Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA, Jimbo Katoliki Bagamoyo: Uzinduzi!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ushirikishwaji wa watu wa Mungu ni changamoto inayopewa kipaumbele cha pekee na Hayati Baba Mtakatifu Francisko. Parokia iwe ni mahali pa kuonesha umoja na utofauti wa karama kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake. Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” unapania pia kuhamasisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji miongoni mwa Parokia jirani, ili kujenga: umoja, mshikamano na mafungamano ya Kikanisa kati ya Parokia zilizoko mjini na zile ambazo ziko pembezoni mwa miji. Katika muktadha huu, Askofu Jimbo anaweza kuwateua madekano, watakaoendeleza umoja na Askofu Jimbo. Pale ambapo baadhi ya Parokia zitaunganishwa ili kuboresha ufanisi zaidi, kuna haja ya kujenga na kuimarisha mchakato wa ushirikiano kati ya Askofu Jimbo, Wasaidizi wake wa karibu pamoja na waamini walei na kwamba, Waraka huu utakuwa ni msaada mkubwa kwao kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ili kuweza kuwa na mwingiliano wa Parokia wenye tija kwa wengi, kuna haja ya kuzingatia historia ya watu, maisha na tofauti zao msingi. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, watu wote wa Mungu wanahusishwa kikamilifu hatua kwa hatua na katika hali ya unyenyekevu, kabla ya kufikia maamuzi ya mwisho, ili kujenga mwendelezo wa mafungamano ya kijamii na wala si kinyume chake! Waraka Kuhusu: Maagizo: “Wongofu wa Kichungaji Katika Jumuiya ya Kiparokia Kwa Ajili ya Huduma ya Uinjilishaji Ndani ya Kanisa” ni jibu makini kwa wakati huu, ili kusoma alama za nyakati, ili kuliwezesha Kanisa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu, wachungaji wakuu wa Kanisa, wakiwa wameshibana na watu wa Mungu chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Maagizo haya yanabeba ndani mwake, utajiri wa kitaalimungu, shughuli za kichungaji na sheria za Kanisa. Lengo ni kujenga umoja katika tofauti kama kielelezo cha amana na utajiri wa Kanisa.
Chimbuko la Jimbo la Bagamoyo: Historia inaonesha kwamba, wakati Wamisionari wakitekeleza majukumu yao ya Uinjilishaji, hali ya utume ilikuwa ngumu katika mambo mbalimbali huko Zanzibar. Hivyo, Wamisionari walimuomba Sultani awapatie ekari 80 katika eneo la Bagamoyo, upande wa Bara. Wakati huo, Bagamoyo ilikuwa kituo ambapo watumwa walikusanywa kabla ya kusafirishwa kwa meli kwenda Zanzibar. Kwa hiyo, Bagamoyo imekuwa Mama wa utume wote wa Kanisa Tanzania Bara. Uinjilishaji wa mwanzo wa Tanganyika ulifanywa na Mashirika matatu. La kwanza, ni Shirika la Roho Mtakatifu ambalo liliinjilisha Zanzibar na kupitia Bagamoyo kuelekea kaskazini hadi Mlima wa Kilimanjaro. Shirika la pili ni Wamisionari wa Afrika waliojulikana kama Mapadre Weupe (White Fathers) kwa sababu ya kanzu zao. Wao waliinjilisha kuanzia Tabora, sehemu yote ya Magharibi hadi Mbeya, Kigoma, Bukoba na Musoma. Shirika la tatu lilikuwa la Wabenediktini wa Mtakatifu Ottilien ambao walianzia Dar es Salaam na kuelekea kusini hadi Bihawana, Dodoma, Mahenge, Songea na Lindi. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza, mashirika mengine yalianza kuingia kusaidia. Miongoni mwao ni: Wafransiskani Wakapuchini, Wakonsolata, Wapalotini na Wapasionisti. Aidha, baada ya Vita Vikuu vya Pili walikuja Wasalvatoriani, Warosmini na Wamaryknoli. Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, (Propaganda Fide) lilitoa sehemu ya kuinjilisha na kuongoza kwa kila Shirika. Majimbo yalipopata Maaskofu wazawa, waliyaalika mashirika mengine mengi kuja kuwasaidia bila kushika uongozi wa jimbo.
