27-29 Januari unafanyika Mkutano wa marais wa Tume za Mawasiliano za mabaraza ya Maaskofu
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Jubilei ya Ulimwengu wa Mawasiliano, ilihitimishwa ambayo ilianza tarehe 24 hadi 26 Januari 2025 na kuwaona washiriki maelfu na maelfu ya wataalamu wa mawasiliano kutoka Ulimwenguni kote wakikusanyika Jijini Roma. Katika fursa hiyo waliweza kukutana, kufanya toba, kupita Mlango Mtakatifu, kukutana na Papa Francisko na hatimaye kufunga kwa misa Takatifu Dominika tarehe 26 Januari katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Ni katika Muktadha huo pia kuanzia siku iliyofuata Jumatatui tarehe 27 hadi 29 Januari 2025 unafanyika Mkutano wa Marais wa Tume za Mabaraza ya Maaskofu kwa ajili ya Mawasiliano na Wakurugenzi wa Ofisi za Kitaifa za Mawasiliano.
Mkutano huu ni sehemu ya Jubilei
Mkutano huu, ni sehemu ya Jubilei ambao unajikita na baadhi mada ambazo mara nyingi wawasilianaji wa Kanisa wanakutana nayo katika kukabiliana hali halisi ya sasa. Kwanza Jumatatu tarehe 27 Januari walikutana na Baba Mtakatifu Francisko ambaye aliwasisitizia wawe wawasilianaji wa upendo kwa wote na kwamba Kanisa lazima litoke nje kwenda kukutana na wengine. Papa alihimiza kujenga mtindo tofauti wa mawasiliano, tofauti katika roho, katika ubunifu, katika nguvu ya kishairi inayotoka katika Injili na isiyokwisha. Kuwasiliana daima ni asili. Tunapowasiliana, sisi ni waundaji wa lugha, wa madaraja. Sisi ndio waumbaji. Mawasiliano ambayo hupitisha maelewano na ni mbadala thabiti wa minara mipya ya Babeli. Papa ameomba kufikiria kuhusu hili kwa muda. Minara mipya ya Babeli kwamba: kila mtu anaongea na haelewani na mwenzake. Kufikiria juu ya ishara hii."
Kwa mujibu wa waandaaji wa Mkutano huu ambao ni Baraza la Kipapa la Mawasiliano, linabainisha kwamba katika ulimwengu unaobadilika kwa kasi kidijitali, Kanisa linajikuta liko mstari wa mbele kukabili mabadiliko ya mara kwa mara; Wawasiliani wanapopitia mahusiano yenye changamoto ya vyombo vya habari, kuongezeka kwa mifumo mipya, na ushawishi wa mitandao ya kijamii, wengi wanajiuliza jinsi gani ya kuunda na kurekebisha mikakati yao ya mawasiliano ili ujumbe wao uweze kuwafikia waamini wa asili zote. Zaidi ya hayo, Kanisa halizuiliki kutokana na migogoro, ubaguzi, taarifa potofu, kutopendezwa na vyombo vya habari vya kilimwengu, udhibiti, na hata mateso ya waamini. Zaidi ya hayo, masuala yanayohusiana na akili mnemba yamezidi kuwa muhimu, na kuongeza safu zaidi ya utata kwa mazingira ya mawasiliano ya Kanisa. Licha ya changamoto, mazingira haya ya vyombo vya habari yanayobadilika yanatoa fursa nyingi kwa wawasilianaji wanaoeneza Habari Njema, na katika mkutano hayo yote yatazingatiwa kwa pamoja!
Washiriki watapata maarifa muhimu kutoka kwa wataalam wa mawasiliano wanaotambulika kimataifa, kubadilishana maoni na uzoefu na wenzao wengine wanaohusika katika mawasiliano ya Kanisa, kushiriki katika warsha na mijadala, kuchunguza mikakati ya kibunifu na mielekeo inayoibuka katika mawasiliano, kusikiliza shuhuda zinazoonesha jinsi mawasiliano yanavyoweza kusababisha kubagua na vile vile mabadiliko chanya katika Kanisa na katika jamii. Kushiriki pia kunawezekana kwa Makatibu Wakuu wa Mabaraza ya Maaskofu au marejeo yoyote mengine kwa ajili ya mawasiliano katika Kanisa mahalia.