Jubilei 2025:Sanamu ya Bikira Maria wa Fatima itakuwa Roma 12-13 Oktoba 2025!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika fursa ya Jubilei ya Tasaufi ya Bikira Maria, inayotajariwa kufanyika tarehe 11-12 Oktoba 2025, Ofisi ya Baraza la Kipapa kwa ajili ya Uinjilishaji, ilitoa taarifa tarehe 27 Februari 2025 kwamba Sanamu asili ya Mama wa Fatima itakuwa Roma. Picha maarufu ya Bikira, inayojulikana kwa waamini duniani kote na ishara ya “Tumaini lisilokatisha tamaa”, itakuwepo miongoni mwa waamini washiriki wakati wa Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro Dominika tarehe 12 Oktoba 2025, saa 4.30 asubuhi, majira ya Ualya na saa 6.30 masaa ya Afrika Mashariki na Kati, na kuzidi kuimarisha wakati huu wa sala na tafakari. Kuingia katika Uwanja wa Mtakatifu Petro wakati wa maadhimisho hayo ya Ekaristi, hakuhitajiki tiketi ya kuingilia. Usajili wa kushiriki katika hafla ya Jubilei hiyo, tayari umefunguliwa kwenye tovuti na utafungwa tarehe 10 Agosti 2025.
Mara ya 4 Sanamu ya Mama Maria wa Fatima kutoka nje
Hii ni mara ya nne kwa sanamu hiyo asili inaondoka kwenye Madhabahu ya Fatima kuja Roma: kwa mara ya kwanza ilikuwa mnamo 1984 katika Jubilei Maalum ya Ukombozi wakati mnamo tarehe 25 Machi mwaka huo Mtakatifu Yohane Paulo II aliweka wakfu kwa Moyo Safi wa Maria Ulimwenguni; mara ya pili ilikuwa ni ndani Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 na ya tatu, ilikuwa mnamo Oktoba 2013, katika hafla ya Mwaka wa Imani pamoja na Papa Francisko.
Mons.Fisichella:Kupata uzoefu wa ukaribu wa Bikira Maria
Kwa mujibu wa Mwenyekti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, Askofu Mkuu Rino Fisichella alisema: “Kuwepo kwa sanamu asili pendwa ya Mama Yetu wa Fatima kutaruhusu kila mtu kupata uzoefu wa ukaribu wa Bikira Maria. Hii ni mojawapo ya sanamu muhimu za Maria kwa Wakristo ulimwenguni kote ambao, kama Baba Mtakatifu anavyosisitiza katika Hati ya Kutangaza Jubilei ya 2025 ya “Spes non confundit,” wanamheshimu kama "mama mwenye upendo zaidi kati ya mama, ambaye kamwe hawatelekezi watoto wake." Huko Fatima, kiukweli, Bikira aliwaambia wale wachungaji wadogo watatu kile anachoendelea kumhakikishia kila mmoja wetu: “Sitawaacha kamwe. Moyo Wangu Safi utakuwa kimbilio lako na njia itakayo waongoza kwa Mungu,” alisisitiza Askofu Mkuu Fisichella.
Padre Cabecinhas:Sanamu Asili inaacha Madhabahu ya Cova ya Iria kwa Ombi la Papa
Na kwa kutoa maoni, msimamizi mkuu wa Madhabahu ya Fatima, Padre Carlos Cabecinhas alisema: "Sanamu hii inaacha Hekalu la Cova ya Iria kwa namna ya kipekee kabisa na kwa ombi la Mapapa. Katika wakati huu wa Jubilei, Bikira wa Fatima ndiye mwanamke wa furaha ya Pasaka, hata katika nyakati za uchungu ambamo ulimwengu unaishi.” Kwa mara nyingine tena “ Mama aliyevaa mavazi meupe” atakuwa msafiri wa matumaini na, huko Roma, atakuwa pamoja na “askofu aliyevaa mavazi meupe”, kama wachungaji wa Fatima walivyomwita kwa upendo Baba Mtakatifu.”
Sanamu ilichongwa kwa mwerezi wa Brazil mnamo 1920
Sanamu hiyo, kazi ya msanii wa Kireno José Ferreira Thedim ambaye aliiunda mnamo 1920, kawaida huwekwa kwenye Kikanisa cha maonesho lya Madhabahu ya Mama Yetu wa Fatima. Katika mahali hapo, kiukweli, kuanzia Mei hadi Oktoba 1917 Bikira alionekana mara sita kwa watoto mchungaji Lucia dos Santos, mwenye umri wa miaka 10, Giacinta Marto, mwenye umri wa miaka 7, na Francisko Marto, mwenye umri wa miaka 9. Sanamu hiyo ina urefu wa sentimita 104 na ilichongwa kutoka kwa mwerezi wa Brazil, kufuatia maagizo yaliyotolewa na wachungaji watatu. Iliwekwa wakfu kwa heshima mnamo tarehe 13 Mei 1946 na, baadaye, risasi iliyompiga Mtakatifu Yohane Paulo II katika jaribio la mauaji ya 1981 ilipachikwa kwenye taji lake.