Vikariati ya Bagamoyo: Misioni ya kwanza iliyokuwa Zanzibar tangu mwaka 1860 haikuwa ikitoa matunda, na maisha ya uinjilishaji yalikuwa magumu. Ingawa makao makuu yalibaki Zanzibar, shughuli nyingi zilihamishiwa Bagamoyo. Misioni ya Bagamoyo ilianza tarehe 4 Machi, 1868. Kazi ya kwanza Bagamoyo ilikuwa kuwahudumia watumwa waliokombolewa. Kazi hii ilifanyika vizuri na kukawa na kijiji cha Wakristo, shule za kuwalea watoto na kufundisha kazi za ufundi kwa watu wazima. Misioni ya Bagamoyo ilikuwa kama mji mdogo wenye zaidi ya nyumba 50 zenye vijana zaidi ya 300 waliojifunza mambo mbalimbali kulingana na umri na uwezo wao. Pia, zilikuwapo takribani familia 30 za Wakristo. Mwaka 1904, Vikariati ya Zanzibar, chini ya Shirika la Roho Mtakatifu, ikiwa na askofu wake, ilikuwa na misioni 19; na kati ya hizo 12 zilikuwa chini ya Bagamoyo na nyingine zikiwa Zanzibar na Kenya. Tangu utume wa Mapadre wa Roho Mtakatifu ulipoanza, makao yake makuu yalibaki kuwa Zanzibar na Askofu wake wa kwanza, Jean-Marie-Raoul Le Bas de Courmont, C.S.Sp., (1883-1896) na aliyemfuata Emile-Auguste Allgeyer, C.S.Sp. (1897 – 1913) waliishi Zanzibar ingawa kazi nyingi za kitume zilikuwa Bagamoyo na baadaye nyingine zikawa Nairobi, Kenya. Januari 15, 1907, Vatican iliigawanya Vikariati ya Zanzíbar ya Kaskazini. Sehemu zilizokuwa chini ya Waingereza kama Zanzíbar na Kenya, zilibaki chini ya Askofu wa Zanzíbar na katika sehemu iliyokuwa chini ya Wajerumani iliundwa vikariati mpya ambayo baadaye iliitwa Vikariati ya Bagamoyo. Padre Xaver Vogt aliteuliwa kuwa Askofu wake wa kwanza. Wakati huo, Vikariati mpya ya Bagamoyo ilikuwa na mapadre 30, mabruda 20 na masista 8. Masista wote walikuwa hapo Misioni ya Bagamoyo. Waamini kwa pamoja walikuwa 13,600, katika vituo vyote vya misioni 14. Masista watatu walifanya kazi katika hospitali iliyojengwa kwa msaada wa Mhindi tajiri, Sewa Hadji. Mwaka 1910, Askofu Vogt alianza ujenzi wa Kanisa Kuu. Kanisa zuri na imara lilijengwa kwa mawe ya baharini (Coral rocks) na kumalizika mwaka 1914 kabla ya Vita Vikuu vya Kwanza. Vita Vikuu vilipoanza, uhusiano kati ya Wamisionari na Wajerumani ulikuwa mzuri. Hata hivyo, kidogo kidogo uhusiano huo ulianza kudorora kiasi cha kufanya shughuli za uinjilishaji kukabiliwa na changamoto kubwa katika eneo la Bagamoyo. Hivyo, baada ya Vita Vikuu vya Kwanza ya Dunia, uinjilishaji ulikazia zaidi sehemu ya nje ya Bagamoyo ambapo waliwapata kwa urahisi wakatekumeni na waamini. Mwishowe, mwaka 1932 makao makuu ya Vikariati yalihamia Morogoro.
Jimbo Lahamia Morogoro: Jimbo la Morogoro linatokana na Vikariati ya Bagamoyo. Historia ya Bagamoyo ni historia ya Morogoro. Kufikia Vita Vikuu vya Kwanza, katika Jimbo la Morogoro la sasa, zilikuwa zimeshafunguliwa misioni 9 ambazo ni: Mandera (1881), Morogoro (1882), Tununguo (1884), Ilonga (1885), Matombo (1897), Mgeta (1905), Maskati (1908), Vidunda (1910) na Lugoba (1911); misioni za Bahi na Kurio baadaye ziliingizwa katika Jimbo la Dodoma. Kulikuwa na misioni nyingine nje ya Morogoro kuelekea Kilimanjaro. Licha ya kumegwa Vikariati ya Kilimanjaro (Moshi) mwaka 1910, sehemu ya Bagamoyo ilimegwa tena ili kuunda unyampara wa Dodoma mwaka 1935. Tarehe 8 Agosti, 1932, kwa sababu ya hitaji la kuwa na makao makuu ya askofu katikati ya vikariati, Askofu Bartholomew Stanley Wilson aliyahamisha makao makuu yake kutoka Bagamoyo na kuyapeleka Morogoro mjini. Tarehe 25 Machi, 1953, pamoja na vikariati nyingine za Tanganyika, Vikariati ya Bagamoyo ilipandishwa hadhi na kuwa Jimbo la Morogoro chini ya Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kuundwa kwa Jimbo la Bagamoyo: Mnamo tarehe 7 Machi 2025, Hayati Baba Mtakatifu Francisko aliliunda Jimbo Katoliki la Bagamoyo, kwa kuligawa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Jimbo la Morogoro na kumteua Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA, kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA alikuwa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Bagamoyo ni la Moyo Safi wa Bikira Maria, lililopo mjini Bagamoyo. Jimbo la Bagamoyo linakuwa na parokia 27 na Parokia Teule 3, mapadre jimbo 14, mapadre watawa 30 na watawa 128.
