MAP

Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Jumatatu tarehe 14 Aprili 2025 amebariki “Sanamu ya Bikira Maria Rosa Mystica” na kuwekwa kwenye Bustani ya Vatican. Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Jumatatu tarehe 14 Aprili 2025 amebariki “Sanamu ya Bikira Maria Rosa Mystica” na kuwekwa kwenye Bustani ya Vatican.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Sanamu ya Bikira Maria Rosa Mystica Iko Bustanini Vatican

Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Jumatatu tarehe 14 Aprili 2025 amebariki “Sanamu ya Bikira Maria Rosa Mystica” na kuwekwa kwenye Bustani ya Vatican. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi wakuu wa Vatican akiwemo Askofu mkuu Emilio Nappa, Katibu mkuu wa Serikali ya Vatican. Ufunuo wa Bikira Maria Rosa Mystica na Bikira Maria Mama wa Kanisa yameunganishwa pamoja huko Brescia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa tarehe 5 Julai 2024 liliridhia mambo chanya kwa upande wa imani na maadili yaliyotokana na ufunuo wa "La Rosa Mistica di Fontanelle" au "Madonna di Montichiari” kwa Pierina Gilli. Kwa kupitia tena tamko lake la awali lililochapishwa kunako mwaka 1984, Baraza likatangaza kwamba, ujumbe wa Bikira Maria "Rosa Mystica" yaani "Waridi lenye fumbo" kwa Pierina Gilli hauna mambo yanayokwenda kinyume na Mafundisho ya Kanisa, ingawa bado kulihitajika ufafanuzi wa kitaalimungu. Pierina Gilli alizaliwa tarehe 3 Agosti 1911 kutoka katika familia maskini; akabahatika kufanya kazi kama mlinzi wa nyumba, muuguzi hospitalini na katika maisha yake, akabahatika kupata ufunuo wa ujumbe wa Bikira Maria. Pierina Gilli alionesha unyenyekevu mkubwa, akahifadhi shajara za uzoefu na mang’amuzi ya ufunuo wa Bikira Maria. Pierina aliishi maisha ya faragha sana na hatimaye, alifariki dunia tarehe 12 Januari 1991 huko Montichiari, katika eneo la Boschetti baada ya: toba, wongofu wa ndani na utakaso wa muda mrefu wa mwili na roho.

Sanamu ya Bikira Maria Rosa Mystica
Sanamu ya Bikira Maria Rosa Mystica

Bikira Maria alimtokea Pierina kwa mara ya kwanza kunako mwaka 1947 akiwa amevaa mavazi ya: Zambarau na vazi jeupe: kielelezo cha huzuni na machozi machoni pake, akionesha huzuni na kwamba, Bikira Maria aliomba sala, toba na wongofu wa ndani kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Tarehe 13 Julai 1947, Bikira Maria alimtokea tena Pierina akiwa amevaa mavazi meupe, akiwa na mawaridi matatu: Jeupe, jekundu na lenye rangi ya dhahabu: Kielelezo cha sala, dhabihu na toba, huku akiomba kwamba, tarehe 13 Julai ya kila mwaka iadhimishwe ibada kwa ajili ya toba ili kulipia gharama ya dhambi zilizotendwa na watu waliowekwa wakfu. Bikira Maria alimtokea tena mwaka 1966 matukio haya yakawa ni chemchemi ya toba, wongofu wa ndani na uponyaji.

Uzinguzi wa Sanamu ya Bikira Maria Rosa Mystica
Uzinguzi wa Sanamu ya Bikira Maria Rosa Mystica   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ni katika muktadha huu, Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, Jumatatu tarehe 14 Aprili 2025 amebariki “Sanamu ya Bikira Maria Rosa Mystica” "Waridi lenye fumbo" na kuwekwa kwenye Bustani ya Vatican. Tukio hili limehudhuriwa na viongozi wakuu wa Vatican akiwemo Askofu mkuu Emilio Nappa, Katibu mkuu wa Serikali ya Vatican. Ufunuo wa Bikira Maria Rosa Mystica na Bikira Maria Mama wa Kanisa yameunganishwa pamoja katika eneo la Fontanelle, lililoko huko Brescia. Bikira Maria alijidhihirisha, akihimiza maisha ya sala, toba na mateso mintarafu rangi: nyeupe, nyekundu na njano za mawaridi yaliyokuwa kwenye vazi la Bikira Maria. Ujenzi wa Madhabahu ya Bikira Maria Rosa Mystica ulianza mwaka 1966 na huko kuna Kanisa kwa ajili ya Ibada kwa Ekaristi Takatifu na Kikanisa kidogo kinachotunza ufunuo wa Bikira Maria Rosa Mystica, "Waridi lenye fumbo."

Bikira Maria
14 Aprili 2025, 14:10