MAP

Askofu Msaidizi Josephat Jackson Bududu anaongozwa na kauli mbiu: “Mapenzi yako yatimizwe”: na kwa lugha ya Kilatini: "Fiat voluntas tua" Mt 26:42. Askofu Msaidizi Josephat Jackson Bududu anaongozwa na kauli mbiu: “Mapenzi yako yatimizwe”: na kwa lugha ya Kilatini: "Fiat voluntas tua" Mt 26:42. 

Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu: Zawadi Kwa Kanisa

Kardinali Protase Rugambwa ameongoza madhehebu ya kuwekwa wakfu kwa Askofu msaidizi Josaphat Jackson Bududu wa Jimbo kuu la Tabora. Sasa amekabidhiwa majukumu ya kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaendelea kulaani kitendo cha aibu, kibaya na kiovu alichotendewa Padre Charles Kitima. Serikali itaendelea kushirikiana na Kanisa na dini mbalimbali katika ustawi, &maendeleo ya watanzania

Na Sarah Pelaji, - Vatican

Jimbo Kuu Katoliki Tabora limepata Askofu msaidizi baada ya aliyekuwa Askofu Mteule Msaidizi Josaphat Jackson Bududu kuwekwa wakfu kuwa Askofu msiaidizi tarehe 25 Mei 2025 katika viwanja vya Kanisa kuu la jimbo hilo huku Madhehebu ya kumuwekwa wakfu yakiongozwa Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora. Askofu mkuu Angelo Accatino Balozi wa Vatican nchini Tanzania ameeleza furaha yake ya kushriki maadhimisho hayo akimkumbuka Hayati Papa Francisko aliyemyetua Askofu Bududu kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo hilo Kuu mnamo tarehe 26 Februari Mwaka 2025 kabla ya kufariki dunia. Ameelezea pia upendo wa kibaba wa Papa Leo XIV ambaye amechaguliwa Mei 8 2025 kuliongoza Kanisa Katoliki Duniani. Amewataka waamini nchini Tanzania kumwombea Papa Leo XIV ili Mungu amlinde, amuelekeze na kumwongoza kwa neema yake afanikiwe kuliongoza na kulisimamia Kanisa la Kristo Yesu. Askofu mkuu Angelo Accatino amempongeza Askofu msaidizi wa Jimbo kuu Katoliki Tabora Josaphat Bududu kwa kuwekwa wakfu kuwa askofu na kumsaidia Askofu wa Jimbo hilo kuu katika shughuli za kichungaji akimsihi kujikabidhi kwa Mungu siku zote kama alivyo kauli mbiu yake ‘Mimi hapa nimekuja kuyafanya mapenzi yako."

Askofu msaidizi Bududu akiwekwa wakfu na Kardinali Rugambwa
Askofu msaidizi Bududu akiwekwa wakfu na Kardinali Rugambwa

"Askofu msaidizi Bududu umechaguliwa kutoka miongoni mwa watu ili kuwawakilisha ya husuyo Mungu, hili litawezekana tu ikiwa unatambua kuwa si kwa sifa zako bali kwa neema ya Mungu. Nyuki uliowachagua katika ngao yako ambao ni rasilimali katika mkoa huu unaowafanya kuwa tajiri kwa asali tamu, wawe daima alama ya dhamana yako katika kunyonya asali ya imani yenye upendo na udugu uliopo mioyoni mwa watu." Aidha amemtaka katika kutimiza wajibu wake kama Askofu wa kufundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza wa Mungu abaki katika ushirika na Baba Mtakatifu, Askofu mkuu wa Jimbo, Maaskofu, Mapadri, Watawa na Waamini ili kukuza umoja na maelewano kwa wote akiamini kuwa atakuwa mchungaji mwema shirikishi, mwenye umoja na upendo wa kibaba, akiwajibika kwa wote katika usawa na huruma hasa kwa watu waliotengwa na waliosahaulika na jamii. Ameshukuru uwepo wa viongozi mbalimbali wa Serikali, viongozi mashuhuri na viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali ambao wanamkumbusha Askofu Bududu kuwa yeye ni Askofu wa watu wote hivyo katika utume wake aendeleze maendeleo ya kijamii bila ubaguzi wowote. Amethamini uwepo wa umati mkubwa wa waamiini kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Tabora wakishiriki na kushuhudia kuwekwa wakfu kwa Askofu Msaidizi Bududu akisema ni ishara inayoonesha imani na upendo usiofutika.

