ĐÓMAPµĽş˝

2025.05.18 Papa Leo XIV katika misa ya kuanza utume wake. 2025.05.18 Papa Leo XIV katika misa ya kuanza utume wake. 

Kard.Parolin:tuunge mkono nia ya Papa Leo XIV ya kujenga madaraja,kukutana,mazungumzo!

Katibu wa Vatican,Kardinali Parolin akiwa nchini Marekani katika hafla iliyofanyika kwenye Umoja wa Mataifa mjini New York amekumbusha juu ya uchaguzi wa Papa kuwa,Vatican inaendeleza juhudi zake za kukuza amani na haki katika ulimwengu uliojaa migawanyiko, migogoro na matatizo ya dharura ya kimataifa.Papa Leo XIV anatoa mwaliko wa kukumbatia Diplomasia ya kutana na hivyo tuitikie mwito wa kujenga amani ya kudumu katika historia na sio wale wanataka kuvuna waathirika.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katibu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin akiwa huko mjini New York Marekani katika Umoja wa Mataifa kwenye hafla ya kuchaguliwa kwa Papa mpya Leo XIV iliyoandaliwa na Mwakilishi wa  kudumu katika Ofisi hiyo, Askofu Mkuu Gabriele Caccia, Jumatatu tarehe 19 Mei 2025, alitoa hotuba yake. Akiwageukia washiriki waliokuwapo, Kardinali Parolin alionesha furaha kuhutubia mkusanyiko huo katika fursa ya kuadhimisha kuchaguliwa kwake Mtakatifu Leo wa kumi na nne. “Natanguliza shukrani zangu kwa  Askofu Mkuu Gabriele Caccia kwa kuandaa tukio hili na kila mmoja wenu kwa uwepo wenu hapa leo.”

Kardinali Parolin aidha alisema kuwa “Uchaguzi wa Papa mpya ni tukio la kufanywa upya, si kwa Wakatoliki pekee bali kwa wote wanaotafuta ulimwengu wa haki zaidi, mshikamano na amani. Papa Leo, katika siku zake za kwanza kama Mrithi wa Petro, ameelezea dhamira yake ya kina ya kujenga madaraja, akisisitiza haja ya kukutana, mazungumzo na majadiliano.” Na kwa njia hiyo “Vatican inathibitisha tena uungwaji mkono wake usioyumba kwa utume wa Umoja wa Mataifa,  kuwa jukwaa ambapo Mataifa hushiriki katika mazungumzo, kutoa sauti za watu wao, na ambapo suluhisho za changamoto kuu za wanadamu zinatengenezwa.”

Kardinali Parolin katika hafla
Kardinali Parolin katika hafla

Kardinali Parolin akitazama mgogoro ya dunia alisema “Katika ulimwengu ulio na mgawanyiko, migogoro, na masuala muhimu ya kimataifa – kuanzia na  mabadiliko ya tabianchi hadi uhamiaji na Akili Nunde,  Papa Leo  anatualika kukumbatia diplomasia ya kukutana. Hii ni diplomasia inayosikiliza kwa unyenyekevu, kutenda kwa huruma, na kutafuta manufaa ya wote juu ya yote.” Kwa hiyo “Vatican chini ya uongozi wake, inaahidi kufanya kazi pamoja nanyi, wawakilishi wa mataifa, kukuza utu wa binadamu, kulinda walio hatarini, na kujenga madaraja ambapo kutokuaminiana kunaweza kutawala. Jukumu lenu kama Wawakilishi wenu katika Nchi zenu ni muhimu katika kutengeneza muundo wa ushirikiano wa kimataifa.”

Na kwa njia hiyo “Vatican inatambua sadaka wanayotoa ili kuendeleza amani na haki, mara nyingi katika uso wa utata mkubwa.” Kardinali Parolin alikazia kusema kuwa “Maono ya Papa Leo yanawiana na harakati hii adhimu ya kupendelea shughuli ya kidiplomasia inayojikita katika nguzo za amani, haki na ukweli. Hivyo basi, Vatican ambayo imejkita katika ukweli na haki, itaendelea kutoa sauti yake ya kimaadili katika kuwatetea maskini na wale wanaohitaji, na katika kutafuta amani na maendeleo fungamani ya binadamu.” Katibu wa Vatican alitoa mwaliko kuwa “Na sisi, kwa pamoja, tuitikie wito wa Baba Mtakatifu na kuwa wale wanaopanda amani ambayo itadumu katika historia, na sio wale wanaovuna waathirika.

Kardinali Parolin wakati wa kutoa hotuba katika hafla ya kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV
Kardinali Parolin wakati wa kutoa hotuba katika hafla ya kuchaguliwa kwa Papa Leo XIV

Kwa mara nyingine tena, Katibu wa Vatican alitoa “asante kwa uwepo wenu na kujitolea kwenu kwa huduma ya wanadamu. Mungu awabariki ninyi, familia zenu, na mataifa mnayowakilisha. Tusonge mbele pamoja, tukiongozwa na matumaini na maono ya Papa Leo.” Kwa kuhitimisha “Tunapoadhimisha sura hii mpya ya maisha ya Kanisa, ninawaalika kuungana nami katika kutoa heshima ya Baba Mtakatifu Leo wa kumi na nne, Bwana amhifadhi, ampe uzima na afya njema, amfanyie furaha duniani na kumlinda na mabaya yote.”

Kardinali Parolin
19 Mei 2025, 20:30