Kikanisa Cha Kwanza Cha Kuabudia Damu Azizi ya Yesu Chazinduliwa Dar Es Salaam
Na Veneranda Malima, - Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Tanzania.
Ibada kwa Damu Azizi ya Kristo Yesu, Mto wa rehema, shule ya utakatifu, haki, upendo, upatanisho na msamaha wa kweli ni chemchemi ya upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu. Hii ni Ibada ambayo inaenezwa kwa namna ya pekee kabisa na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., Shirika la Masista Waabuduo Damu Azizi ya Yesu, ASC, Mashirika ya Kitawa pamoja na waamini walei walioko kwenye utume wa Damu Azizi ya Yesu, sehemu mbalimbali za dunia. Fumbo la upendo wa Kristo Yesu limekuwa ni kivutio kikubwa cha waamini na waanzilishi wa Mashirika ya Kitawa kama vile Mtakatifu Gaspari del Bufalo na Mtakatifu Maria de Mathias, kiasi kwamba, fumbo hili la upendo na huruma ya Mungu limekuwa ni msingi wa maisha na utume wa Mashirika haya. Damu Azizi ya Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu wa ulimwengu na kwamba, ni alama ya juu kabisa inayoshuhudia upendo na sadaka ya maisha kwa ajili ya wengine. Sadaka hii inajirudia tena na tena katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, chanzo na kilele cha maisha na utume wa Kanisa, kiasi cha Kristo Yesu kuwakirimia waamini Mwili na Damu yake Azizi; Damu ya Agano Jipya na la milele, iliyomwagika kwa ajili ya maondoleo ya dhambi, maisha na uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kujitambua kama watu waliotiwa muhuri ili kushiriki katika utume wa Kristo Yesu, ili waweze kuwa ni mwanga na baraka inayofufua na kupyaisha; mwanga unaoponya na kumweka mtu huru; tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao.
Ni katika muktadha wa kukuza na kudumisha Ibada ya Kuabudu Mwili na Damu Azizi ya Kristo Yesu, Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwa'ichi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam O.F.M.Cap., tarehe Mosi, Machi 2025 amezindua Kikanisa la kuabudia Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo katika Parokia ya Mtakatifu Gaspari Del Bufalo eneo la Mbezi Beach, Jimbo Kuu la Dar es Salaam ambapo pia ni Kituo cha Hija.Katika mahubiri ya uzinduzi huo ulioshuhudiwa na watu wa Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo kuu la Dar es Salaam, Askofu mkuu Ruwa’ichi amewaasa waamini kutambua thamani ya Kikanisa hicho ambacho ni cha kwanza kuanzishwa nchini Tanzania na hivyo kuwataka wawe na heshima, ibada, imani na uadilifu wa hali ya juu wanapoingia kuabudu Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo. Askofu mkuu Ruwa’ichi amesema kwa mazoea Yesu wa Ekaristi amekuwa akiabudiwa katika maumbo ya “Mwili” pekee lakini yakihesabiwa sawa na Mwili na Damu Azizi ikiwa ni ukumbusho kwamba sisi binadamu tumekombolewa kwa Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo. “Hapa katika Parokia ya Mtakatifu Gaspari, mmependa kumwabudu Yesu Kristo katika maumbo ya Mwili na Damu … nawapongeza sana”, amesema Askofu mkuu Ruwa’ichi na kuongeza kuwa Yesu Kristo anapaswa kuabudiwa, kuheshimiwa na kutukuzwa. Pamoja na waamini, kupata fursa ya kuabudu katika Kikanisa hicho cha kuabudia Damu na Mwili wa Yesu, Askofu mkuu Ruwa’ichi ametoa maagizo ya kuboresha mahali palipowekwa Damu Azizi ya Yesu ili uwekwe uzio imara wa kioo kisichovunjika na pia pawe na mlango wa mtu anayeruhusiwa kufungua mahali hapo.
Aidha, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amefafanua na kuwataka waamini wazingatie kwamba, Kikanisa hicho cha kuabudia Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo hakipaswi kutumika kwa ajili ya ibada ya Misa Takatifu au kuimba bali ni kwa ajili ya tafakari ambapo kila mmoja anapaswa kusali, kuabudu na kumshirikisha Kristo Yesu ili: Amlinde, ambariki na amtakatifuze ili kuufikia Ufalme wa mbinguni unaosimikwa katika: kweli na uzima, utakatifu na neema; haki, mapendo na amani. Licha ya kuzindua Kikanisa la kuabudia Mwili na Damu Azizi ya Yesu, Askofu Mkuu Ruwa’ichi amezindua pia Pango la Bikira Maria na nyumba ya Mapadre iliyofanyiwa ukarabati mkubwa. Naye Mheshimiwa Padre Vedasto Ngowi, C.PP.S., Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Tanzania amesema kuwa kabla ya kuridhia kuzindua Kikanisa cha kuabudia Damu Azizi na Mwili wa Yesu, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alimwelekeza atoe Katekesi ya kuwaelimisha waamini maana ya Ibada ya kuabudu Mwili na Damu Azizi ya Yesu, agizo ambalo amebainisha kwamba alilitekeleza parokiani hapo na kuongeza kwamba, kwa sasa maelezo hayo yamewekwa kwenye maandishi katika Kikanisa hicho cha kuabudia Mwili na Damu Azizi ya Kristo ili kila mwamini anayeingia kwa mara ya kwanza aweze kuyasoma, kuyaelewa na kuyamwilisha kama sehemu ya mchakato wa safari ya imani.
Padre Ngowi amenukuu maneno ya Mtakatifu Yohane wa XXIII kwenye Waraka wake wa Kitume “Inde a primis” wa Mwaka 1960 akisema kwamba, huu ni mwaliko kwa waamini kujikita katika uchaji na tafakari ya kina juu ya Damu Azizi ya Kristo Yesu “bei ya fidia yetu, dhamana ya wokovu na uzima wa milele.” Damu Azizi iliyomwagika ni ishara na onesho la maisha yanayoyotolewa kwa njia ya umwagaji damu kama ushuhuda wa upendo mkuu, tendo la unyenyekevu wa Kimungu, kuelekea hali yetu ya kibinadamu. Mwenyezi Mungu alichagua ishara ya damu, kwa sababu hakuna ishara nyingine iliyo fasaha sana kuonesha uhusika kamili wa watu wake. Rej. Mahubiri ya Mtakatifu Yohane Paulo II, 1 Julai 2000. Ibada ya Ekaristi Takatifu isiishie kwenye kutoa heshima bali ifikiriwe kuabudu kwa kujua ukombozi upo pale. Amesema anaamini na kutumaini kwamba, kupitia Kikanisa hicho cha kuabudia Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo, imani itakolea na kumwilishwa kwa kuzingatia thamani ya wokovu kwa njia ya sala, shukrani au kuabudu tu.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Bwana Simon Njau kwa niaba ya Paroko Padre Thadei Memba, C.PP.S., amesema Historia ya Kanisa la kuabudia Mwili na Damu Azizi ya Yesu Kristo katika Kituo cha Hija cha Mtakatifu Gaspari Del Bufalo, Jimbo kuu la Dar es salaam ilianza mwaka 1990 kilipoanzishwa Kigango cha Maria De Mattias (eneo lililoitwa wakati huo Mbezi Machakani) na Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ambao walipanga itakapofika Jubilei ya Miaka 50 tangu Mtakatifu Gaspari del Bufalo atangazwe kuwa Mtakatifu waombe kujenga Kituo cha Hija. Muda huo ulipofika, mwaka 2001 walimwomba Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Kardinali Polycarp Pengo (mstaafu) ambaye aliwashauri wajenge Parokia kwa kuwa eneo hilo la Mbezi Beach lilikuwa na uhitaji huo changamoto iliyovaliwa njuga na Padre Domenico Altieri, C.PP.S., Ujenzi ulianza mwaka 2001 na Parokia ya Mtakatifu Gaspari Del Bufalo ilizinduliwa rasmi tarehe 11Machi 2007 na Askofu Mkuu wa Jimbo la Dar es salaam wakati huo Kardinali Polycarp Pengo. Tangu wakati huo chini ya Maparoko mbalimbali, pamekuwa pakiendelezwa kwa ajili kupafanya kuwa eneo la Hija la kuvutia ambapo Kanisa hilo lilitabarukiwa Oktoba 24, 2015. Katika kutimiza ndoto ya Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu ya kuifanya Parokia ya Mtakatifu Gaspari Del Bufalo kuwa Kituo cha Hija na kuweka Pango la Hija, mwaka 2018 ulianza ujenzi wa makazi na vivutio vya kiroho (Vituo vya Njia ya Msalaba, Rozari ya Damu Azizi ya Yesu, Pango la Bikira Maria wa Damu Azizi, Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, Bikira Maria wa Fatima na hatimaye, Kikanisa cha kuabudia Mwili na Damu Azizi ya Yesu.