Kardinali Protase Rugambwa, akimpatia Askofu msaidizi vitendea kazi
Kardinali Protase Rugambwa, akimpatia Askofu msaidizi vitendea kazi

Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania Askofu Wolfgang Pisa ametoa shukrani na pongezi kwa zawadi ya Askofu msaidizi Josaphat Jackson Bududu pamoja na Kardinali Rugambwa kama Askofu Mkuu wa Jimbo kumpata msaidizi. Mintarafu kumpata Baba Mtakatifu mpya, Askofu Pisa amemshuku Kardinali Rugambwa kwa kuiwakilisha Tanzania katika Mkutano wa Baraza la Makardinali kwa ajili ya kumchagua Papa akisema kuwa ni heshima na zawadi kwa Kanisa Katoliki Tanzania. Amemuasa Askofu Msaidizi Bududu kuwa kazi ya kuwa msaidizi si kushauri kile ambacho bosi anapenda na matakwa yake tu kwani akifanya hivyo hatakuwa si mshauri mzuri bali kusaidiana kushauri katika unabii. Katika kila kitu mumuulize kwanza Mungu anataka nini ili kufanikisha utume wao katika jimbo hilo.

Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania
Baraza la Maaskofu katoliki Tanzania   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Askofu Wolfgang Pisa amewashukuru waamini kwa sala zao juu ya afya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC Padri Charles kitima aliyevamiwa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana akisema kwa sasa afya yake imeimarika hivyo muda wowote anaweza kurejea kazini. “Sisi tunaendelea kulaani kitendo hicho ambacho ni cha aibu, kibaya na kiovu kilicholenga kukatisha uhai wa Padri Kitima ambaye ni katibu wetu Mkuu TEC. Katika utawala bora na wa kisheria wahalifu wale walipaswa wawe wameshafikishwa mahakamani mpaka sasa. Ni matumaini yetu uchunguzi huo hautachukua muda mrefu zaidi ili wahusika wafikishwe mbele ya vyombo vya sheria. Hakuna raia anayependa kuishi katika nchi isiyo na Amani hivyo ni hatari kukaa na magenge hayo ya wahalifu kuendelea kukaa katika jamii kwani si salama kwa raia na kwa wenye mamlaka pia, mlifahamu hilo,” amesisitiza Rais wa TEC. Amesisitiza waamini kujiombea, kuiombea nchi ya Tanzania kuwa na mifumo na sheria nzuri ya kulinda raia ili Amani, haki, ukweli na Demokrasia vitawale.

Kardinali Rugambwa anamshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu Msaidizi
Kardinali Rugambwa anamshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu Msaidizi

Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa jimbo hilo kupata Askofu msaidizi huku akiwaalika waamini wamuombee Hayati Papa Francisko aliyetoa zawadi na Baraka kwa jimbo hilo kabla ya kufariki yaani kupewa Askofu Msaidizi. “Tangu nipate taarifa ya kupata Askofu Msaidizi nimejawa na furaha moyoni hivyo ninakukaribisha Askofu Josaphat Bududu tufanye kazi kwa pamoja tuliyokabidhiwa na kiti cha kitume. Pamoja na kushukuru Maaskofu, Mapadri, Watawa na Waamini kwa ushirikiano tangu uteuzi wa Askofu mpaka kufanikisha maadhimisho hayo, ametangaza Parokia tatu mpya na Parokia Teule Nne zote zikiwa tayari na wachungaji watakaozihudumia. Parokia mpya ni ya Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni Mgelela Paroko wake akiwa ni Padri Paschal Kadege. Parokia ya Mtakatifu Theresia wa Kalkuta Oysterbay Urambo Paroko wake akiwa Padri Cornelio Chaula. Parokia ya Mtakatifu Yuda Thadei Kidatu Paroko wake akiwa Padri Joseph Mgejwa. Pia alizitaja Parokia Teule kuwa ni Parokia Teule ya Mtakatifu Charles Boromeo Igurubi Igunga na Msimamizi akiwa Padri Jacob Mayengo. Mtakatifu Francisko Xavery Ibologero Msimamizi akiwa Padri Peter Kulwa. Parokia Teule ya Rosa wa Lima, Kalemela A Urambo Msimamizi akiwa ni Padri Edward Ntunde. Parokia teule ya Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Kitunda Msimamizi akiwa ni Padri Ignasi Akilimali.