Historia Fupi ya Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA (“Loquere Domine Quia Audit Servus Tuus”) “Nena Bwana kwa Maana Mtumishi Wako Anasikia” Maisha ya Awali na Safari ya Wito: Alizaliwa tarehe 25 Septemba 1969, katika Kijiji cha Malonji, Wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe. Baba yake ni Lameck Musomba na mama yake ni Maria Kandonga. Safari yake kielimu ilianzia katika Shule ya Msingi Malonji kuanzia kwaka 1979 hadi mwaka 1985 alipohitimu darasa la saba. Alijiunga na Seminari Ndogo ya Maua iliyopo Jimbo Katoliki Moshi kwa ajili ya masomo ya kidato cha kwanza hadi cha sita, kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1995. Baada ya hapo, alijiunga na Taasisi ya Wasalvatoriani huko Kola, Morogoro, kwa ajili ya masomo ya Falsafa na Taalimungu kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2003 na kutunukiwa shahada za awali za Falsafa na Taalimungu. Katika safari ya wito, alianza kuvutiwa na wito wa kitawa tangu mwaka 1988 na kwenda kupata uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya kitawa katika Shirika la Waagustiniani (OSA) huko Mahanje, Jimbo Kuu la Songea. Baada ya hapo, alijiunga na upostolanti kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 1998 huko Mahanje na baadaye huko Morogoro. Kuanzia mwaka 1998 hadi 1999, alipokea malezi ya unovisi huko Jimbo Kuu la Manila, nchini Ufilipin. Mnamo tarehe 25 Septemba 2002, aliweka nadhiri za daima katika Shirika la Kitawa la Waagustiniani (OSA) na mwaka huo huo tarehe 9 Disemba, 2002, alipata daraja la Ushemasi katika Taasisi ya Wasalvatoriani ambayo kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Jordan Morogoro.
Huduma ya Kipadre: Alipewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 24 Julai, 2003, huko Mahanje, Jimbo Kuu la Songea. Baadaye aliteuliwa kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mavurunza kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2004. Baada ya hapo, alitumwa kwenda kusomea Elimu ya Mababa wa Kanisa (Patrology) kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2008 katika Chuo cha Instutum Patristicum Augustinianum kilichopo Roma, Italia, ambapo alitunukiwa Shahada ya Umahiri katika masomo ya Taalimungu akibobea katika Elimu ya Mababa wa Kanisa (Patrology). Baada ya masomo huko Roma, kuanzia mwaka mwaka 2008 hadi mwaka 2009, alikuwa mlezi katika Nyumba ya Shirika la Waaugustiani na mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro. Mwaka 2009 alitumwa na Shirika kwenda Jimbo Kuu la Manila, nchini Ufilipin, kwa ajili ya kutoa semina mbalimbali kwa Wanovisi, Waprofesi na Wapostulanti. Mwaka 2009 hadi mwaka 2015, alikuwa Paroko wa kwanza katika Parokia ya Temboni, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, huku akiendelea kuwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Jordan Morogoro. Mwaka 2015 aliteuliwa tena kuwa Wakili Paroko wa Parokia ya Mavurunza na msimamizi wa Jumuiya ya Mtakatifu Monika Mavurunza. Mwaka huohuo aliteuliwa kuwa Paroko wa muda wa Parokia ya Mtakatifu Ambrose Tagaste, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, hadi mwaka 2016. Mwaka 2016 aliteuliwa kuwa Mlezi na Mkuu wa Nyumba ya Malezi ya Mtakatifu Agostino iliyopo Morogoro, nafasi alizohudumu hadi 2019. Kuanzia mwaka huo 2019 hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu Msaidizi, alikuwa ni Paroko na Msimamizi wa Jumuiya za Kitawa za Mtakatifu Monika Mavurunza, Temboni na Mtakatifu Rita wa Kashia. Vilevile, katika kipindi chote, pamoja na nyadhifa zingine zilizotajwa, kuanzia mwaka 2008 hadi 2021, alihudumu kama Katibu Mwakilishi wa Shirika la Waagustiniani nchini Tanzania. Kuteuliwa Uaskofu Tarehe 7 Julai 2021, aliteuliwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na kuwekwa wakfu kuwa askofu tarehe 21 Septemba 2021. Tarehe 7 Machi 2025, Baba Mtakatifu Francisko aliliunda Jimbo Katoliki la Bagamoyo, nchini Tanzania, kwa kuligawa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Jimbo la Morogoro na kumteua Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA, kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo.