Kujifunza historia ili kuishi imani leo hii
Andrea Tornielli
Inasemekana kwamba Mtakatifu Philip Neri alikuwa akimwambia rafiki yake Cesare Baronio, mwanzilishi wa historia ya Kikatoliki: njoo angalau mara moja kwa mwezi kufundisha historia ya Kanisa kwa wanafunzi wetu kwa sababu hawaijui tena, na ikiwa hawaijuhi historia itafikia kwamba hawajuhi tena imani. Umakini huu wa maafunzo ya historia unafaa zaidi kuliko hapo awali na Waraka uliochapishwa na Papa Francisko unaonesha hili kwa uwazi mkubwa. Kama ilivyotokea katika Barua iliyotangulia ya mwezi Agosti iliyopita, iliyojitolea kwa umuhimu wa fasihi, Mrithi wa Petro anazungumza kwanza na makuhani wanaofikiria juu ya mafunzo yao, lakini anaaakisi mada ambayo sio ya kupendeza kwao tu. Kujifunza historia ya Kanisa ni njia ya kuhifadhi kumbukumbu na kujenga siku zijazo. Na ni njia bora ya kutafsiri ukweli unaotuzunguka. Kuelimisha vizazi vichanga ili kuzama zaidi katika siku za nyuma, si kuamini kauli mbiu zinazorahisisha, kuvinjari mamilioni ya "habari" ambazo mara nyingi ni za uongo au angalau zenye upendeleo na zisizo kamili, ni dhamira inayotuhusu sisi sote. Maneno ya Mtakatifu Philip Neri yanasisitiza juu ya uhusiano wa kipekee wa imani ya Kikristo na historia.
Umwilisho, kifo na ufufuko wa Mwana wa Mungu ni tukio ambalo limegawanya historia ya mwanadamu katika sehemu mbili - kati ya kabla na baada. Imani ya Kikatoliki kwanza kabisa sio wazo, falsafa, maadili, lakini ni uhusiano, maisha, ukamilifu, na historia. Sisi ni Wakristo kutokana na ushuhuda ambao umetolewa kutoka kwa mama hadi kwa mwana, kutoka kwa baba hadi binti, kutoka kwa babu hadi kwa wajukuu. Na tukirudi nyuma mnyororo huu tunawafikia mashahidi wa kwanza, mitume, ambao walishiriki, siku baada ya siku, maisha yote ya hadhara ya Yesu. Upendo huu kwa historia, unaoambatana na mtazamo wa imani, unatufanya tuangalie kwa makini hata kurasa zisizo bora na zenye giza za zamani za Kanisa. "Jifunzeni bila ubaguzi kwa sababu Kanisa halihitaji uwongo bali ukweli tu," alisema Papa Leo XIII alipofungua Nyaraka za Siri ya Vatican mnamo 1889.
Bila shaka, kuzama katika historia kunatuweka katika mawasiliano na "madoa" na "mikunyanzi" ya zamani. Papa Francisko anaeleza kwamba “historia ya Kanisa inatusaidia kulitazama Kanisa halisi ili kulipenda lile lililopo kweli na ambalo limejifunza na linaendelea kujifunza kutokana na makosa yake na anguko lake. Kujitambua hata katika nyakati zake za giza kunalifanya kuwa na uwezo wa kuelewa "madoa na majeraha" ya ulimwengu wa leo. Kwa hiyo mtazamo wa Papa uko mbali sana na wasiwasi wowote wa kuomba msamaha, unaolenga kuwasilisha ukweli uliopakwa sukari; pamoja na mielekeo ya kiitikadi ambayo badala yake inalichora Kanisa kuwa ni lindi la watenda maovu. Kiukweli Kanisa ambalo linajua kweli jinsi ya kukalibisha na kila kasoro ya maisha yake ya nyuma lina uwezekano mkubwa wa kubaki kuwa nyenyekevu kwa sababu linafahamu kwamba ni Bwana anayeokoa ubinadamu, na sio mikakati ya soko la kichungaji au tabia ya mtindo huu au ile ya mtindo ya kisasa.