Baadhi ya Maaskofu Katoliki wakishiriki katika Ibada ya Masifu ya jioni
Baadhi ya Maaskofu Katoliki wakishiriki katika Ibada ya Masifu ya jioni

Aidha Kardinali Rugambwa ameligawa jimbo Kuu Tabora katika maeneo makuu mawili ya ya shughuli za kichungaji. “Ili mimi na Askofu tuweze kutoa huduma stahiki na zinazohitajika kwa walengwa na ikiwa ni baada ya kusikiliza maoni ya washauri wetu tumeona kuwa inafaa kuligawanya Jimbo ikiwa ni sehemu ya kutekeleza mikakati ya kichungaji jimboni kwetu. Hivyo, Dekania ya Igunga na Nzega zitakuwa chini ya uangalizi wa karibu wa Askofu msaidizi Josaphat Jackson Bududu. Dekania za Tabora na Urambo zitakuwa chini ya uangalizi wa karibu wa Askofu Mkuu wa Jimbo. Mungu aliyetuita na akataka tumtumikie yeye mwenyewe tunamwomba asimamie na kuyaongoza yote yatakatofanyika,” alisema Kardinali Rugambwa. Alimkaribisha Wakili wa Jimbo hilo Padri Faustine Rwechungura kutaja zawadi ya Jimbo Kuu la Tabora kwa Askofu msaidizi Bududu ambapo Padri Rwechungura alisema jimbo hilo limemzawadia chombo cha usafiri aina ya Landcruzer Prado ili limwezshe kutekeleza shughuli zake za kitume na kichungaji.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania likishiriki Masifu ya jioni
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania likishiriki Masifu ya jioni

Akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Mhe. Willium Lukuvi amempongeza Askofu msaidizi Josaphat Bududu kuwekwa wakfu na kuwa Askofu Msaidizi Jimbo Kuu Katoliki Tabora. Amesema Serikali inatambua mchango wa huduma za kijamii zinazotolewa na Kanisa Katoliki nchini hususani Jimbo Kuu Tabora ambapo pamoja na kuwa na shule mbalimbali ipo shule maalumu ya watu wasiosikia (viziwi) inayotoa huduma kwa wananchi wote bila ubaguzi. Amewaomba maaskofu na waamini wote kuendelea kuiombea nchi ya Tanzania hasa Rais Samia Suluhu Hassan anayeshikilia hatma ya nchi ili aendelee kuliongoza taifa vyema. Pia amesema serikali itaendelea kushirikiana na taasisi za dini katika kuleta maendeleo ya nchi. Pia ameomba viongozi wa dini kuliombea taifa katika kipindi hiki cha uchaguzi ili tendo hilo la kidemokrasia lifanikiwe huku wakiwahamasisha waamini wao kushiriki kikamilifu bila kushinikizwa na mtu au taasisi yoyote. Amesisitiza viongozi wa serikali kuendelea kushirikiana na viongozi wa dini katika kudumisha umoja, amani na mshikamano nchini Tanzania.

Askofu Msaidizi Bududu akisalimiana na baadhi ya Maaskofu
Askofu Msaidizi Bududu akisalimiana na baadhi ya Maaskofu

Wakati huo huo, Jumamosi, tarehe 23 Mei 2025 Askofu msaidizi Josephat Bududu aliyechaguliwa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko mnamo tarehe 26 Februari 2025 kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora amekiri Imani na kula kiapo katika Masifu ya kwanza ya jioni, katika mkesha wa kuwekwa wakfu yaliyofanyika tarehe 24 Mei 2025 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu Jimbo Kuu Katoliki Tabora. Kabla ya Masifu hayo ya jioni Askofu Msaidizi Mteule Bududu alipokelewa kutoka katika Parokia ya Sikonge kwa maandamano makubwa ya watu wa Mungu kutoka Jimbo kuu la Tabora na kufanya kituo kwenye Parokia ya Mtakatifu Yosefu Mfanyakazi Kipalapala, ambapo aliwahi kuwa Paroko wa Parokia hiyo kwa takriban miaka mitano. Waamini wa parokia hiyo walimkaribisha kwa nyimbo, vigelegele vya shangwe, vifijo na nderemo wakiongozwa na Paroko msaidizi wa Parokia hiyo Padri Andrea Mziga ambaye alitoa neno la shukrani kwa Askofu Mteule Bududu akisema kuwa miaka mitano iliyopita Parokia hiyo ilimpokea kwa shangwe kama Paroko wao na tarahe 24 Mei 2025 wanamuaga kwa shangwe kwakuwa amekuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Tabora.

Askofu Msaidizi Bududu akilakiwa kwa shangwe uaskofuni
Askofu Msaidizi Bududu akilakiwa kwa shangwe uaskofuni

“Sisi wanaparokia wa Parokia ya Yosefu Mfanyakazi Kipalapala ndiyo wazaa chema kwani umetumikia hapa kama Paroko kwa miaka takribani mitano. Tunakushukuru kwa utume wako wa kutuchunga sisi kondoo wako kwa upole, wema, unyenyekevu na ushirikiano. Tunakusindikiza kuelekea Jimboni kwa sababu hutaadhimisha tena misa hapa kama Padri tu bali kama Askofu, ukiwa na jukumu la kuwaongoza, kuwatakatifuza na kuwafundisha watu wa Mungu." Kwa upande wake, Askofu Mteule Josaphat Bududu aliwashukuru waamini hao wa Parokia ya Mtakatifu Yosefu Kipalapala kwa ushirikiano wao alipokuwa Paroko wao hadi alipoteuliwa kuwa Askofu Msaidizi. “Tulishirikiana na kufanya kazi kwa pamoja na Paroko Msaidizi Andrea Mziga, watawa hasa Shirika la Mabinti wa Maria, kamati tendaji pamoja na waamini wote. Nawashukuru pia Mapadri wa Seminari Kuu ya Kipalapala kuanzia Gambera Hermani Kachema, watawa na waseminari wote kwa ushirikiano, kusaidia katika kukua kwa ajili ya kazi za kichungaji ndani ya Kanisa,” alisema Askofu Mteule Bududu.

TEC imempongeza na kumshukuru Askofu Mstaafu Paulo Ruzaka
TEC imempongeza na kumshukuru Askofu Mstaafu Paulo Ruzaka

Ndipo Msafara wa mapokezi ukaelekea Jimboni na kupokelewa na Kardinali Protase Rugambwa, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Tabora, Askofu mkuu Angelo Accatino, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, Askofu Wolfgan Pisa OFM Cap, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, Maaskofu, Mapadre, watawa na waamini kutoka ndani nan je ya Jimbo kuu la Taobora. Kardinali Rugambwa alimkaribisha Askofu Mteule akawakaribisha waamini wote waliokuwa kwenye msafara wa maandamano. Kisha Askofu Mteule Bududu akatoa baraka. Majira ya saa kumi jioni Ibada ya Masifu ya jioni ilianza na Askofu Christopher Ndizeye wa Jimbo Katoliki Kahama. Kabla ya Masifu kuanza Askofu mkuu Angelo Accatino alimtambulisha Askofu mteule kwa wanajimbo la Tabora kisha kuonesha hati ya uteuzi wake na kuibabidhi kwa Askofu Mteule Msaidizi Josaphat Bududu ambaye alimwonesha Kardinali Protase Rugambwa na Katibu wa Jimbo.

Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu wa Jimbo kuu la Tabora
Askofu Msaidizi Josaphat Jackson Bududu wa Jimbo kuu la Tabora

Kisha Katibu wa Jimbo akathibitisha kwa waamini uhalali wa hati hiyo. Askofu Ndizeye katika mahubiri yake waliwataka waamini wa Jimbo kuu la Tabora   kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Askofu msaidizi Bududu waliyopewa na Mungu.” Askofu Bududu ni zawadi kwa wana Tabora na zawadi kwa Kanisa Katoliki Tanzania na kwa Kanisa la Kiulimwengu. Tunampongeza pia yeye kwa kukubali kupokea utume huo,” amesema. Anaeleza kuwa, Askofu msaidizi Bududu ametumwa kwenda kutangaza matendo makuu ya Mungu katika Daraja Takatifu ya Uaskofu hivyo wajibu wa waamini ni kumsikiliza, kumpa ushirikiano na kumwombea katika kuishi yale aliyoyatamka katika kiri ya imani na kiapo cha uaminifu. Mambo hayo ni mazito lakini kupitia sala ataweza kuyatekeleza hata katika ugumu wake. Mdo 14:22. “Askofu msaidizi Bududu atafanya pamoja nasi na kwa ajili yetu kazi ya uchungaji hivyo tuwe tayari kushirikiana naye kwa upendo katika ukweli na haki ili mapenzi ya Mungu yaweze kudhihirika kupitia maisha na utumishi wake,” amehitimisha Askofu Ndizeye. Kisha Askofu msaidizi Josaphat Bududu alikiri Kanuni ya Imani na kula kiapo cha utii akisindikizwa na Maaskofu mashahidi wawili ambao ni: Askofu wa Jimbo Katoliki Kigoma Joseph Roman Mlola ALCP/OSS na Askofu msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma Wilbroad Henry Kibozi.

Askofu Msaidizi Bududu
26 Mei 2025, 15:25