matumaini kwa watu wa Mungu! Watawa kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria chini ya Msalaba, wanataka kuwa ni mashuhuda na vyombo vya matumaini kwa watu wa Mungu. Wakuu wa Mashirika wanaungana na Kanisa zima katika: Sala na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu ili kuombea uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili Baba Mtakatifu atakayechaguliwa awe kweli ni chombo cha haki, amani, maridhiano; Mjenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari.