Waziri Mkuu wa Hispania Akutana na Papa Francisko Mjini Vatican
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa tarehe 11 Oktoba 2024 amekutana na kuzungumza na Bwana Pedro Sánchez Pérez-Castejón, Waziri mkuu wa Hispania, ambaye baadaye amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.
Katika mazungumzo kati ya Baba Mtakatifu Francisko na mgeni wake, wamejadili kuhusu masuala mbalimbali ya Kimataifa; uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Hispania pamoja na masuala msingi, ili kuendeleza majadiliano kati ya Kanisa na Hispania sanjari na watu wote wa Mungu. Mwishoni, viongozi hawa wawili wamejikita katika masuala ya kikanda, mintarafu vita na kinzani za kijamii zinazoendelea “kufuka moshi” na kwamba, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza katika kutafuta, kudumisha sanjari na kulinda amani. Wamegusia pia wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji hususan kwenye Bahari ya Mediterrania na Visiwa vyake.