Vatican yataka uwepo wa mazungumzo ya amani na utoaji wa misaada huko Congo DRC
Vatican News
Tarehe 7 Februari 2025 kilifanyika Kikao Maalum cha 37 cha Baraza la Haki za Kibinadamu, ambapo Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa, huko Geneva, Uswiss Askofu Mkuu Ettore Balestrero, alitoa hotuba yake akilaani vikali machukizo ya hivi karibuni ya muungano wa waasi wa AFC/M23, ambao waliupiga mji wa Goma huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo(DRC) na sasa unasonga mbele kuelekea maeneo ya karibu ya Bukavu. Askofu Mkuu Ettore alianza kwa kusema kuwa Vatican imesikitishwa sana na kuongezeka kwa ghasia mashariki mwa DRC na inalaani vikali mashambulizi ya hivi karibuni, ambayo yamezidishwa na kutekwa kwa mji wa Goma na muungano wa waasi wa AFC/M23 na kusonga mbele kuelekea mji wa Bukavu.
Mzozo umeleta tishio la maisha na ukiukaji wa haki za binadamu
Kuongezeka huku kwa mzozo kumesababisha hasara kubwa ya kusikitisha ya maisha, na ongezeko la kutisha la ukiukaji wa haki za binadamu. Imesababisha uporaji katika mji wa Goma na miji inayozunguka, na imeongeza idadi kubwa ya watu ambao tayari wamekuwa fukara kutokana na migogoro ya mara kwa mara ambayo imekumba majimbo ya Kivu Kaskazini na Kusini kwa miaka 30 iliyopita. Pia Vatican inasikitisha sana kwamba hata Askari wa kulinda amani, wanaotekeleza majukumu waliyokabidhiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, wameuawa au kujeruhiwa wakiwa kazini. Ili kupunguza mzozo wa kibinadamu - angalau kwa ajili ya utoaji wa misaada ya kibinadamu na uhamisho wa waliojeruhiwa zaidi - uwanja wa ndege wa Goma unapaswa kufunguliwa mara moja, na pande zote zinazohusika zinapaswa kufanya mipango muhimu kwa lengo hili.
Papa Francisko anataka kukomeshwa uhasama na kulinda raia
Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican alisisitiza kuwa “Papa Francisko amezitaka pande zinazozozana kujitolea katika kukomesha uhasama na kulinda raia, akipendekeza kwamba "Mamlaka mahalia na Jumuiya ya Kimataifa kufanya kila linalowezekana kutatua hali ya migogoro kwa njia za amani." Aidha alisema Askofu Mkuu Ettore kuwa “ Vatican inatoa ukaribu, mshikamano na rambirambi kwa familia zote zilizopoteza wapendwa wao katika mgogoro huu. Pia inazikumbusha pande zote kwenye mzozo wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, inazitaka kuheshimu makubaliano ya kusitisha mapigano, inathibitisha uungaji mkono wake kwa Mchakato wa Luanda” vile vile “ inataka kuanzishwa tena mara moja kwa mazungumzo ndani ya mfumo huo, na inakaribisha pendekezo la kuanzisha misheni huru ya kutafuta ukweli.” Kwa kuhitimisha Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican alisema kuwa “M23 inapaswa kusitisha mara moja uhasama wote na kujiondoa katika maeneo yanayokaliwa. Uadilifu wa eneo la DRC lazima uheshimiwe kikamilifu.”