ĐÓMAPµĽş˝

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa hija ya kitume mjini Vatican Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa hija ya kitume mjini Vatican 

Askofu Stephano Lameck Musomba, OSA, Jimbo Katoliki la Bagamoyo

Askofu Stephano Lameck Musomba OSA, ameteuliwa na Papa Francisko kuwa ni Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Stephano Lameck Musomba alikuwa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Bagamoyo ni Kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria, lililoko mjini Bagamoyo. Jimbo Katoliki la Bagamoyo linakuwa na Parokia 22, Mapadre Jimbo 8, Mapadre watawa 37 na watawa 8.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 7 Machi 2025 ameunda Jimbo Katoliki la Bagamoyo, nchini Tanzania, kwa kuligawa Jimbo kuu la Dar es Salaam na Morogoro na kumteuwa Askofu Stephano Lameck Musomba OSA, kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Stephano Lameck Musomba alikuwa ni Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Bagamoyo ni Kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria, lililoko mjini Bagamoyo. Jimbo Katoliki la Bagamoyo linakuwa na Parokia 22, Mapadre Jimbo 8, Mapadre watawa 37 na watawa 8. Askofu Stephano Lameck Musomba OSA, Kauli mbiu yake ya Kiaskofu ni “Loquere Domine Quia Audit Servus Tuus” yaani “Nena Bwana Kwa Maana Mtumishi Wako Anasikia”. Alizaliwa tarehe 25/9/1969 katika kijiji cha Malonji Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, baba yake ni Lameck Musomba mama yake ni Maria Kandonga. Safari yake kielimu inaanzia katika Shule ya msingi Malonji kuanzia kwaka 1979 hadi mwaka 1985 alipohitimu darasa la saba. Alijiunga na Seminari ndogo ya Maua iliyopo katika Wilaya ya Moshi Vijijini kwa kidato cha kwanza hadi cha sita kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1995. Baada ya hapo alijiunga na Taasisi ya Wasalvatoriani huko Kola Morogoro kwa masomo ya Falsafa na Taalimungu kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 2003 na kutunukiwa Shahada za awali za Falsafa na Taalimungu. Katika safari ya wito alianza kuvutiwa na wito wa kitawa tangu mwaka 1988 na akaenda kupata uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya kitawa katika Shirika la Waagustiniani (OSA) huko Mahanje, Jimbo kuu la Songea. Baada ya hapo alijiunga na upostolanti kuanzia mwaka 1993 hadi mwaka 1998 huko Mahanje na baaadaye huko Morogoro.

Askofu Stephano Lameck Musoma OSA wa Jimbo Katoliki Bagamoyo
Askofu Stephano Lameck Musoma OSA wa Jimbo Katoliki Bagamoyo

Kuanzia mwaka 1998 hadi mwaka 1999 alipokea malezi ya unovisi huko Jimbo kuu la Manila, nchini Ufilipin. Mnamo tarehe 25/9/2002 aliweka Nadhiri za daima katika Shirika la kitawa la Waagustiniani (OSA) na mwaka huo huo tarehe 9/12/2002 alipata Daraja ya Ushemasi katika Taasisi ya Wasalvatoriani ambayo kwa sasa ni Chuo kikuu cha Jordan Morogoro. Alipewa Daraja Takatifu ya Upadri tarehe 24/7/2003 huko Mahanje, Jimbo kuu la Songea. Baada ya Daraja Takatifu ya Upadre aliteuliwa kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Mavurunza kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2004. Baada ya hapo alitumwa kwenda kusomea Elimu ya Mababa wa Kanisa (Patrology) kuanzia mwaka 2004 hadi mwaka 2008 katika Chuo cha "Instutum Patristicum Augustinianum" kilichopo Roma, Italia ambako alitunukiwa Shahada ya Uzamili katika masomo ya Taalimungu akibobea katika Elimu ya Mababa wa Kanisa (Patrology). Baada ya masomo huko Roma kuanzia mwaka mwaka 2008 hadi mwaka 2009 alikuwa Mlezi katika Nyumba ya Shirika la Waaugustiani na Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Jordani Morogoro. Mwaka 2009 alitumwa na Shirika kwenda Jimbo kuu la Manila, nchini Ufilipin kutoa semina mbalimbali kwa Wanovisi, Waprofesi na Wapostulanti.

Papa Francisko akiwa na Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa hija yao ya kitume
Papa Francisko akiwa na Maaskofu Katoliki Tanzania wakati wa hija yao ya kitume   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2015 aliteuliwa kuwa Paroko wa kwanza katika Parokia ya Temboni Jimbo kuu la Dar es Salaam na wakati huo huo akiwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Jordan Morogoro. Mwaka 2015 aliteuliwa tena kuwa Wakili Paroko wa Parokia ya Mavurunza, na Msimamizi wa Jumuiya ya Mtakatifu Monika Mavurunza. Mwaka huo huo aliteuliwa kuwa Paroko wa muda wa Parokia Mtakatifu Ambrose Tagaste Jimbo kuu la Dar es Salaam hadi mwaka 2016. Kuanzia mwaka 2016 hadi mwaka 2019 aliteuliwa kuwa Mlezi na Gambera wa Nyumba ya Malezi ya Mtakatifu Agostino iliyopo Morogoro. Kuanzi mwaka huo 2019 hadi kuteuliwa kwake kuwa Askofu msaidizi amekuwa ni Paroko na Msimamizi wa Jumuiya ya Mt. Monika Mavurunza, Temboni na Mtakatifu Rita wa Kashia. Kuanzia mwaka 2008 hadi mwaka 2021 alihudumu kama Katibu Mwakilishi wa Shirika la Waagustiniani nchini Tanzania. Askofu Stephano Musomba wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo ni mzoefu wa kuongea lugha mbalimbali ikiwemo, Kiswahili, Kiingereza, Kiitalia pamoja na kusoma Kihispania, Kifaransa, Kigiriki, na Kilatini. Tarehe 7/7/2021 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam na kuwekwa wakfu kuwa Askofu tarehe 21 Septemba 2021. Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo tarehe 7 Machi 2025.

Jimbo la Bagamoyo
07 Machi 2025, 11:57